Na Zulfa Mfinanga, JamhuriMedia, Arusha
Nchi ya Tanzania imefanikiwa kupanda daraja kutoka kundi B hadi kundi A na kushika nafasi ya 26 duniani, nafasi ya pili barani Afrika baada ya Mauritius na nafasi ya kwanza Afrika Mashariki kwenye ukomavu wa matumizi wa TEHAMA Serikalini.
Akisoma hotuba ya ufunguzi wa kikao kazi cha tano cha serikali mtandao leo jijini Arusha kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais Dkt Philip Mpango amesema matokeo hayo yametokana na utafiti uliofanywa na Benki ya Dunia (WB) mwaka 2022 kuhusu Ukomavu wa Matumizi ya Teknolojia Duniani katika Utoaji wa Huduma za Serikali na ushirikishwaji wa wananchi katika nchi 198 duniani.
Dkt. Mpango amesema ripoti hiyo imebainisha kuwa mafanikio hayo yametokana na utayari wa serikali wa kusimamia kwa karibu matumizi ya TEHAMA katika Taasisi za Umma, uwepo wa Dira mahususi kuhusu Sera ya TEHAMA, Sheria, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao, Mikakati madhubuti na utekelezaji unaosimamiwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA).
![](https://www.jamhurimedia.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/1002490903-1024x957.jpg)
“Dhamira kuu ni kuhakikisha tunaendesha Serikali Kidijitali, na kuwawezesha wananchi kupata huduma za Serikali kwa gharama nafuu, kwa urahisi na mahali popote walipo, na ili kutimiza dhamira hii, Serikali imeandaa mikakati mbalimbali inayotuwezesha kufikia malengo haya ikiwa ni pamoja na Sera ya Taifa ya TEHAMA inayosimamia na kuongoza maendeleo ya sekta ya TEHAMA nchini, pamoja na Mkakati wa Kitaifa wa Uendelezaji wa Miundombinu ya TEHAMA”
“Mikakati mingine ni Mikakati wa Uchumi wa Kidijitali na Mkakati wa Kitaifa wa Serikali Mtandao unaolenga kuwa na matumizi sahihi ya TEHAMA katika utendaji wa Serikali ili kuongeza ufanisi, uwazi, na upatikanaji wa huduma kwa wananchi”
Hata hivyo amewakumbusha na kuwaelekeza wakuu wa taasisi za umma kuzingatia Sheria, Kanuni na Miongozo inayotolewa na Mamlaka husika katika utekelezaji wa jitihada za Serikali Mtandao pamoja na kuhakikisha mifumo ya TEHAMA katika taasisi za umma zinawasiliana na kubadilishana taarifa kidijitali ili kurahisisha utendaji kazi katika taasisi hizo na kuwarahisishia wananchi wanaowahudumia.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Serikali Mtandao Mhandisi Benedict Ndomba ametaja mafanikio kadhaa tangu kuanzishwa kwa Mamlaka hiyo mwaka 2019 ikiwa ni pamoja na ujenzi na matumizi ya rasilimali shirikishi za TEHAMA ukiwemo Mfumo wa Baruapepe Serikalini (GMS) unaotumiwa na taasisi 770.
![](https://www.jamhurimedia.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/1002490906-1024x683.jpg)
Mafanikio mengine ni uwepo wa Mfumo wa Huduma za Serikali kupitia simu za Mkononi (mGov) unaotumiwa na taasisi 429, Mfumo wa Ofisi Mtandao (GeOS) unaotumiwa na taasisi 347 pamoja na Mtandao wa mawasiliano Serikalini (GovNet) ambao umeunganisha ofisi 457 za umma.
“Mafanikio mengine ni ujenzi wa mifumo tumizi ya kisekta na kitaasisi kwa kushirikiana na taasisi husika ikiwemo Mfumo wa Kusimamia Rasilimali Watu Serikalini (New HCMIS,) uliojengwa kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, ambao unatumiwa na taasisi 466 kati taasisi 530, pamoja na Mifumo ya fedha iliyojengwa kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Taasisi zake ambazo ni Mfumo wa Malipo Serikalini (GePG), Mfumo wa Kusimamia Hesabu za Serikali (MUSE), Mfumo wa Kusimamia Mali za Serikali (GAMIS), na Mfumo wa kuwezesha miamala ya Malipo (TIPS)” amesema Mhandisi Ndomba.
Amesema mamlaka imetekeleza maelekezo ya Rais Dkt. Samia kwa kujenga Mfumo unaowezesha Mifumo ya Serikali Kuwasiliana na Kubadilishana taarifa ujulikanao kama Government Enterprises Service Bus (GovESB) ambao umechochea kuongezeka kwa ufanisi wa utendaji kazi katika taasisi za umma na utoaji wa huduma kwa wananchi.
Ametaja baadhi ya taasisi zilizo chini ya sekta hiyo ambazo mifumo yake inawasiliana na kubadilishana taarifa kuwa ni pamoja Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Ofisi ya Taifa ya Mashitaka (NPS), Mahakama na Jeshi la Polisi.
“Mifumo mingine iliyounganishwa na kubadilishana taarifa ni Mfumo wa Ununuzi wa Umma Kielektroniki (NeST), Mfumo wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mfumo wa Leseni za Biashara (BRELA) na Mifumo ya Fedha ya Benki Kuu ya Tanzania (BOT)”
Amesema katika sekta ya elimu Tume ya Usimamizi wa Vyuo Vikuu (TCU) imeunganishwa na mifumo mbalimbali ya Taasisi za Elimu ya Juu na katika sekta ya Afya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umeunganishwa na wadau mbalimbali zikiwemo hospitali binafsi na za Serikali.
Mfumo wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) umeunganishwa na Mifumo ya watoa huduma mbalimbali wa sekta ya umma na binafsi, Mifumo ya sekta ya fedha kupitia Mfumo Mkuu wa Malipo ya Serikalini (GePG) imeunganishwa na mifumo ya taasisi za huduma za kifedha zikiwemo benki na kampuni za simu zote nchini, na Mifumo ya Kusimamia Rasilimali Watu imeiunganishwa na Mifumo ya Wizara ya fedha, Mifuko ya Hifadhi za Jamii na mifumo ya kibenki.