Haifai, kwenda kusimama juu ya milima,
kupokea mapesa kwa mabepari,
kwa kutaka kuangamiza nchi, haifai.
Tizameni nyiye mambo mnayotaka kuyafanya,
ni mabaya sana, roho za watu wengi zitakuja potea,
na wakati huo Mungu atakuja wakasirikia. Haifai.
Tanzania itakuja chanika ooh!
Na mambo yote yatakuja haribika ooh!
Inakuja kuwa hasara ya milele
Tanzania itakuja waka moto ooh!
(Utunzi wa King Michael Enock ‘Teacher’ wa Dar Jazz Band. Umerekodiwa Septemba 9, 1970 – Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD).
Nimenukuu mashairi ya wimbo huo ‘Ubepari haufai’ ulioimbwa miaka ya 1970 na bendi ya dansi iliyokuwa maarufu nchini ikiitwa Dar es Salaam Jazz. Kwa lugha ya mitaani mashabiki waliwaita wasanii hao ‘Majini wa Bahari’ katika mitindo yao ya Dar Sengo, Kamata Mundo na mingineyo.
Nia yangu si kuelezea umaarufu wa bendi hiyo. Hapana. Madhumuni yangu ni kurandana na maneno yaliyotumika katika wimbo huo kuhusu hali ya siasa na uongozi enzi zile za Awamu ya Kwanza ya Serikali yetu ilivyokuwa, nikilinganisha na mwenendo wa leo katika siasa na uongozi unavyoipeleka jamii ya Watanzania.
Hata kama wasanii wa muziki wa leo katika bendi za dansi na taarab na wale waimbaji wa nyimbo za Bongo Fleva na Mipasho, bado hawajashawishika wala kuzinduka kwenda na kauli na vitimbi (visa) vya wanasiasa, wafanyabiashara na wanaharakati, hainifungi kusema yafuatayo;
Kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, 2015 kila pembe ya nchi yetu, Watanzania – wake kwa waume – baadhi yao walilalama, walilia na walifadhaika kutokana na mfumo na mwenendo wa siasa, uongozi na utawala wa Serikali uliokuwako ulionekana kama hauwatendei mema wananchi wa kawaida.
Tuhuma za ukweli na zisizo na ukweli kutoka kwa wananchi zilielekezwa serikalini na kuhisiwa imekwenda likizo kwa maana Serikali iliachia mambo ya rushwa kutawala, ufisadi kupanuka na dhuluma kutamalaki dhidi ya wananchi walalahoi. Hata baadhi ya viongozi na wananchi kukejeli Serikali na kuwapa chambi wapinzani wa siasa na Serikali kucheza ‘kasimbago’.
Vyama vya siasa vya upinzani hadharani vilitangaza kuing’oa Serikali na chama tawala – CCM. Kauli zilizotolewa zilibeza na kukejeli vyombo hivyo vimeshindwa kuendesha nchi na kuweka kaulimbiu ‘Mabadiliko ni Lazima’ – bila kueleza mabadiliko ya aina gani.
Nchi ilitikisika. Miamba iliwaka moto. Bahari, maziwa na mito ilichemka na wananchi walikimbia huku na kule wakitafuta mabadiliko ili kuondoa mifadhaiko ya hali ya maisha na siasa. Uchumi nao ulionekana kwenda fyongo. Nani wa kuleta mabadiliko ya kweli ndiyo iliyokuwa hoja ya Taifa letu.
Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mtu wa kuleta mabadiliko ya kweli alipatikana. Siyo wa mabadiliko. Hapo mambo yalianza kugeuka. Wale waliotaka mabadiliko wakawa mbele kulalamika. Wameonewa na wameibwa kura zao. Hawakubali na watahakikisha serikali zilizonyakuwa kura zao hazitafika mwaka 2020.
Si hivyo tu, wanaendelea kusema kuwa kama si busara zao za kupenda amani, leo nchi isingetawalika. Wanasema kuwa wanasikitishwa kuona sera zao zinatekelezwa na serikali zilizopo madarakani na wanashindilia kwa kusema uongozi uliopo ni wa kidikteta.
Na hivi sasa wanafanya mipango zaidi kuwapata washirika na nguvu kutoka Mahakama ya Kimataifa na mashirika ya fedha ya serikali za ughaibuni kuisulubu Tanzania. Kauli hizo zinaweka mashaka na maswali ndani ya mioyo ya wananchi wazalendo. Nchi isingetawalika wangefanya nini? Na kwa faida ya nani?
Huko nyuma, watu haohao walisikika na kukaririwa wakisema tunahitaji kiongozi ambaye ataweza kupambana na kuondoa rushwa, wizi, ufisadi na dhuluma ambazo ni kero na bughudha kwa wananchi. Mtu mwenye uwezo huo alihitajika na alitafutwa kutoka vyama vya siasa. Chama kilichofaulu kutoa mtu kama huyo ni Chama Cha Mapinduzi.
Dakta John Pombe Magufuli amepatikana. Uongozi wake unalenga kuondoa hizo kero na bughudha. Wananchi wa kawaida bila ya mashaka wanafurahia utendaji wake na kutoa heko jinsi mambo yanavyokwenda bambam. Tayari lawama zinajengwa na kuporomoshwa na walewale waliotaka mabadiliko. Wanasema kiongozi huyu (Magufuli) ni dikteta na falsafa yake ya kutumbua majipu.
Kamusi ya Kiswahili Sanifu iliyotolewa na Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI) Toleo la tatu la mwaka 2013 inasema: Dikteta – mtu anayetawala nchi kwa amri yake peke yake bila ya kushauriwa na pili, mtu mwenye tabia ya kutaka lifanywe lile analosema bila ya kupingwa. Kwa maana hizo udikteta wake uko wapi? Kuwatumbua wala rushwa, wezi wa umma, walevi kazini, mafisadi na wadhulumati hadharani ndiyo udikteta?
Watanzania, jambo la msingi ni kuangalia kwa makini mtu mwenye tabia ya kuzua na kutia fitina baina ya watu au pande mbili au zaidi, na akawa anajifanya kwamba unaunga mkono kila upande, mtu huyo ni mdhabidhabina. Na hao ndiyo waliyopo. Hadhari ichukuliwe.
Mdhabidhabina ni mtu hatari sana. Wasanii wa Dar es Salaam Jazz Band waliwaona watu hao ambao wanapokea mapesa kutoka kwa mabepari kwa kutaka kuangamiza nchi, huku wakijifanya wanawatetea wananchi. Hakika mambo hayo ni mabaya sana. Nchi itawaka moto na itaangamia. Mwenyezi Mungu atatukasirikia.
Watanzania wenzangu, tufungue macho na milango ya fahamu kwani dalili za kutaka kuangamiza nchi zinaonekana. Someni kauli za baadhi ya viongozi. Vijembe, mipasho na dharau zinatolewa bungeni na minong’ono kwenye mitandao mbalimbali. Ninachosema, kila mchelea mwana kulia hulia mwenyewe.