Jumamosi, Oktoba 22, 1966, wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na vyuo vingine jijini waliandamana kwenda Ikulu wakiwa na mabango yaliyoandikwa maneno machafu dhidi ya Serikali ya Awamu ya Kwanza iliyoongozwa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Bango moja liliandikwa: “AFADHALI WAKATI WA MKOLONI.”
Desemba 9, 1961 nchi yetu ilipata Uhuru kutoka kwa Wakoloni Waingereza waliotutawala kwa miaka 43. Wakati tunapata Uhuru kulikuwa na wahandisi 2 na madaktari 12 tu Waafrika (Watanganyika). Asilimia 85 ya watu wazima walikuwa hawajui kusoma wala kuandika. Baada ya Uhuru kupatikana Serikali ikiongozwa na Mwalimu Nyerere ilichukua hatua mbalimbali za makusudi kabisa ili wananchi wapate elimu.
Ubaguzi wa kuwapo kwa shule za Wazungu, Wahindi peke yao na Waafrika kivyao, uliondolewa. Shule za msingi na sekondari ziliongezwa, vyuo mbalimbali vilijengwa; madarasa ya Elimu ya Watu Wazima yalianzishwa kote nchini. Elimu ikatolewa bure tangu shule ya msingi hadi chuo kikuu. Mwalimu Nyerere alipoondoka madarakani mwaka 1985, asilimia 91 ya wananchi walikuwa wanajua kusoma na kuandika na karibu kila mtoto wa Kitanzania alikuwa anaenda shule.
Ukiacha elimu bure, matibabu nayo yakawa bure.  Ili mradi Serikali ilihakikisha wananchi maskini na watoto wao wanafurahia matunda ya Uhuru.
Kama hali ilikuwa hivyo, kwa nini wanafunzi wale wasomi waliandamana na kubeba mabango kuitusi Serikali?
Katika hotuba yake aliyoitoa Jumapili, Oktoba 23, 1966 kutokana na maandamano yale – hotuba iliyopewa kichwa cha habari “TANZANIA ITAJENGWA NA WENYE MOYO”, Mwalimu Nyerere aliwaeleza wananchi nini kilichojiri.
Alianza kwa kusema: “Jana tumewafukuza wanafunzi 393 kutoka vyuo mbalimbali vya Dar es Salaam baada ya maandamano ya kupinga mpango wa Serikali wa “National Service” (Jeshi la Kujenga Taifa, kifupi JKT).
Mwalimu akawaeleza wananchi kwamba nchi nyingi duniani zina “National Service”. Nchini Tanzania Serikali ilianzisha mpango wa aina hiyo kutaka vijana watumike kujenga Taifa lao kwa kipindi cha miaka miwili.
Baada ya mpango huo kuanzishwa, ilibainika kwamba waliokuwa wakijitolea kujiungana Jeshi la Kujenga Taifa walikuwa vijana wenye elimu ndogo ama wasio na kazi. Vijana waliopata elimu ya juu walikuwa hawajiungi. Kwa maneno yake Mwalimu: “…Wenye kitumbua na kazi mahali walikuwa hawaji…”
Kwa hiyo, Bunge likapitisha sheria kwamba kijana yeyote akimaliza masomo ya juu na akimaliza kusomea kazi yoyote, kabla hajaanza kazi lazima ajiunge JKT. Sheria ikatamka kwamba kijana atalipwa posho inayolingana na asilimia 40 ya mshahara ambao angeupata kazini; atapewa kodi ya nyumba na pesa za mavazi. Pesa hizo zote hazitakatwa kodi.
Enzi hizo, mshahara wa kima cha chini (kcc) ulikuwa Sh 180 (zilikuwa zinatosha kwa mahitaji muhimu.) Mshahara wa mwalimu aliyetoka Chuo Kikuu, pamoja na marupurupu ulikuwa Sh 1,320. Kwa hesabu hiyo, malipo ya posho ya kijana mwalimu msomi akienda JKT yalikuwa takriban Sh 790 kwa mwezi – mara 4 ya mshahara wa kima cha chini.
