Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko ameeleza kuwa, Tanzania na Indonesia zitashirikiana katika kuendeleza shughuli za uchimbaji wa madini hapa nchini ili kufungamanisha Sekta ya Madini na sekta nyingine za kiuchumi.

Hayo yamebainishwa na Dkt. Biteko Mei 4, 2023 jijini Dodoma alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Indonesia nchini Tanzania Mhe.Tri Yogo Jatmiko na ujumbe wake kuhusu kuwekeza katika shughuli za uchimbaji.

Amesema kuwa, mwitikio wa nchi mbalimbali kutaka kuwekeza katika Sekta ya Madini unatokana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kufungua fursa za uwekezaji hapa nchini.

Wizara ya Madini itatoa ushirikiano wa kutosha kwa nchi ya Indonesia ili kuboresha Sekta ya Madini, pia tupo tayari kushirikiana kwa kuwa na “Memorandum of Understanding” katika kila hatua na nchi ya Indonesia,”

Dkt. Biteko amesema kuwa, Sheria ya Madini inaruhusu wawekezaji ndani na nje ya nchi kuwekeza katika Sekta ya Madini na kuongeza kwamba nchi ya Tanzania imeweka mazingira rafiki na salama kwa wawekezaji ili taifa linufaike na uchumi wa madini.

Vile vile, amesema hivi sasa nchi ya Tanzania na Indonesia zina uhusiano mzuri katika nyanja zote ikiwemo Sekta ya Madini, afya na kilimo. Dkt. Biteko amemkaribisha balozi huyo katika Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka 2023.

Pia, wamezungumzia kuhusu ushirikiano wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na Taasisi inayojishughulisha na uchimbaji wa madini nchini Indonesia pamoja na fursa za mafunzo ya shughuli za uchimbaji nchini humo ikiwemo usalama migodini.

Naye, Balozi wa Indonesia hapa nchini Mhe. Tri Yogo Jatmiko amesema nchi yao inachimba madini mbalimbali ikiwemo shaba, dhahabu na kinywe na kueleza nchi hiyo ipo tayari kuwekeza Tanzania katika uchimbaji wa madini.

“Ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Indonesia ni mzuri katika nyanja zote. Uwekezaji utakaofanyika utakua manufaa makubwa kwa pande zote mara baada ya majadiliano kukamilika,” amesema Balozi Jatmiko.

Aidha, amemueleza Dkt. Biteko, Rais wa Indonesia atatembelea Tanzania mwezi Oktoba mwaka huu ili kushuhudia utiaji saini wa mikataba mbalimbali ya uchimbaji wa madini. Amesema hiyo ni njia nzuri ya kuendeleza ushirikiano kati ya nchi hizo.

Waliohudhuria kikao hicho ni Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa, Naibu Katibu Mkuu Msafiri Mbibo, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Mhandisi Yahya Samamba, Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Dkt. Venance Mwasse, Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Jilojia na Utafiti wa Madini Dkt. Mussa Budeba na watendaji wengine wa wizara na taasisi.