Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Christopher Sayi, amesema Serikali imeanzisha mradi mkubwa wa maji katika Jiji la Dar es Salaam na utakapokamilika, kwa miaka 15 ijayo Jiji hili halitakuwa na shida ya maji.
Mipango ya mradi huo ni pamoja na uchimbaji wa visima 20 katika Bonde la Kimbiji na Mpera, kujenga bwawa huko Kidunda nje kidogo ya Jiji na kupanua chanzo cha maji cha Ruvu Chini. “Serikali imeshatenga fedha kwa ajili ya mradi huo,” Sayi alisema.
Kazi ya kulaza bomba la inchi 71 umbali wa kilometa 60 kutoka Ruvu Chini hadi Dar es Salaam, imeanza Januari 2012. Bomba hili litafanya kazi sambamba na bomba la inchi 54 lililopo sasa.
Sayi alisema kwa sasa kiwango cha maji kinachozalishwa kinaweza kuwatosheleza asilimia 55 ya wakazi wa Dar es Salaam, lakini kiasi hicho chote hakiwafikii wananchi kwa ukamilifu kutokana na uvujaji. Wakati maji yanapofika Dar es Salaam yanapungua kutoka lita za ujazo milioni 300 hadi milioni 168.
“Uvujaji huo unapunguza jitihada zetu; ni hasara kubwa ambayo hatuwezi kuimudu,” alisema Sayi, na kuongeza kuwa hali iliyopo sasa haiwezi kuvumilika.
Washirika wa maendeleo wa kimataifa wamekuwa wakiisaidia Tanzania kugharamia mradi huo, ikiwa ni pamoja na Ushirikiano wa Changamoto za Milenia (MCC), India na mfuko wa wafadhili.
Kwa sasa Jiji linahitaji lita milioni 480 za maji kila siku. Kiwango cha uzalishaji kila siku kitaongezeka na kufikia lita milioni 710 baada ya mradi huu kukamilika, Sayi alisema.
Licha ya upanuzi wa miundombinu, Dar es Salaam inaweza pia kuwa na upungufu wa maji katika miaka michache ijayo kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu, kwa mujibu wa taarifa zinatokana na utabiri rasmi.
Aliyekuwa Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Gerson Lwenge, aliliambia Bunge Aprili mwaka huu kuwa kuboreshwa kwa usambazaji wa maji kunatarajiwa kutosheleza ongezeko la idadi ya watu hadi mwaka 2025.
Hata hivyo, baadhi wanatabiri kwamba idadi ya watu wa Dar es Salaam itaongezeka kutoka watu milioni 4 hadi milioni 10 kwa kipindi cha chini ya miaka kumi. Kwa hiyo, Mbunge wa Kinondoni, Idd Azzan, aliwaambia wabunge Aprili 15 kuwa kasi ya watu kuingia Dar es Salaam ni kubwa kuliko hata uboreshaji huo.
Mipango ya serikali ni kujenga bwawa jingine katika chanzo cha maji cha Ruvu Juu ifikapo mwaka 2025 litakalowezesha usambazaji wa maji ya kutosheleza zaidi ya mwaka huo, alisema Sayi.
Juma Mfinanga, ambaye ni daktari, alisema habari ya kupatikana maji ni njema kwa hospitali zote za Dar es Salaam, kwani maji yana kazi kubwa katika hospitali zote nchini.
Anasema tiba bila maji haiwezekani kwani wagonjwa waliopata ajali, wenye vidonda na magonjwa yasiyomithilika, tiba namba moja ni kuwafanyia usafi na huwezi kufanya usafi bila maji.
“Maji yanasaidia kuepusha uhamishaji wa magonjwa kutoka kwa mgonjwa kwenda kwa mgonjwa au mgonjwa kwenda kwa daktari na kusambazwa zaidi… chukulia watu waliopata ajali. Wakifika hospitalini wanakuwa na vumbi na matope, hivyo kitu cha kwanza ni kutumia maji kuwasafisha kisha ndipo tunaanza kuwapa dawa,” aliliambia Gazetila JAMHURI.
Anasema maji yanapaswa kupatikana wakati wote kwa ajili ya kusafishia vyoo, wodini, ufuaji na kusaidia katika usafi binafsi wa wagonjwa. “Maji yanapokosekana, hospitali husimamisha huduma zote ikiwamo upasuaji,” anasema.
Naye Jonas Kamaleki, mkazi wa Dar es Salaam, anasema ana wasiwasi kama serikali itaweza kutimiza ahadi yake. “Tatizo ni kuwa serikali yetu inaahidi mengi. Mwaka jana tuliahidiwa kuwa mgawo wa umeme ungemalizika mwezi Desemba, lakini bado leo tunao mgawo wa kimya kimya,” Kamaleki ameiambia JAMHURI.
Kamaleki anasema katika miaka minne iliyopita, wakazi wa Dar es Salaam wanalazimika kuishi bila uhakika wa maji safi. “Tunatumia maji ya chumvi yasiyofaa kwa kunywa wala kuoga. Hali imekuwa mbaya zaidi katika wiki mbili zilizopita, wakati hata yale matone machache ya maji yaliyokuwa yanapatikana mabombani sasa yamekauka.”
Afisa Uhusiano wa Shirika la Maji Safi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASCO), Teddy Mlengu, amesema umma unapaswa kuisaidia serikali kwa kuunga mkono mradi huo na kuachana na dhana potofu.
Mlengu amesema vyombo vya habari pia vina wajibu wa kuuelimisha umma usiharibu miundombinu ya maji.
“Watu wanapaswa kufahamu kuwa nao ni wamiliki wa miundombinu ya maji. Hivi sasa, tuna asilimia 44 ya uvujaji wa maji, na tunakusudia kuupunguza hadi asilimia 32 ifikapo mwakani, lakini sehemu kubwa ya uvujaji huo inasababishwa na wanaoharibu mabomba kwa kujifurahisha tu,” anasema.