Wasomi wale waliukataa utaratibu huo. Kwenye barua yao waliyomwandikia Rais na kuikabidhi siku ya maandamano, walidai Serikali ilikuwa ikitaka kuwanyonya. Wakalalamika kwamba kwa nini wao tu ndio wahusike kwenye utaratibu huo wa kukatwa pesa zao. Wakataka wenye mishahara minene serikalini nao waingizwe kwenye utaratibu huo.
Wanafunzi  wale walisema, kama Serikali itawalazimisha kwenda JKT, basi wataenda mwili tu, moyo hautakwenda!
Maandamano na madai ya wanafunzi wale yalimkasirisha na kumsononesha sana Mwalimu Nyerere. Katika hotuba yake ile, alisema kwa hasira na uchungu: “….Vijana wanapita mjini na makaratasi yao (mabango) yameandikwa maneno mengi machafu-machafu! Baadaye nilisikiliza redio BBC – redio ya waheshimiwa Waingereza. Nikavizia nisikie nini hasa kilichowapendeza wakakitangaza. Wanasema: Mwalimu Nyerere leo amefukuza wanafunzi wapatao 390 kutoka Chuo Kikuu, na vyuo vingine baada ya vijana hao kuandamana na kusema hawataki masharti ya ‘National Service’, na kusema kwamba “AFADHALI WAKATI WA MKOLONI. Na Waingereza wakarudia maneno yale katika BBC, AFADHALI WAKATI WA MKOLONI! Ndivyo wanavyosema vijana wetu…”
Mwalimu Nyerere akawaeleza wananchi hatua za makusudi zilizochukuliwa na Serikali kuelimisha watu wake baada ya nchi kupata Uhuru, kwa kusema:
“…Tuliingia serikalini mwaka 1960 na kukuta mpango wa wakoloni kujenga Chuo Kikuu cha Tanganyika , labda mwaka 1967 labda! Sisi tukasema tutakijenga na tutakianzisha sasa hivi. Wakasema mtaanzisha wapi majengo hamna. Tukasema lile pale, jengo la TANU. Wakasema, wanafunzi mtapata wapi? Tukasema, vyuo havianzi na wanafunzi elfu, vinaanza na wachache. Tukaanza na wanafunzi 17. Leo vijana wetu wananambia “AFADHALI WAKATI WA MKOLONI!..”
Mwalimu akataja vyuo mbalimbali vilivyojengwa baada ya Uhuru kwa kusema: “…Wananchi, Mkoloni hakujenga Chang’ombe… Si Mkoloni aliyejenga Chuo cha Madaktari (Muhimbili), tumejenga sisi … Mkoloni hakujenga Chuo cha Ufundi, tumekijenga sisi na tumekifungua juzi juzi tu. Vijana wananiambia “Afadhali wakati wa Mkoloni!..”
Mwalimu akasema idadi ya wanafunzi 17 walioanza Chuo Kikuu Dar es Salaam imepanda kufikia wanafunzi 408 mwaka 1966 – ongezeko la mara 24! Idadi ya wanafunzi wote waliokuwa wamekwisha kupata elimu ya juu kutoka vyuo mbalimbali ndani na nje ya nchi kwa kugharimiwa na Serikali ilikuwa imefikia 2,033.
