Tanzania imeahidi kuendelea kushirikiana na Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) ili iweze kunufaika zaidi na kazi za Mahakama hiyo yenye hadhi ya juu duniani.
Ahadi hiyo imetolewa leo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Africa Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) wakati wa mazungumzo na Jaji wa Mahakama hiyo, Jaji Abdulqawi Yusuf yaliyofanyika kwenye Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.
Aidha, wamejadili ushirikiano uliopo baina ya Tanzania na Taasisi ya Afrika ya Sheria za Kimataifa yenye Ofisi zake Jijini Arusha ambayo Jaji Abduqlqawi ni Mwenyekiti. Taasisi hiyo imejikita kwenye kutoa mafunzo na kufanya tafiti kwenye masuala yanayohusu Sheria za Kimataifa.
Jaji Yusuf alimhakikishia Balozi Mulamula utayari wa Taasisi hiyo kuendelea kutoa mafunzo kwa watanzania kwenye maeneo mbalimbali yanayohusu Sheria za kimataifa.
Kwa upande wake Balozi Mulamula alieleza kuwa Serikali itaendelea kutekeleza wajibu wake kama kupitia Mkataba wa Uenyeji.
Taasisi ya Afrika ya Sheria za Kimataifa ilianzishwa mwaka 2012 na Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika kwa lengo la kutoa mafunzo na kufanya tafiti kwenye masuala yanayohusu Sheria za kimataifa na Sheria za Umoja wa Afrika na kuvijengea uwezo Vitivo vya Sheria vya Vyuo Vikuu vya Afrika na Wanasheria wa Afrika wanaoshughulika na Sheria za Kimataifa.