Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) imeeleza kuwa inaendelea na uratibu wa ushiriki wa Tanzania katika Maonesho ya Expo 2025 Osaka, yatakayofanyika kuanzia 13 Aprili hadi 13 Oktoba, 2025, katika jiji la Osaka, Japan.

Aidha TanTrade inasema kuwa ushiriki wa Tanzania utaelekezwa katika kutangaza fursa mbalimbali zilizopo nchini, ikiwemo sekta za Afya, Nishati, Madini, Utalii, Kilimo, Uchumi wa Buluu, Sanaa, Utamaduni, na juhudi za Serikali za kuwezesha uwekezaji na biashara, ikiwemo miradi ya kimkakati ya ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli, viwanja vya ndege, pamoja na nishati ya umeme na gesi.

Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Bi. Latifa M. Khamis, alieleza hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa mamlaka hiyo leo, Machi 13, 2025, katika ofisi za Idara ya Habari – MAELEZO, jijini Dodoma.

Bi. Khamis amesema kuwa jumla ya program nane zimepangwa kufanyika wakati wa maonesho, ambapo makundi mbalimbali yatashiriki.

Amezitaja Programu hizo ni Utalii 25 Aprili hadi 6 Mei, 2025,Miundombinu: 15 hadi 26 Mei, 2025,Kilimo, Mifugo, Uvuvi, na Uchumi wa Buluu: 5 hadi 16 Juni, 2025,Afya: 20 Juni hadi 1 Julai, 2025,lugha ya Kishwahili na Utamaduni: 1 hadi 7 Julai, 2025,Uwezeshaji Wanawake: 1 hadi 12 Agosti, 2025,Nishati: 17 hadi 28 Septemba, 2025 na Sayansi na Teknolojia: 2 hadi 12 Oktoba, 2025

Amesema faida kuu za Tanzania kushiriki katika maonesho ya Expo 2025 ni pamoja na kufungua fursa za biashara na masoko ya bidhaa zinazozalishwa nchini, kuvutia wageni watalii, kutangaza miradi ya maendeleo inayohitaji mitaji, wabia na wawekezaji, na kuimarisha mahusiano ya kiuchumi na kidiplomasia kati ya Tanzania na nchi nyingine zinazoshiriki.

Aidha, kutakuwa na fursa kwa makampuni kujitangaza, kunadi bidhaa na huduma zinazozalishwa nchini, na kutangaza Kiswahili, mila, utamaduni, na desturi za Watanzania.

Pia, amesema kuwa TanTrade imefanikiwa kuimarisha uwezo wake wa kujiendesha kwa kuwekeza katika ujenzi wa kumbi mpya tatu zenye hadhi ya kimataifa, pamoja na vifaa vya maonesho vyenye thamani ya shilingi 457,625,000 katika eneo la Mbarouk Mwandoro Square.

Mkurugenzi huyo pia ameeleza kuwa nchi zinazoshiriki katika Expo zimeongezeka kutoka 17 hadi 28, huku idadi ya watembeleaji wa maonesho ikifikia zaidi ya 300,701 pamoja na Ajira za muda mfupi kuongezeka kutoka 11,200 hadi 11,869, na mauzo ya papo kwa papo yamefikia shilingi bilioni 3.62.

Aidha, fursa za mauzo kupitia maonesho zimefikia thamani ya shilingi bilioni 25.16, huku mikataba ya kibiashara yenye thamani ya shilingi bilioni 176 ikisainiwa, ikiwa ni ongezeko kubwa kutoka shilingi bilioni 5.6.

Mkurugenzi huyo pia ameeleza mafanikio yaliyopatikana kupitia maonesho mengine kama Maonesho ya Mbogamboga Expo Doha 2023/24, ambapo kampuni 13 zilishiriki na kufanikisha mauzo ya papo kwa papo ya shilingi milioni 370, huku fursa za mauzo za shilingi milioni 125 zikitokana na mazungumzo ya kibiashara.

Katika kuendeleza uwezo wa wafanyabiashara, TanTrade imeendelea kutoa mafunzo na ushauri kwa sekta binafsi, hususan wafanyabiashara wadogo na wa kati, ili kuwawezesha kushindana katika masoko ya ndani na nje. Jumla ya programu 37 za mafunzo zimeratibiwa, zikihusisha wafanyabiashara 3,556.

Katika kipindi cha miaka minne, mafanikio mengine ni pamoja na kliniki za biashara ambapo wafanyabiashara 3,256 walihudumiwa, changamoto 1,324 ziliwasilishwa na 1,298 kutatuliwa. Pia, kampuni 482 zilipatiwa msaada wa usajili kupitia taasisi wezeshi kama BRELA, BPRA, na TRA, na kampuni 137 zilisaidiwa kupata ushauri kuhusu alama za ubora, vifungashio vya kimataifa, na mbinu za kuongeza thamani ya bidhaa.

Mkurugenzi huyo pia alieleza mafanikio 7yaliyopatikana kupitia mifumo ya Taarifa za Biashara na Masoko. Mfumo wa TanTrade Biashara App umepata watumiaji 1,460, huku TanTrade Portal ikiwa na watumiaji 92,403. Biashara 36 za Kitanzania zimesajiliwa katika Shirikisho la Kimataifa la Vituo vya Biashara (WTPF), na ripoti 25 za bei za masoko zimesambazwa kwa wadau 179,728.