Tanzania kwa sasa inaweza kujiendesha bila kupata msaada wa nchi yoyote iwapo kasi ya ukusanyaji mapato, kuziba mianya ya uvujaji na matumizi sahihi ya kinachokusanywa itaendelea ilivyo sasa chini ya Rais John Pombe Magufuli.
Uchunguzi wa mfumo wa kodi, mbinu za ukwepaji kodi na sheria za fedha uliofanywa na Gazeti la JAMHURI kwa mwaka mzima chini ya ufadhili wa Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF), umebainisha kuwa Tanzania inaweza kukusanya kodi ikagharamia matumizi yote ya nchi na kubakiza ziada.
Wataalam wa masuala ya kodi, maafisa wa TRA, wafanyabiashara na wananchi wa kawaida, wameonyesha uhalisia kuwa tatizo la nchi hii ni mfumo mbovu wa ukusanyaji kodi, ulegelege wa sheria zinazosimamia kodi na Rais anayekuwa madarakani kutowajibika kujieleza matumizi ya fedha zilizokusanywa yamefanyikaje.
Takwimu za vyanzo mbalimbali, zinaonyesha kuwa Tanzania ina uwezo wa kukusanya hadi Sh trilioni 2 kwa mwezi na hivyo kupata wastani wa Sh trilioni 24 kwa mwaka kiwango ambacho ni zaidi ya bajeti iliyotengwa na Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2015/2016 cha Sh trilioni 22.
Mfumo wa Kodi
Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa Tanzania ina utitiri wa kodi kwa biashara yoyote inayoanzishwa hapa nchini. Kodi hizi mbali na kukatisha tamaa wafanyabiashara wachanga, zinawashawishi wafanyabiashara wakubwa kukwepa kwani zinakuwa nyingi kwa kiwango cha kuwakatisha tamaa.
Biashara inayohesabiwa kufanya vizuri, inalazimika kulipa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), Kodi ya Mapato (PAYE), Kodi ya Zuio, Kodi ya Ujuzi na Maendeleo, kodi ya mashirika, kodi ya majengo, kodi ya ardhi, gawio, ushuru wa forodha, leseni, huduma za miji, pango na kodi nyingine nyingi.
Mfumo unaotumika kutoza kodi ni kwa njia ya makadrio (presumptive) kwa biashara nyingi na hesabu zilizokaguliwa kwa biashara chache. Uchunguzi umebainisha kuwa nchi inapoteza mapato mengi kuanzia eneo hili. Mwanzo kabla ya kutanua wigo wa kodi, biashara zilizopaswa kulipa VAT ni zile zenye kuingiza pato la kuanzia Sh milioni 40 na kwenda juu kwa mwaka, lakini wigo huo umeshushwa hadi Sh milioni 14 mwaka jana.
Eneo hili ndipo mapato yanapotelea. Unakuta kiwanda kikubwa kinatumia leseni ya Jina la Biashara. Hii maana yake ni kwamba haandai hesabu. Huyu anakuja na kukutana Afisa wa TRA wanazungumza na rushwa inapita, kisha anakadriwa kiasi kidogo badala ya kushurutishwa kutumia mashine za EFD, akatunza kumbukumbua na kufikia kiwango halisi cha kulipa VAT.
“Tatizo hili tumeliona, na TRA tayari internally (kwa ndani) tumeanza mjadala wa kumfanya kila Mtanzania [mwenye umri wa maiaka 18 kwenda juu na kipato] alipe kodi. Hapa tunachopaswa kufanya ni kuhakikisha kila Mtanzania anajisali kulipa kodi, anawasilisha hesabu zake na kama hajafikisha kiwango cha kupata faida na kulipishwa kodi, basi atapita, aliyepata faida atalipa kodi. Ulaya na nchi zilizoendelea zote zinatumia utaratibu huu,” Rashid S. Herith, aliyekuwa Kaimu Meneja wa TRA Mtwara, aliliambia JAMHURI Januari 28, mwaka huu.
