Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Mary Maganga leo amefungua warsha ya Mafunzo ya Kikanda kuhusu Mpango wa Matumizi ya Eneo la Bahari (Marine Spatial Planning – MSP) na Ukanda wa Pwani ya Magharibi mwa Bahari ya Hindi katika Hotel ya Protea iliyopo mjini Dar es salaam.
Amesema lengo la Warsha hiyo ni kujenga uwezo wa wataalamu kutoka nchi wanachama wa Mkataba wa Nairobi katika kuandaa na kutekeleza Mpango wa Matumizi ya eneo la Bahari, Usimamizi wa taarifa za Kimazingira, kubadilishana uzoefu na kufahamu hatua zilizofikiwa na nchi wanachama katika kuandaa na kutekeleza mpango wa Matumizi ya eneo la Bahari.
Maganga amesema Tanzania ni mwenyeji wa kikao kazi hicho kinachohusisha wajumbe kutoka zaidi ya nchi 10 wanaotekeleza Mkataba wa Nairobi unaohusu Hifadhi, usimamizi na uendelezaji wa Mazingira ya Bahari na Ukanda wa Pwani ya Magharibi.
“Warsha hii imehusisha nchi wanachama wa Mkataba wa Nairobi na nchi zinazoshiriki ni pamoja na Tanzania, Komoro, Kenya, Somalia, Madagascar, Mauritius, Msumbiji, Shelisheli, Re-Union na Afrika Kusini “Alisisitiza Bi. Maganga.
Amesema warsha hii itasaidia kuja na mpango na usimamizi endelevu wa matumizi ya rasilimali za bahari ikiwa ni pamoja na mgawanyo sahihi wa matumizi ya bahari. Bi. Maganga amesema Tanzania inajipanga mapema katika kuandaa mpango huo kwa kuzingatia kuwa uchumi wa bluu ni miongoni mwa agenda za dunia.
“Ninapozungumzia uchumi wa bluu ninasisitiza usimamizi endelevu na shirikishi wa mifumo ikolojia ya Pwani na bahari ya Tanzania ili kuendelea kutoa bidhaa na huduma muhimu ikiwa ni pamoja masuala ya uvuvi na uchimbaji wa mafuta na gesi pale vitakakapogundulika”Alisisitiza Bi. Maganga
Warsha ya Mafunzo ya Kikanda kuhusu Mpango wa Matumizi ya Eneo La Bahari (Marine Spatial Planning – MSP) Na Ukanda wa Pwani Magharibi mwa Bahari ya Hindi na Kujenga Uwezo Katika Usimamizi wa Taarifa za Mazingira imeanza leo tarehe 28 Novemba na inatarajia kukamilika 1 Disemba 2022. Warsha hii inafanyika katika Hotel ya Protea Jijini, Dar es Salaam.