Taifa jirani la Burundi lipo katika msukosuko mkubwa na wachambuzi wa masuala ya migogoro ya kisiasa wanasema kuna kila dalili kuwa taifa hili sasa litatumbukia katika mauaji ya kimbari.
Burundi imeingia katika mgogoro baada ya Rais aliyeko madarakani Pierre Nkurunziza kugombea muhula wa tatu. Nkurunziza alidai kuwa mwaka 2005 aliingia madarakani kwa kuchaguliwa na Bunge badala ya wananchi, wakati Katiba ya Burundi inataka Rais achaguliwe na wananchi kwa mihula miwili.
Hoja hii ya Nkurunziza inapingwa na wataalam wa masuala ya kisheria, kwa maelezo kuwa wabunge ni wawakilishi wa wananchi hivyo walipomchagua mwaka 2005, walifanya kazi hiyo kwa niaba ya wananchi. Mwaka 2010 alichaguliwa na wananchi na hivyo alipaswa kuhitimisha kipindi cha uongozi wake mwaka 2015.
Kinachotisha zaidi, tangu Nkurunziza alipotangaza nia ya kugombea urais kwa muhula wa tatu, Aprili mwaka huu wameuawa watu 400 katika vurugu za kisiasa hadi sasa. Watu 3,500 wamekamatwa na 220,000 amekimbia makazi yao. Tukio baya zaidi ni pale askari walipoua wananchi 87 wanaodai kuwa walivamia kambi ya jeshi Ijumaa iliyopita.
Mauaji ya aina hii yanaleta wasiwasi mkubwa. Mwaka 1994, watu wanaokisiwa kuwa 300,000 waliuawa nchini Burundi. Nchi jirani ya Rwanda, watu 800,000 waliuawa na zaidi ya 2,000,000 wakakimbia makazi.
Kwa sasa dunia iko kimya. Umoja wa Afrika umetumia mkataba wa kuanzishwa kwake unaouruhusu kupeleka askari wa kulinda amani hata kama nchi mwanachama haijaridhia. Burundi imejibu kuwa kupeleka askari hao 5,000 itakuwa ni sawa na kuingilia mambo ya ndani ya nchi hiyo.
Kinachosikitisha zaidi, hata hiyo AU inasubiri msaada wa kifedha kutoka UN ingawa haitamki bayana. Burundi yenyewe imejikita katika kuishutumu Rwanda kuwa inaandaa waasi kwa kuwapa mafunzo. Mbaya zaidi, nchi jirani ambazo ni wanachama wa Afrika Mashariki; Tanzania, Kenya, Uganda na Rwanda zimeshindwa kukemea kinachoendelea Burundi, na zote ziko kimya kana kwamba wanaouawa ni kuku.
Tangu wiki iliyopita idadi ya wananchi wa Burundi waonavuka mpaka kuja Tanzania imeongezeka. Pale wilayani Ngara kuna sura nyingi ngeni zilizokimbia mapigano. Aprili 6, 1994 walipouawa marais wawili; Juvenal Habyarimana (Rwanda) na Cyprien Ntaryamira (Burundi) wakitika Dar es Salaam, yaliibuka mauaji na usalama wa Tanzania ukatetereka.
Ikiwa Warundi wataingia kwenye mauaji ya kimbari kwa mwelekeo uliopo ambako Watutsi na Wahutu wanaweza kuonana ni maadui, basi tujue usalama wa Tanzania utakuwa hatarini kwani silaha zitazagaa mikononi mwa raia, utekaji wa magari utarejea kama tulivyoshuhudia miaka michache iliyopita.
Sisi tunadhani wakati umefika. Rais John Magufuli si lazima uanze wewe. Unaweza kumtuma Waziri wa Mambo ya Nje Dk. Augustino Mahiga, ambaye ni mtaalam wa masuala ya migogoro na usuluhishi angalau akatoa kauli yenye kufubaza mgogoro huo, kisha kuanzia hapo amani irejeshwe Burundi. Sisi tunadhani hali ilipofikia Burundi, nchi jirani hazipaswi kuendelea kuwa kimya. Tuwasaidie Warundi, ni binadaku wenzetu, kwani ipo simu tunaweza kuhitaji msaada wao pia. Rais Magufuli tafadhali chukua hatua.