Harith anasema kodi ya mauzo inapotea kutokana na watu kutokuwa na utamaduni wa kudai risiti, ambapo watu wanafanya ununuzi wa bidhaa na huduma kisha wanaondoka bila kupewa risiti. Anasema wafanyabiashara wenye mzunguko (turn over) unaofikia Sh 4,000,000 wamekuwa wakikadriwa kodi, huku wenye mzunguko unaofikia 20,000,000 wakitakiwa kuandaa hesabu, lakini kwake yeye anaona hilil linatoa fursa ya kuwepa kodi.
“Kila anayesatahili kulipa kodi inabidi ajaze fomu maalum kuonyesha alipata nini na alilipa nini, hii itatuondolewa migogoro yote,” anasisitiza na kuongeza kuwa Serikali inapaswa kutoa elimu ya mlipakodi kwa kina kwani baadhi ya Watanzania hadi leo hawajui jinsi ya kuendesha biashara. Anaongeza kuwa baadhi ya wafanyabiashara wanadhani ukitangaza kupata faida unatozwa kodi kubwa jambo ambalo si kweli.
Anasema kutokana na utaratibu usio mzuri, baadhi ya magari hayalipi kodi ya hati ya njia. “Hivi leo mtu anataka motor vehicle wilaya kama Masasi, Mtwara au Newala, lazima aje Mtwara Mjini. Hii inawafanya watu waone ni gharama kwenda kulipa hii kodi, hivyo wanaendelea kuendesha vyombo vya moto bila kuvilipia kodi husika,” anasema.
Anapendekeza kila wilaya iwe na wakala au kitengo kinachoweza kutoza kodi au malipo ya kila aina kwa vyombo vya moto kutoa fursa ya wamiliki wa vyombo vya moto vyote kulipa kodi zinazohusika bila bughudha.
Elinami Terry, Mejena Msaidizi Madeni na Ulipaji Kodi kwa Hiyari, wa Mamlaka ya Mapato Tanzania Mkoa wa Kagera, ameliambia JAMHURI, kuwa bila hata kutanua wigo Serikali ikifanikiwa kuhakikisha kila anayenunua bidhaa yoyote anapewa risiti ya elektroniki, basi makusanyo yatakuwa makubwa kuliko wakati wowote.
Akizungumza na JAMHURI Juni 9, 2015 pale Mjini Bukoba, Terry amesema TRA mkoani Kagera walianzisha kampeni ya kutoa elimu kwa mlipa kodi na kusisitiza risiti kwa kila bidhaa anayonunua mtu. “Imefika mahala kwa Bukoba kijana wa pikipiki ukimpa mzigo anakwambia risiti iko wapi, maana anafahamu akikutana na maafisa wa TRA usumbufu atakaoupata ni mkubwa.
“Yuko tayari asibebe mzigo wako akose hela, kuliko kuubeba bila risiti akasumbuliwa na TRA. Hii imetuongezea mapato na kwa miezi ya Machi, Aprili na Mei tumevuka lengo,” anasema.
Novatus Tiigelerwa, Meneja Mkuu wa Chama Kikuu cha Ushirika wilayani Karagwe (KDCU) akizungumza na JAMHURI, Juni 12, mwaka huu, alisema nchi inakosa mapato mengi kwa kutokuwa na utaratibu rafiki wa mfumo wa kodi.
“Hapa kuna kodi zipatazo 26 kwenye kahawa. Kiasi hiki cha kodi kinapungumza mno mapato ya mkulima. Ikumbukwe wameruhusiwa wanunuzi binafsi wa kahawa, hawa hawana mfumo rasmi. Matokeo yake kahawa inauzwa yote Uganda kwa njia ya magendo bila kulipiwa hata chembe ya kodi, na serikali inakosa mapato yote. Kama kodi zingepunguzwa zikabaki mbili au tatu, nchi ingekusanya mapato makubwa na wakulima wakapata pato la uhakika,” anasema.