Mwalimu Nyerere aliwaambia wananchi: “…Mkoloni hakujali ujinga wetu, Mkoloni hakujali umaskini wetu, Mkoloni hakujali maradhi yetu. Mkoloni aliutumia unyonge wetu kama kisa, kama sababu, kama hoja, ya kuendelea kututawala zaidi. Sikupata kumsikia hata Mkoloni mmoja anatembeatembea anawaambia wananchi wa Tanzania, kazaneni mjitegemee kwa nguvu zenu wenyewe, sikumsikia hata Mkoloni mmoja anatangaza hivyo. Vijana tunaowasomesha wenyewe wanasema na wanasaidiwa kutangaziwa na Wakoloni, kwamba ‘Afadhali Wakati wa Mkoloni’!…”
Hata hivyo, dai la wanafunzi wale kutaka wenye mishahara mikubwa nao wahusishwe, Mwalimu Nyerere alikubaliana nalo. Aliwaambia wananchi jambo hilo hakulichukia hata kidogo! Papo hapo alianza na mshahara wake. Akasema upunguzwe kwa Sh 1,000.  Baadaye, mishahara yote mikubwa ilipunguzwa –mishahara iliyorithiwa kutoka kwa wakoloni.
Kilichofuata, wanafunzi wale walifukuzwa vyuoni na kurejeshwa makwao chini ya ulinzi maalum. Walitakiwa kila mwisho wa mwezi kupiga ripoti kwa viongozi wa Serikali huko makwao.
Mwalimu Nyerere alikuwa kiongozi mkali, lakini mwenye hekima na busara.  Pamoja na hayo, alikuwa na huruma. Baada ya miezi kadhaa kupita, aliwahurumia vijana waliofukuzwa. Aprili, 1967 walitakiwa waandike barua kuomba radhi ili warudi masomoni. Aliwaruhusu warudi vyuoni, akiamini walikuwa wameelewa kwamba kosa walilofanya lilikuwa ni kutanguliza ubinafsi; kujali zaidi maslahi yao badala ya kuangalia maslahi ya Taifa lao changa.
Mwalimu alitaka wajifunze kwamba Tanzania itajengwa na wenye moyo na wao walipaswa kuwa na moyo huo wa kujenga nchi yao.
Vijana wale na wengine waliofuata, walipohitimu masomo yao walijiunga na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mujibu wa sheria. Walihenya  kambini kwa miezi sita. Walivaa magwanda ya JKT wakiwa kazini kwa miezi 18 iliyofuata na kulipwa asilimia 40 ya mishahara yao waliyostahili.
Waliopitia JKT enzi za Mwalimu Nyerere, wapo waliolielewa somo lile na mengine mengi aliyofundisha Mwalimu kupitia uongozi wake uliotukuka. Moja lililoeleweka ni kwamba bila Serikali kuchukua hatua za makusudi kusaidia watoto wa maskini, wengi wao hata dawati la darasa wasingekalia – wangeishia kuchunga ng’ombe na mbuzi na kuwa wakulima maisha yao yote. Wasomi wangebaki kuwa watoto wa watu waliokuwa na uwezo kifedha kama ilivyokuwa wakati wa Mkoloni.
Wengi wao sasa ni wazee; wanawasimulia watoto na wajukuu zao kwamba mpango ule wa kujiunga JKT ulikuwa mzuri, ulisaidia sana katika kujenga uzalendo, uadilifu, usawa, umoja, udugu na mshikamano miongoni mwa Watanzania. Kulikuwa hakuna matabaka wala ubaguzi ama tofauti kati ya mtoto wa maskini na tajiri; msomi na asiyesoma, na kadhalika.
Kutokana na hayo, Watanzania waliishi kwa amani na utulivu.  Tanzania ikaitwa “Kisiwa cha Amani.”
Wapo wasomi na wananchi wa kawaida waliozingatia aliyokuwa akiyasimamia Mwalimu Nyerere. Hawa waliitumikia nchi yetu kwa moyo thabiti katika nafasi mbalimbali bila kujali maslahi binafsi. Lakini, wapo waliokuwa na tamaa na ubinafsi. Waliona Mwalimu na siasa zake, alikuwa akiwabana na kuwazuia kutumia usomi wao na nafasi walizokuwa nazo, kujipatia mali.
