Kuna matokeo ya hivi karibuni ya utafiti uliyofanyika kupima kiwango cha furaha ya watu wa mataifa duniani na Tanzania inashika nafasi ya 153 kati ya nchi 156 zilizoshirikishwa kwenye utafiti huo. Finland inashika nafasi ya kwanza, wakati Burundi inashika nafasi ya mwisho.

Hawa watafiti wangenishirikisha mimi kwenye utafiti wao, naamini Tanzania tungekuwa kwenye 10 bora. Lakini ingekuwa ni 10 bora iliyopatikana kwa mujibu wa mtazamo wangu wa tathmini ya maisha yangu. Isingekuwa ile ya mkulima wa korosho wa Mtwara ambaye anaweza kuwa na mtazamo tofauti na wangu.

Swali la kuulizana kupima ukweli wa utafiti huu ni: nani aliyeulizwa maswali ya utafiti? Jibu kutoka Mtwara halitafanana na jibu la Butiama.

Mimi sikubaliani kabisa na maelezo kuwa kipo kigezo kinachoweza kutumika kupima hali ya furaha kwa binadamu wote, kama vile tunavyoweza kusema kwa uhakika kuwa nyuzijoto 25 ni nyuzijoto 25, uwe Marangu, New York, au Beijing.

Furaha ni suala linaloguswa sana na utamaduni wa binadamu, na tunafahamu kuwa utamaduni wa Wachaga, hauwezi kulinganishwa moja kwa moja na utamaduni wa wakazi wa New York, au wale wa Beijing.

Kwenye tamaduni zetu nyingi sisi, tunasherehekea kwa vinywaji na chakula ambacho kinajumuisha nyama zinazotokana na wanyama tuliowachinja. Wapo watu kutoka jamii ya nchi zilizoendelea ambao ukiwaalika kwenye sherehe zetu wakashuhudia kuchinja ng’ombe au kuku ambaye baadaye ataliwa kwenye sherehe hizo, basi utakuwa umewatumbukiza waalikwa kwenye huzuni kubwa.

Wao wamezoea kununua kitoweo dukani ambacho hawakushuhudia kimefikaje kwenye majiko yao, na wanaposhuhudia jambo hilo linazua huzuni na hata hasira ndani ya jamii. Jambo la furaha isiyo ya kifani kwa mtu mmoja linaweza kuzua huzuni ya kudumu kwa mtu mwingine.

Tunapataje matokeo ya utafiti ambayo yanadai kutoa majibu, wakati yanaibua maswali mengi tu? Kwanza, tuchunguze ni vigezo gani vinatumika kupima furaha kwenye utafiti huu. Mkazo mkuu wa utafiti wa mwaka huu ni uhamiaji; ni kipimo cha jinsi gani watu wanaohama kutoka nchi moja kwenda nyingine, au kutoka sehemu moja kwenda nyingine ndani ya nchi hiyo hiyo wanapima kiwango cha furaha yao.

Anaulizwa mkimbizi aliyekimbia mapigano nchini Syria na kuhamia nchi mojawapo ya Ulaya, na anaulizwa pia aliyehama Butiama na kwenda kuishi Dar es Salaam.

Utaona kuwa kundi la wanaojibu maswali linaacha sehemu kubwa ya watu wa nchi moja ambao hawashirikishwi kwenye utafiti. Sina imani kuwa idadi ndogo ya watu waliohama Butiama kwenda Dar es Salaam na wakaanza kupambana na hali ngumu ya maisha ya mjini watawakilisha kipimo cha furaha cha watu zaidi ya 20,000 tuliobaki Butiama.

Kuna imani ya watafiti ambayo haitamkwi bayana kuwa mtu anayehama haridhiki na maisha anayoyahama. Watafiti wanakusudia kuchunguza iwapo aliyehama anaridhika na maisha yake sehemu alikohamia.

Wahamiaji wanaohojiwa wanatakiwa kujipima kuridhika kwao na vigezo sita vya msingi: kipato, wastani wa umri wa kuishi, msaada wanaopata kutoka kwa kijamii, uhuru, kuaminiana, na moyo wa ukarimu.

Hata vigezo hivi navyo vinaweza kuzua tatizo la tafsiri kwa aliyevichagua na yule anayejibu maswali yanayopima vigezo hivyo.

Tuchukue kigezo cha kipato tu. Mtu wa mjini hawezi kuridhika na pesa kidogo ambayo mtu wa kijijini inamtosheleza mahitaji. Gharama ya maisha mijini huwa ni ya juu kuliko gharama ya maisha vijijini. Swali lile lile juu ya kutosha au la kwa kipato linaweza kuibua majibu mawili tofauti kutegemea na anayejibu anaishi wapi.

Tuangalie pia suala la uhuru kama kigezo kimojawapo cha kupima furaha ya mtu. Uhuru una tafsiri ile ile kwa kila mtu? Hapana. Kwa mtu mmoja uhuru ni uhuru wa kuamua kufunga ndoa ya jinsia moja. Kwa mtu mwingine ni kuwa huru kutoa mawazo yake kwa mtu yeyote, iwe yanakubalika au la.

Lakini si mtazamo ambao upo kila pembe ya dunia. Niliwahi kusikia mahojiano ya mfanyabiashara Mmarekani anayeishi China akiombwa kutoa maoni juu ya hali ya demokrasia nchini humo, akilinganisha na Marekani. Alijibu kuwa anachoona yeye ni kuwa Wachina wanachakarika kufanya biashara na kuboresha maisha yao bila kusumbuliwa sana na hoja ya kuwa wanaminywa demokrasia.

Kuna mabilionea (kwa kipimo cha dola ya Marekani) zaidi ya 2,200 duniani. Kati ya idadi hiyo China, nchi isiyo na demokrasia, inayo mabilionea 594. Marekani, nchi ambayo inayo demokrasia kubwa na inayoruhusu raia hata kuwa na uhuru kushona chupi kwa kutumia bendera ya nchi, inayo mabilionea 535.

Jaribu kumuuliza bilionea anayeongoza China, Wang Jianlin, kama ana uhuru wa kutosha nchini China na si ajabu akashangaa kuulizwa swali la kipuuzi. Uhuru wa kunyimwa kuwa na utajiri wa kufikia dola bilioni 30, badala ya utajiri wake halisi uliokadiriwa mwaka 2017 kufikia dola bilioni 25.22?

Baada ya kutangazwa matokeo ya utafiti nilisikiliza mahojiano ya Mtanzania anayeishi Norway kwa miaka mingi, nchi ambayo imeongoza kwa furaha ya raia wake kwa mujibu wa matokeo ya utafiti.

Kwa ujumla, alisifia maisha mazuri yenye masuala yaliyonyooka, hasa kwenye suala la huduma mbalimbali kwa wanajamii. Lakini alihoji iweje watu ambao wanaonekana mitaani wamenuna muda wote watokee kuongoza kwa furaha duniani.

Najaribu kujenga hoja kuwa watafiti wametumia vigezo ambavyo wanaamini vinabeba tafsiri moja kwa kila mtu; jambo ambalo si sahihi.

Watafiti hawa wangekuwa na nia ya kuupa jina sahihi utafiti wao wangesema wanapima furaha ya wahamiaji wa ulimwenguni, lakini siyo hali ya furaha kwa watu wote.