Na Frank Christopher
Katika makala iliyopita Toleo Na 335 mwandishi alieleza misingi ya ukuaji uchumi kwa taifa lolote duniani, ambayo Tanzania haiwezi kuikwepa. Leo tunakuletea sehemu ya pili ya makala hii ya kiuchumi inayodadishi mfumo, mkondo, faida na hasara zinazotokana na uamuzi unaofanywa na Serikali kiuchumi. Anasisitiza umuhimu wa kuipa kipaumbele sekta binafsi. Endelea…
Tumeshuhudia serikali ikiamua kufanya biashara na taasisi zake yenyewe jambo linalochagiza kupunguza kasi na na mchango wa sekta binafsi katika maendeleo ya nchi. Licha ya hilo tumeshuhudia kubadilika kwa sera na miundo ya utunzaji wa amana za serikali katika taasisi zilizo chini ya sekta binafsi na kuchagiza kubadilika kwa mtazamo na imani ya wafanyabiashara na wawekezaji kwa sekta binafsi na hasa mabenki na hatimaye kushusha kiwango cha ushindani kwa sekta binafsi kutokana na wengi kuwa na imani na serikali zaidi kibiashara kuliko sekta binafsi na hili linaweza kuonekana kwa benki zaidi kwani nyingi kwa sasa hupendelea kuikopesha zaidi serikali kuliko sekta binafsi.
Serikali kutokopa kutoka vyanzo vya nje kutokana na hali ya soko la fedha
Kwa mwaka wa fedha 2016/17 serikali ilipanga kukopa Sh. 2.1 trilioni kama mikopo ya kibiashara kwa ajili ya kugharamia bajeti yake. Lakini katika nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha 2016/17 serikali haikufanikiwa kukopa kiwango kilichotakiwa kutoka vyanzo vya nje kutokana na soko la fedha la kimataifa kuwa na riba kubwa ikilinganishwa na ile iliyotegemewa hapo awali. Kwa mfano, kiwango cha riba kwa ajili ya mikopo katika bara la Ulaya kilipanda kutoka asilimia 6 hadi asilimia 9 kiasi cha kufanya serikali kuahirisha kukopa kwa wakati husika hivyo kuhamishia utafutaji wa mikopo kwa nchi nyingine kama India, China na Korea Kusini.
Hali hii ilisababisha kukwama kwa miradi mingi ya maendeleo na hatimaye kuchangia kwa kiasi kikubwa kupunguza mzunguko wa fedha katika uchumi wa nchi. Fedha nyingi zilizopatikana hasa kutoka katika vyanzo vya nje kama mikopo ya kibiashara na ya masharti nafuu katika mwaka wa fedha uliopita ilipatikana hasa katika robo ya tatu na ya nne ya mwaka wa fedha kitendo kilichokwamisha utekelezaji bajeti kwa wakati na kwa uhakika zaidi.
Na, kwa upande wa mikopo kutoka vyanzo vya ndani, kwa mwaka wa fedha 2016/17 serikali ilifanikiwa kukopa asilimia 58 ya lengo katika kipindi cha miezi sita ya kwanza ya mwaka wa fedha hatua iliyochangia pia utekelezaji hafifu wa miradi kwa wakati husika na hatimaye kushuka kwa kasi ya kukua kwa uchumi (Wizara ya Fedha, 2016).
Tishio la mikopo chechefu (nonperforming loans)
Ni ukweli usiopingika kwamba sekta ya fedha ni injini kubwa ya maendeleo ya kiuchumi kwa nchi yoyote ile. Sekta imara ya fedha itajenga uchumi imara na kadhalika. Kuyumba kwa sekta ya fedha ni kuyumba pia kwa uchumi wa nchi kwa maana kwamba wawekezaji hawatapata mitaji ya uwekezaji ya muda mrefu au wataipata kwa gharama kubwa kuliko inavyostahili.
Kwa mwaka 2015, mikopo ya mabenki kwa sekta binafsi ilikua kwa asilimia 24.8, lakini kwa mwaka 2016 iliporomoka na kuwa asilimia 7.2 jambo lililopelekea kupungua kwa kasi ya uwekezaji na hatimaye ukuaji wa uchumi. Hali hii ilitokana na tishio la mikopo chechefu (mikopo iliyo kwenye hatari ya kutolipika) kwenye sekta ya mabenki ambapo mpaka Disemba 2016 ilifikia asilimia 9.53 ambayo ni juu ya kiwango kiichowekwa na Benki Kuu cha asilimia 5.
Na kuondokana na tatizo hili mabenki yalipunguza kasi ya utoaji mikopo kwa kuongeza riba (gharama za ukopaji) pamoja na kuongeza ukwasi (akiba) kitendo kilichochangia pia kupungua kwa mzunguko wa fedha katika uchumi wa nchi licha ya hatua hizo kuongeza uhimilivu katika sekta ya mabenki.
