Na Mwandishi Wetu, WHMTH, Arusha
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeahidi kuendelea kushirikiana na Umoja wa Posta Duniani (UPU) na Mashirika mengine ya kimataifa kukuza na kuendeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) na ustawi wa jamii yote ulimwenguni.
Ahadi hiyo imebainishwa leo tarehe 13 Juni, 2024, Naibu Katibu Mkuu Bw. Nicholas Merinyo Mkapa akimwakilisha Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Maryprisca Mahundi, katika hotuba ya Ufunguzi wa Mkutano wa Kikanda wa Mkakati wa Dunia wa Maendeleo ya Posta kwa Afrika.
Katika hotuba hiyo, Naibu Katibu Mkuu amesema kuwa, Tanzania imejitoa kwa dhati kuhakikisha kuwa Sekta ya Posta, inaendelea kubaki yenye manufaa, na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kukuza na kuimarisha uchumi wa nchi za Afrika.
“Tanzania inajitoa kwa dhati kuhakikisha kuwa Sekta ya Posta, inaendelea kubaki yenye manufaa, na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kukuza na kuimarisha uchumi wa nchi zetu” alisema Mhandisi Mahundi.
Aidha, washiriki wa mkutano huo na wadau wa sekta ya posta kutoka Afrika na Duniani, wametakiwa kujitoa kwa dhati kufanya kazi ya kujadili Mkakati wa Umoja wa Posta Duniani 2026-2029 unaohusika na maendeleo ya Sekta ya Posta, na kuutekeleza kwa moyo, uwajibikaji na kwa ushirikiano.
“Mchango wenu katika Mkutano huu ni muhimu katika kuhakikisha kuwa majadiliano yenu yanakuwa na matokeo chanya, yatakayokuja na Mpango Mkakati utakaotuongoza kwa wakati ujao” Mhandisi Mahundi aliwaambia wajumbe hao.
Amesema, ana uhakika kuwa, siku mbili za mkutano huo, zitaainisha mtazamo wa pamoja wa kuanzisha Mkakati imara utakaoiweka Sekta ya Posta, mbele ya mawasiliano na biashara Duniani, na kwa namna ya pekee, Ukanda wa Afrika.
Awali akimkaribisha Mgeni Rasmi kufungua mkutano huo, Bi Salome Kessy, aliyemwakilisha Katibu Mkuu Bw. Mohammed Khamis Abdulla, amesema katika siku mbili za mkutano huo, wajumbe watajadiliana kwa kina na kutoa mapendekezo yanayooanisha Mikakati ya Kikanda na mwenendo na uvumbuzi wa Posta Duniani.
Amesema, mambo makuu yanayolengwa katika mkutano huo ni uimarishaji wa utoaji huduma, matumizi ya teknolojia mpya na kuhakikisha huduma za posta Afrika zinakuwa endelevu na himilivu.
Mkutano wa Kikanda wa Kujadili Mkakati wa Dunia wa Maendeleo ya Posta wa Mwaka 2026-2029, kwa Afrika, unaosimamiwa na Umoja wa Posta Duniani UPU, utahitimishwa tarehe 14 Juni, 2024 kwa maazimio yatakayoisaidia Sekta hiyo kusonga mbele kwa mafanikio.