Tunakumbuka, Mwalimu alipoondoka madarakani zilianza kuchukuliwa hatua na kufanywa uamuzi ulioashiria kubomolewa kwa misingi ya utu, usawa, uzalendo na uadilifu aliyoijenga Mwalimu.
Mfano mmojawapo ni uamuzi uliofanywa na viongozi wa CCM ‘wasomi’, Februari 1991. Azimio la Arusha lilifutwa likapitishwa Azimio la Zanzibar badala yake. Azimio hilo la Zanzibar lililegeza miiko ya uongozi bila kuangalia kwa makini madhara ya baadaye kwa Taifa.
Mwalimu Nyerere alilalamika kwamba Azimio la Arusha halikustahili kufutwa kwa sababu lilikuwa na misingi bora – misingi ya utu, lilikuwa na miiko ya uongozi.
Viongozi wa ngazi mbalimbali walichangamkia ruksa iliyotolewa na Azimio la Zanzibar, wakatumia nafasi zao kujitafutia na kujilimbikizia mali kwa njia halali na haramu. Wagombea wa nafasi mbalimbali wakajiingiza kwenye vitendo vya kununua uongozi. Rushwa ikapewa jina zuri la “takrima”! Wasiokuwa na fedha hawakuwa tena na uwezo wala nafasi ya kugombea ama kushinda; tofauti na kipindi cha Mwalimu ambako ilikuwa mwiko kuutafuta uongozi kwa kutumia fedha.
Upo uamuzi na mipango iliyopangwa na viongozi na wasomi wa nchi hii kwa misingi ya ubinafsi tu bila wahusika kutanguliza mbele maslahi ya Taifa. Mambo ya msingi aliyoyasimamia Mwalimu Nyerere wakati wa uongozi wake yalipuuzwa na kutelekezwa kwa kisingizio cha kwenda na wakati.
Wakati wa uhai wake, Mwalimu alijaribu sana kuwatahadharisha viongozi na wananchi kwamba huko nchi inakopelekwa siko. Hakusikilizwa!
Akaishia kuasa: “Fikra nzito hazifi kwa urahisi, zinabakia zikikera, na kila jamii ya binadamu katika historia inajipalia makaa kwa kuzipuuza!”
 Makosa yaliyotendeka katika awamu tatu zilizofuatia ile ya kwanza, matokeo yake yakawa ni kuporomoka kwa maadili nchini. Tanzania iliyokuwa na sifa nzuri nje ya mipaka yake, ikaanza kupoteza sifa. Nchi ikanuka rushwa, ikasifika kwa ufisadi na dawa za kulevya. Wananchi wa kawaida wakaendelea kubaki maskini wa kutupa wakati viongozi wao na watu wengine waliotumia nafasi zao kujitajirisha, wakiishi kama wako peponi.
Chama tawala- Chama Cha Mapinduzi- nacho kikaanza kuporomoka umaarufu wake na kutishiwa kuondolewa madarakani. Viongozi wa Chama wakagundua kumbe Mwalimu alikuwa sahihi kwamba ubinafsi ni hatari, ni janga kwa ustawi wa chama chao, Serikali, na maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla.
Wakati wa Uchaguzi Mkuu mwaka 2015, Chama Cha Mapinduzi kiliwatumia wasomi wake kutayarisha Ilani iliyokuwa na maudhui ya kujisahihisha na kurejea mambo ya msingi aliyoyasimamia Mwenyekiti wa kwanza wa Chama hicho, Mwalimu Nyerere. Akapatikana mgombea msomi, Dk. John Pombe Magufuli (ambaye naye aliwahi kupitia JKT!) Akazunguka nchi nzima kuinadi ilani ya chama chake kwa nguvu.
Viongozi  ‘wasomi’ wa vyama vya upinzani nao wakaona umuhimu wa kujinadi kwa kutumia jina la Baba wa Taifa lao Mwalimu Julius K. Nyerere, kwa kazi nzuri aliyoifanya kwa Taifa.