Mfumo wa kukadria kodi
Rukia Chivalavala, Mkazi wa Mtwara anasema mfumo wa TRA kukadria mapato bila kuangalia ukubwa wa biashara unaikosesha nchi mapato. “Mtu anakuja Afisa wa TRA anakwambia kwa biashara hii utalipa Sh milioni moja. Unalia unazungumza naye mnaishia kukadriwa Sh 300,000. Ukionekana mgumu bila ‘kuzungumza naye vizuri’ anakuandikia Sh 1,000,000 hiyo hiyo. Ukizungumza naye ‘vizuri’ kodi inashuka hadi 300,000,” anasema.
Anahoji wanakopata utajiri maafisa wa TRA: “Hivi tunajiuliza mishahara hata kama wangekuwa wanalipwa Sh milioni 5, hawa wangeweza kuneemeka hivi wakawa na nyumba za kupangisha, biashara kubwa kila mahala kweli? Tunajiuliza hivi hata hizo kodi tunazolipa zinafika?”
Anapendekeza uwepo utaratibu wa kukadria kiasi anachopaswa kulipa muhusika, na baada ya hapo TRA ifanye ufuatiliaji kuona iwapo biashara ya mtu inakua au la, kuepusha kumkadria kodi kubwa mtu, na biashara ikafa.
Tom Kabigumila, mfanyabiashara kati ya Lindi na Mtwara anasema TRA wanapaswa kuelimisha wananchi umuhimu wa kufanya baishara kwa kutumia kampuni na kuweka maeneo ya kulipia kodi jirani na watu. “Mtu hawezi kutoka Mtambaswala, akajileta Mtwara Mjini kulipa kodi au kusajili biashara. Usafiri na malazi vinakuwa gharama juu ya kodi anayokwenda kulipa,” anasema.
Wakala wa Usajili wa Biashara nchini (Brela) alipowasiliana na JAMHURI juu ya usajili wa kampuni, alisema kwa sasa wameanzisha mfumo wa kusajili biashara mtandaoni hivyo Mtanzania yeyote anayetaka kusajii anaweza kuisajili popote alipo.
Wengi wa waliohojiwa na JAMHURI, wamelalamikia mtindo wa kwenda kulipa kodi benki wakaambiwa mtandao uko chini na hivyo wakatumia siku nzima wamepanga mstari benki na pengine wasifanikiwe kulipa, hali waliyosema inakatisha tamaa.
Salum Said, mfanyabiashara katika soko la Mchikichini, Dar es Salaam, ameliambia JAMHURI kuwa Serikali inapoteza mapato mengi kutokana na kinachoitwa biashara ya wamachinga. “Kuna watu wanauza hadi Sh milioni 20 kwa siku au hata 40, hawa bado wanaitwa wamachinga. Kodi anayotozwa mfanyakazi, kwa wengi hapa [Mchikichini] ni pato na dakika 10 tu,” anasema.
Anasema biashara nyingi si za vijana wanaoshinda juani, bali matajiri wenye maduka makubwa huwapa vijana bidhaa kwa bei ya punguzo, ambao nao huuza mara mbili hadi tano ya bei halisi, kisha jioni hurejesha hesabu na bidhaa zilizosalia, hivyo hilo nalo ni dirisha jingine la kukwepea kodi.
“Wafanye kama Uganda. Kila mtu pale Nakivubo, ana chumba chake cha biashara. Ana namba yake ya mlipa kodi na mashine ya risiti. Wanaposema kutanua wigo wa kodi, hapa walipaswa kuiga wakubwa hawa. Walipaswa kila machinga kumpa namba ya mlipakodi na hivyo wangekusanya fedha nyingi ajabu,” anasema.
Urafiki wafanyabiashara na TRA
Suala jingine lililojitokeza kwa kiasi kikubwa ni tabia au utaratibu wa wafanyakazi wa TRA kuwa na urafiki wa karibu na baadhi ya wafanyabiashara wanaotuhumiwa kukwepa kodi au wanasiasa wanaofanya biashara na kutumia nafasi zao kuingia kila ofisi na kutoa amri.
