Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejipanga kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na Italia katika kuendeleza sekta ya madini, hususan kwa kutumia teknolojia na mitambo rafiki kwa mazingira.

Waziri wa Madini, Mh. Anthony Mavunde (Mb), amesema hayo tarehe 06 Januari 2025, alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Italia nchini Tanzania, Mh. Giuseppe Coppola, katika ofisi ndogo za Wizara ya Madini Jijini Dar es Salaam.

Waziri Mavunde amesema, “Rais wetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameifungua nchi yetu kwa kuimarisha mahusiano ya kimataifa kupitia falsafa yake ya 4R. Sisi wasaidizi wake tutaendelea kuhakikisha tunasimamia maono hayo na kujenga mahusiano zaidi na washirika wetu kwa manufaa ya uchumi na wananchi wa pande zote. Zipo fursa nyingi kwenye sekta ya madini nchini kuanzia kwenye utafiti mpaka uongezaji thamani madini. Mazingira ya uwekezaji ni mazuri, hivyo ninawakaribisha sana wawekezaji kutoka Italia kuja kuwekeza Tanzania.”

Kwa upande wake, Mh. Coppola aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano wa dhati na kusisitiza kuwa Italia ina makampuni mengi yanayojikita katika teknolojia na utengenezaji wa mitambo ya kisasa kwa sekta ya madini.

“Mwezi Februari, 2025, tunatarajia kuwa na mkutano wa wafanyabiashara baina ya Tanzania na Italia. Tunatarajia makampuni na wawekezaji katika sekta mbalimbali, hususan madini, kuja kushiriki. Ninaamini mkutano huo utakuwa fursa nzuri kwa wawekezaji kutoka Italia kuona na kuzichangamkia fursa zilizopo nchini Tanzania,” alisisitiza Balozi Coppola.

Waziri Mavunde alionyesha kufurahishwa na mpango huo wa mkutano wa wafanyabiashara, akieleza umuhimu wa uratibu wa kina wa mkutano huo ili kuhakikisha wachimbaji wa madini, wakubwa na wadogo, wanashiriki kikamilifu na kunufaika.

Mkutano huo unatarajiwa kuwavutia kampuni za Italia zinazobobea katika utengenezaji wa vifaa vya madini, huku wachimbaji wa Tanzania wakitarajiwa kunufaika kupitia teknolojia na mitambo ya kisasa inayozingatia utunzaji wa mazingira.