Na Lookman Miraji
Tanzania kwa kushirikiana na nchi jirani za Afrika mashariki za Kenya na Uganda zinategemea kuwa wenyeji wa michuano ya Afrika ya CHAN 2024 na AFCON mwaka 2027.
Kwa upande wa Tanzania kupitia kamati ya maandalizi ya CHAN imeeleza juu ya utayari wake katika kuwa mwenyeji wa mashindano hayo.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya CHAN kitaifa Leodgar Tenga amesema kuwa mpaka sasa maandalizi yamefikia katika hatua nzuri huku akiipongeza Serikali kwa jitihada zake katika ukarabati wa miundombinu ya michezo nchini.
“Serikali imefanya kazi kubwa ya kusimamia ukarabati wa viwanja vya michezo vya Benjamin Mkapa na New Amaan complex pamoja na maboresho ya miundombinu katika viwanja vya mazoezi vya gymkhana, Law school pamoja na uwanja wa Meja Isamuyo”.
Aidha pia Mwenyekiti Tenga amewaasa watanzania kutumia fursa zitakazokuja kupitia uenyeji mashindano hayo kwani yatasaidia kuinufaisha nchi katika nyanja mbalimbali.
Mashindano ya CHAN yalipangwa kuanza nchini kuanzia Februari mosi na kuhitimika Februari 28 mwaka huu lakini kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa usiku wa jana Januari 14 na shirikisho la soka Afrika imeeleza kusogezwa mbele kwa michuano hiyo mpaka mwezi Agosti mwaka huu huku sababu kubwa ikiwa ni kutoa muda zaidi kwa nchi wenyeji kujiandaa kikamilifu kuandaa mashindano hayo ya Afrika.