“Tumeshuhudia harusi ya mtoto wa mmoja wa makamishna wa TRA, ilihudhuriwa na wafanyabiashra wengi wanaotiliwa shaka uadilifu wao. Tena bila aibu, Kamishna huyu akawatambulisha kama marafiki wa familia. Akatoa nyumba iliyojengwa na kukamilika. Mtoto wake anafanya kazi kwenye kampuni hizi zinazotiliwa shaka. Hii ni aibu kwa nchi na Serikali inaona tu, hakuna inachosema,” alisema mmoja wa watumishi wa TRA.
Uchunguzi unaonyesha watumishi wengi wa TRA kila mmoja ana kisawe chake. Wengi wamepata utajiri kupitia mlango wa kukadria kodi kampuni, watu binafsi na taasisi badala ya kuchunguza hesabu za kampuni husika au ‘kuwasaidia’ wafanyabiashara kufaulisha mizigo yao. K
wa wafanyakazi wengi huo ndio mlango wa rushwa. Wanajinasibu na wafanyabiashara wakubwa na wakati wa siku kuu wanakuwapo kulinda masilahi ya wafanyabiashara.
Baadhi ya watu waliozungumza na JAMHURI walivituhumu hata vyombo vya dola kuwa vinafahamu kila kitu na kwamba baadhi ya maofisa wanapata malipo kila mwezi kutoka kwa wafanyabiashara kuhakikisha wanakuwa ‘wasindikizaji’ wa mizigo ya dili. “Hili ni hatari. Ukiliandika linaweza kuchukua hata maisha yako, kwani hayo ndiyo maisha. Kampuni za mafuta ni hatari sana. Hawa wanaua ukichapisha habari zao jinsi wanavyokwepa kodi na mzigo ukasindikizwa,” alisema mtoa taarifa.
Kodi zinakopotelea
Takwimu rasmi za kiserikali, zinaonyesha katika mwaka wa fedha 2013/2014 ulioishia Juni 30, Serikali ilipoteza kiasi cha Sh bilioni 1,834.097 kupitia misamaha ya kodi. Misamaha hii imetolewa kwa kampuni, taasisi, mashirika na sekta ambazo wakati mwingine zinaacha mashaka. Kiasi hiki kimeongezeka kwa asilimia 21 ikilinganishwa na mwaka wa fedha uliotangulia.
Kiasi ni asilimia 3 ya pato la taifa, wakati sera inasema misamaha ya kodi isizidi asilimia 1 ya pato la taifa. Kwa ujumla katika sekta mbalimbali Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kupitia misamaha mbalimbali Serikali imepoteza kiasi cha Sh 676,882,527,383 ikiwa ni sawa na asilimia 36.9 ya kodi zote zilizosamehewa.
Kisekta, sekta ya madini inashika namba moja katika misamaha ya kodi. Kwa mwaka wa fedha uliokwisha ilisamehewa Sh 371,216,680,897 ikiwa ni sawa na asilimia 20.24 ya misamaha yote iliyotolewa. Mashirika ya Umma yameibuka namba tatu kwa kusamehewa 151,320,063,168 sawa na asilimia 8.25 ya misamaha yote.
Hata hivyo, yanayoitwa mashirika ya umma uchunguzi huru unaonyesha ni yake aliyokwishafilisika au Serikali ina hisa kidogo kati ya asilimia 20 hadi 50, ambayo faida yake kwa uchumi ni vigumu kuipima. Mashirika yanayotajwa kuwa ya umma na hisa zake kwenye mabano ni PUMA (50), SNOTASHIP (50), TAZARA (50), TIPER (50), Abood Seed Oil (20), In-flight Catering Services Company/ LGS Sky Chef (21) na New Africa Hotel (23).
Mashirika mengine ni ALAF (24), Kilombero Sugar Company (25), Mbeya Cement Company (25), Moshi Leather Company (25), Mwananchi Engineering and Construction Company (25), Tanganyika Planting Company (25), Williamson Diamond Company (25), East African Cables Tanzania Ltd (29), Kiwira Coal Mines (30), National Bank of Commerce (30), National Microfinance Bank (30), TANELEC (30), Mbozi Coffee Curing (32), Tanzania Development Finance Ltd (32) na TAZAMA Pipeline Ltd (33).
