Na Magrethy Katengu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

TANZANIA inatarajiwa kuungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Siku ya Haki ya Mtumiaji Duniani Machi 15, 2025 ambapo kitaifa maadhimisho hayo yatafanyika mjini Morogoro yakiongozwa na kauli mbiu isemayo ‘Matumizi endelevu ya rasilimali ambayo ni masuala ya msingi kwa maendeleo ya Taifa’.

Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Jukwaa la Watumiaji Tanzania (TCF) ambaye pia ni Katibu Mtendaji wa LATRA-CCC, Daudi F. Daudi wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

“Kwa mwaka huu maadhinisho haya yatabebwa na kaulimbiu ya “Haki na Maisha Endelevu kwa Mtumiaji “. Maadhimisho haya yanakusudia kuhamasisha matumizi salama na endelevu ya rasilimali, huku yakitoa jukwaa la majadiliano kati ya Watumiaji, watoa huduma na wadau wa Maendeleo kwa kutoa Elimu ” amesema Daudi.

Daudi kupitia Jukwaa la Watumiaji Tanzania (Tanzania Consumer Forum-TCF) kwa Ushirikiano na The Foundation for Civil Society (FCS) amewatangazia wananchi kushiriki katika maadhimisho hayo muhimu ambayo yatatoa fursa ya kujifunza kuhusu haki za Mtumiaji na jinsi ya kutumia huduma salama.

Amebainisha kuwa maadhimisho hayo yanaadhimishwa kimataifa yakiwa na lengo la kulinda haki za watumiaji na kuhimiza matumizi salama na endelevu ya huduma.

Amesema hiyo ni fursa ya kipekee kwa qananchi kupata elimu kuhusu haki zao, huku Serikali na wadau wa Sekta husika wakihimizwa kuhakikisha huduma bora na za haki zinapatikana kwa wote.

Mtumiaji anapaswa kuwa na nguvu ya kufanya maamuzi sahihi kwa kupata huduma salama, nafuu, na endelevu. Kila mtu ana haki ya kuishi katika jamii inayowajibika kulinda mazingira na rasilimali kwa vizazi vijavyo,” ameongeza Daudi.

Amefafanua kuwa maadhimisho hayo, TCF yanatilia mkazo matumizi salama ya huduma katika Sekta za Nishati, mawasiliano, na usafiri wa anga na mchi kavu.

Amesema Serikali inalenga kuhakikisha kuwa ifikapo 2034, asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia.

“Tusibaki nyuma katika mabadiliko haya. Kutumia nishati safi si tu kwa faida ya leo, bali kwa afya na ustawi wa kesho,” amebainisha Daudi.

Kwa upande wa afisa mawasiliano TCRA CC Mary Msuya amesema usalama wa Mtumiaji mtandaoni ni ajenda muhimu Mwaka huu ambapo TCF itahimiza ulinzi wa faragha na matumizi salama ya huduma za kidigitali, pia usalama katika Sekta ya usafiri wa anga na Nchi kavu utaangaziwa ili kuhakikisha huduma bora Kwa Watumiaji.

Kwa upande wake Afisa Mawasiliano wa FCS Sarah Masenga amesema lengo la maadhimisho ni kuhakikisha wanawapa Wananchi uelewa wa haki zao kwa huduma wanazopatiwa kwani mwananchi ni mdau mkubwa wa maendeleo.

Maadhimisho hayo yameandaliwa na Jukwa la Watumiaji Tanzania (TCF), linalojumuisha mabaraza ya kutetea Watumiaji wa huduma zinazodhibitiwa ambayo ni LATRA-CCC, TCAA-CCC, EWURA-CCC na TCRA -CCC, pamoja na Shirika lisilokuwa la Kiserikali la The Foundation.