Na pia, kutokana na tishio hili la mikopo chechefu, benki za kibiashara nchini ziliamua kuongeza amana zao kwa kupunguza ununuzi ya dhamana za serikali pamoja na kuuza sehemu ya dhamana za serikali (treasury bills) walizokuwa wakizishikilia kuongeza ukwasi katika sekta ya benki.
Kwa mwaka ulioishia Disemba 2016 dhamana za serikali zilizoshikiliwa na benki zilipungua kwa asilimia 12.28 kitendo kilichopunguza takribani bilioni 599.7 katika mzunguko wa fedha (Taarifa ya Benki Kuu, 2016).
Hatua nyingine zilizochukuliwa na benki kujikinga na athari za mikopo chechefu ni pamoja na kuongeza riba kwa mikopo mipya inayotolewa, kuongezeka kwa riba za mikopo kati ya benki pamoja na kuongeza umakini zaidi hasa kwenye utoaji wa mikopo mipya. Na benki nyingine ziliamua kutafuta mikopo ya masharti nafuu kutoka kwa taasisi za kimataifa pamoja na kuuza hati fungani za benki zao ikiwa ni juhudi za benki kuongeza ukwasi.
Hatua hizi zilizochukuliwa zilipunguza kiwango cha ukopeshaji kwa sekta binafsi kwani kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 2017 mikopo ya benki kwa sekta binafsi iliongezeka kwa asilimia 1.3 tofauti na mwaka wa fedha unaoishia Juni 2016 ambapo ongezeko la mikopo kwa sekta binafsi lilikua asilimia 7.2 huku mwaka 2015 ukiwa na ukuaji wa asilimia 24.8 (Tume ya Mipango, 2017).
Haya yote yalichangia biashara na uwekezaji kudorora na hatimaye kupungua kwa mzunguko wa fedha katika uchumi. Hatua hizi pia ziliathiri kiwango cha ukopaji cha serikali kwa benki za kibiashara kwani katika nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha 2016/17 serikali ilikopa asilimia 58 tu ya lengo la ukopaji hali iliyochangiwa na kupanda kwa riba ya mikopo kutokana na benki kujilinda na tishio la mikopo chechefu na hatimaye kupungua kwa ukwasi tofauti na asilimia 96 ya kufikiwa lengo la ukopaji kwa mwaka wa fedha 2017/18 kwa miezi mitatu ya kwanza ya utekelezaji bajeti ikiakisi kupungua kwa riba katika benki kutokana na mwendelezo wa hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Benki Kuu (Wizara ya Fedha, 2017).
Utekelezaji wa bajeti ya 2017/18 kuanzia Juni 2017 hadi Disemba 2017
Utekelezaji wa bajeti ya nchi yoyote hutegemea makusanyo ya mapato ya ndani ya nchi pamoja na vyanzo vingine vya kibajeti. Licha ya ongezeko la mapato ya ndani kwa asilimia 1.0 katika miezi mitatu ya kwanza ya utekelezaji bajeti ikilinganishwa na mwaka wa fedha uliopita, makusanyo hayo yalikuwa asilimia 15 pungufu ya maoteo ya lengo la wakati husika sawa na upungufu wa bilioni 700 (Wizara ya Fedha, 2017).
Licha ya kuongezeka kwa wastani wa makusanyo kwa mwezi kutoka Sh. 850 kwa mwezi wakati wa Serikali ya Awamu ya Nne mpaka Sh.1.2 trilioni kwa mwezi kwa serikali ya Awamu ya Tano hivi sasa pamoja na kuziba mianya ya uvujaji wa mapato, ni wazi kwamba bado vipo vyanzo vingine vikubwa vya ndani ambavyo havijatozwa ipasavyo.
Mfano kodi ya majengo, kodi ya ardhi na uvuvi bahari kuu. Iwapo serikali itawekeza ipasavyo katika vyanzo hivi, ni dhahiri kwamba itakusanya mapato zaidi kuliko ilivyo sasa.
Misaada na mikopo ni chanzo kingine cha mapato kwa serikali kwa ajili ya kutekeleza bajeti yake. Chanzo hiki kwa siku za karibuni kimekuwa hakitabiriki kutokana na wahisani wengi kutoa fedha kidogo kuliko kiwango walichokiahidi, kuchelewa kutoa na pengine kutokutoa kabisa.
Hali hii imefanya serikali ipunguze utegemezi wa kibajeti kutoka asilimia 14.5 hadi 12.5 ili kukabiliana na hali. Hali hii itaifanya serikali kufikiria zaidi hatua za kuchukua kwa kutafuta suluhu za muda mrefu za utekelezaji wa bajeti yake ikiwa ni pamoja na kuongeza ukusanyaji wa mapato, kutafuta vyanzo vipya vya kimapato, mikopo nafuu pamoja na kuhuisha uhusiano na ushirika wa kimaendeleo na washirika wa maendeleo kisekta na hata kwa ujumla wake.
Je, unafahamu matarajio ya utekelezaji wa bajeti katika nusu ya pili ya mwaka wa fedha 2017/2018? Usikose toleo lijalo.
Mwandishi wa Makala hii anapatikana kwa namba ya simu 0763643199