Pia yapo Datel Tanzania Ltd (35), Celtel Tanzania Ltd (sasa Airtel (40), Keko Pharmaceutical (40), Tanzania Pharmaceutical (40), Mbinga Coffee Curing (43), Friendship Textile Ltd (49), Kariakoo Market Cooperation (49), Tanscan Timber Company Ltd (49) na Usafiri Dar es Salaam (UDA (49).
Uchunguzi unaonyesha kuwa misamaha kwenye maduka ya jeshi, imeligharimu taifa Sh 12,245,651,978 sawa na asilimia 0.6 ya misamaha yote. Kinachosikitisha, uchunguzi unaonyesha kuwa misamaha hii haiwanufaishi askari bali wafanyabiashara wajanja. “Hivi kama lengo ilikuwa ni kuwawezesha askari kujenga nyumba za kuishi, unajiuliza inakuwake askari mmoja huyo huyo kila mwezi ananunua mabati 200 kwa mwaka mzima mfulululizo. Hiyo nyumba isiyoisha inalinganaje?” anahoji mmoja wa maaskari aliyeomba jina lake lihifadhiwe.
Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa licha ya askari kutumia fursa hiyo kujipatia chochote kwa kuwanunulia raia vifaa kwa bei nafuu na kuweka cha juu kidogo, wenye maduka ya jeshini wamekuwa wakipita katika maduka ya uraiani na kutofautisha bei ya bidhaa za jeshini na za maeneo kama Kariakoo kwa wastani wa Sh 1,000 hadi 5,000 hivyo wanaishia kupata faida ya kutupa.
Mashirika ya dini, uchimbaji wa mafuta, taasisi binafsi, miradi ya wafadhili na sehemu nyingine nyingi ilizozibainisha JAMHURI katika uchunguzi huu zimekuwa mianya ya kuvuja mapato ya taifa kwa ujumla.
Kutodai Risiti za elektroniki
Prof. Mussa Juma Assad, ambaye ni Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG), anasema mwanya mkubwa wa ukwepaji kodi unatokana na wafanyabiashara wengi kutotoa risiti za elektroniki. Anasema hadi sasa Serikali kwa kufanya biashara na watu wasiotoa risiti za elektroniki inahamasisha watu kukwepa kodi kwani wanachuma fedha nyingi kutoka serikalini na hawalipi kodi.
Anasema kabla ya kulibaini hilo, katika mwaka wa fedha 2012/13 Serikali ilipoteza kiasi cha Sh 47,935,509,285 kupitia utaratibu wa wafanyabiashara kutoipatia Serikali risiti za elektroniki, lakini baada kudhibiti mwanya huu, katika mwaka uliofuata 2013/14 kiasi kinachopotea kimeshuka na kufikia Sh 4,095,224,472, hivyo kupitia risiti za elektroniki Serikali imeokoa Sh 43,840,284,813.
“Nashauri Serikali iendelee kutoa elimu juu ya utekelezaji wa hiari kuzingatia Kanuni za Sheria ya Kodi ya Mapato (Electronic Fiscal Devices) za mwaka, 2012 kuhusu matumizi ya hiari ya mashine za EFD ambazo zitachangia kwa kiasi kikubwa kuongeza mapato ya Serikali kama kila manunuzi ya Serikali yataambatana na Risiti. Pia, ninapendekeza kwamba serikali isiendelee kufanya biashara na wauzaji ambao hawatumii mashine [za] EFD na kutoa risiti za kielektroniki,” anasema Prof. Assad.
Mbinu za kukwepa kodi
Uchunguzi umebaini kuwa wafanyabiashara walio wengi wanakwepa kodi katika ngazi tofauti. Wapo wanaokwepa wakati wa kuingiza bidhaa nchini, wengine wanakwepa wakati wa kuuza madukani na baadhi hawalipi kabisa, kwa kutumia mbinu zifuatazo.