Mwisho wa yote, CCM ikapata ushindi uliopatikana kwa kazi ya ziada iliyofanywa na mgombea wao machachari na wapambe wake.
Mheshimiwa Dk. John Magufuli akawa Rais wa Tano wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi. Kwa kofia zake hizo mbili akateua na anaendelea kuteua wasomi waliobobea kushika nafasi mbalimbali za uongozi.
Tanzania aliyoipokea Rais Magufuli, haina tofauti sana na ile ya mwaka 1966 walipoandamana wale vijana wasomi. Pamoja na rasilimali lukuki zilizopo na kuwapo kwa mamilioni ya wasomi, umaskini bado uko palepale.
Tumeshuhudia jinsi Rais Magufuli alivyoianza vizuri na kwa staili yake, kazi ngumu ya kuliongoza Taifa. Tumeona jinsi wananchi maskini walivyoitikia kwa moyo mwito wake wa ‘Hapa Kazi Tu’na wanavyoendelea kumsikiliza na kujishughulisha kwa matumaini ya maisha bora.
Ombi langu kwa wasomi wa nchi yetu wanaoteuliwa  kumsaidia Rais, na wengine walio kwenye sekta za umma na sekta binafsi,  wabunge na wananchi kwa ujumla, warejee somo Mwalimu Nyerere alilowafundisha vijana wale waliokataa kujiunga JKT kwamba ubinafsi haujengi nchi. Nchi inajengwa kwa moyo wa kujitolea na kwa kufanya kazi kwa bidii.
Pia, katika kuijenga Tanzania mpya, lazima uwepo mshikamano, bila kujali vyama ama tofauti nyingine. Kama alivyotaka Rais Magufuli, uchaguzi ukiisha; Watanzania waungane, washikamane kujenga nchi yao kwa manufaa yao wenyewe na vizazi vijavyo.
Wakati kama huu wa kumbukizi ya kuzaliwa Baba wa Taifa letu, nawaomba wasomi nchini wasiiishie kufanya makongamano ya kumuenzi Mwalimu Nyerere kwenye kumbi zenye viyoyozi. Watoke, waende kwa wananchi kama alivyokuwa akifanya yeye. Wakawafundishe wananchi jinsi Mwalimu na viongozi wengine wa wakati wake walivyojitolea kwa moyo kuijenga nchi yao. Wananchi waelewe madhara ya ubinafsi, na bila kujali itikadi zao, wajue wana wajibu mkubwa wa kujenga nchi yao kwa moyo, ili Tanzania isonge mbele haraka kimaendeleo.
Nampongeza Profesa Penina Mhando, Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambaye hivi karibuni nilimsikia akieleza kwamba Kigoda hicho kina mpango wa kwenda shuleni kuwaelimisha wanafunzi  juu ya maisha ya Baba wa Taifa lao na kazi kubwa na nzuri aliyofanya kwa manufaa ya Taifa.
Ninaamini wanafunzi watakaojifunza juu ya maisha na kazi za Mwalimu Nyerere watakuja kuwasimulia watoto na wajukuu zao juu ya uongozi wake uliotukuka.
Pia, hawatasahau kwamba Mwalimu Nyerere hakusita kuwaadhibu wanafunzi walioonyesha ubinafsi na kukataa mwito, uliotolewa na Serikali iliyowasomesha bure, wa kulitumikia Taifa lao kwa moyo.
Ni muhimu kwa Watanzania wa kizazi cha leo na vizazi vijavyo kuelewa kazi na mafunzo ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, na kuzingatia  kwamba “TANZANIA ITAJENGWA NA WENYE MOYO”; na si vinginevyo.

Anna Julia Chiduo-Mwansasu
Katibu Muhtasi Mstaafu wa Serikali Awamu ya Kwanza
0655 774 967