Tanzania na Ireland zimeazimia kuimarisha ushirikiano katika nyanja mbalimbali za maendeleo na uchumi ili kukuza uhusiano wa kidiplomasia, biashara, na uwekezaji kati ya Nchi hizo mbili.

Makubaliano hayo yamefikiwa wakati wa mazungumzo rasmi kati ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) na Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara wa Ireland anayeshughulikia masuala ya ushirikiano wa kimataifa, maendeleo, na Diaspora, Mhe. Neale Richmond.

Mazungumzo hayo yamefanyika katika ofisi ndogo ya Wizara jijini Dar es Salaam, ambapo viongozi hao walijadili fursa na mikakati ya kuimarisha mahusiano ya pande mbili kwa manufaa ya kiuchumi na kijamii.

Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Kombo ameishukuru Serikali ya Ireland kwa ushirikiano wa muda mrefu na mchango wake katika sekta za elimu, biashara, uwekezaji, utalii, afya, jinsia, uwezeshaji wa wanawake, pamoja na mifugo.

Aidha, alimpongeza Mhe. Richmond kwa ziara yake rasmi nchini Tanzania tangu alipoteuliwa, akisisitiza kuwa ziara hiyo ni ishara ya juhudi za dhati za kuimarisha uhusiano kati ya mataifa haya mawili.

Mhe. Kombo amesisitiza umuhimu wa kuongeza kiwango cha biashara kati ya Tanzania na Ireland, akihimiza wawekezaji kutoka Ireland kuchangamkia fursa zilizopo nchini, hasa katika sekta za kilimo, utalii, nishati mbadala, teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA), viwanda, na miundombinu.

Pia, amebainisha kuwa kiwango cha biashara kati ya mataifa hayo bado ni kidogo, hivyo kuna haja ya kuweka mikakati madhubuti ya kuongeza biashara yenye uwiano sawa.

Katika sekta ya utalii, Waziri Kombo amependekeza kuimarishwa kwa juhudi za kutangaza vivutio vya Tanzania kwa soko la Ireland na kuboresha miundombinu ya usafiri ili kuvutia wageni zaidi.

Aidha, amependekeza kuanzishwa kwa mfumo wa mashauriano ya kisiasa kati ya Tanzania na Ireland ili kuimarisha zaidi uhusiano wa kidiplomasia na kuweka msingi wa ushirikiano wa karibu katika masuala ya kimataifa.

Kwa upande wake, Mhe. Richmond ameahidi kuimarisha mshikamano wa kiuchumi na kijamii kati ya mataifa haya mawili kwa manufaa ya pande zote. Akitilia mkazo mshikamano wa kiuchumi, utamaduni, na elimu na kusisisitiza umuhimu wa sekta ya elimu kama nyenzo ya maendeleo endelevu.

Aidha, amebainisha kuwa amani na usalama ni misingi muhimu kwa ustawi wa mataifa, akihimiza juhudi za pamoja katika kuhakikisha utulivu wa kisiasa na kijamii kwa maendeleo yenye usawa