Kwa wafanyabiashara wasio waaminifhu huiamba makontena kutoka bandarini. Njia hii inawarahisishia kupata faida ya karibu asilimia 95, kwani wanachofanya ni kushirikiana na baadhi ya maofisa wa Bandari na TRA wakakwapua makontena kutoka bandarini mchana au usiku kisha wakafuta kumbukumbu zote zinazohusiana na makontena hayo.
Vyanzo vya habari kutoka TRA na Bandari, vimeliambia JAMHURI kuwa kwa nia ya kumaliza mchezo wa maontena kuibwa, ni lazima zifungwe CCTV camera katika maeneo yote ya Bandari na wasiruhusu mzigo wowote kupata kibali cha kuondolewa bandarini ikiwa kukumbukumbu zake hazikufanywa kielektroniki. “Unaporuhusu billing ikafanywa manually, hicho ndicho kinakuwa chanzo cha makontena kupotea,” anasema mtoa taarifa wetu.
Njia nyingine wanayoitumia kuiibia Serikali, ni kutumia mitambo ya kisasa kurudufisha (photocopying) risiti halali kwa ustadi wa hali ya juu, ambapo risiti moja inaweza kuota hadi makontena 50 bandarini. “Njia hii wameitumia sana. Ikiishagusishwa kompyuta inaitambua kama risiti halali, kumbe ni hiyo hiyo inatoa makontena yasiyohusika,” anasema afisa mwingine.
Mtoa taarifa wetu anasema mbinu nyingine inayotumiwa, ni kutoa mzigo wakidai inasafirishwa kwenda nje ya nchi kisha ikahifadhiwa kwenye Bandari Kavu (ICDs), na unapopita mwezi mmoja mizigo hii hulipiwa ushuru nusu au robo kisha wanaiuza nchini bila kodi. “Mfano mzuri ni mafuta. Mtu analeta mafuta tani 60,000 anasema yanakwenda nje anayahifadhi kwa mwezi mmoja kisha anafuata sheria na ku-localize tani 20,000 anaonekana amelipa kodi, kumbe tani 40,000 zilizosalia zinauzwa bila kodi.”
Msemaji wa Mamlaka ya Mapato nchini Kenya (KRA) Kennedy Onyonyi, anasema nchini Kenya walimaliza tatizo la ukwapaji kodi kwa kuwataka waagizaji wote wa mafuta kulipa kodi kabla ya kushushwa melini. “Mwagizaji analipa kodi zote, kisha akiyasafirisha nje ya nchi anarejeshewa kodi aliyolipa na ni lazima uwepo ushahidi kuwa ameyapeleka nje ya nchi,” anasema.
Kwa utaratibu huo wa localization, ushuru wa bandari ambao ni asilimia 1.5 ya thamani ya mzigo inayojumuisha gharama, bima na usafirishaji (CIF) hupotea kwani ushuru huu hulipishwa kwa bidhaa zinazouzwa ndani tu, na ikiwa zimeonyeshwa kuwa ni za transit (kwenda nje ya nchi) zikiwa ‘localized’ zikauzwa ndani mapato hayo ya asilimia 1.5 ya thamani ya mzigo hupotea.
Watoa habari wetu, kwa nyakati tofauti na uchunguzi uliofanywa na JAMHURI kwa kuingia ndani ya Bandari, baadhi ya makontena huingizwa nchini nyaraka zikionyesha kuwa wameingiza neti za mbu, kumbe ndani yake kuna vipuri vya magari. Mbinu nyingine ni kushusha thamani halisi ya mzigo. Kwa mfano gari lenye thamani ya Sh milioni 150, baadhi ya wateja kwa njia ya rushwa huandikisha kuwa lina thamani ya Sh milioni 20, na kuishia kulipishwa kodi ya wastani wa Sh milioni 9, badala ya Sh milioni 80.
Suluhisho ni nini?
Katibu wa Kwanza wa Bodi ya Mamlaka Mapato Tanzania (TRA), Mushengezi Nyambele, ameliambia JAMHURI kuwa awali alikuwa na mawazo kuwa wafanyabiashara wadogo waachwe wawe huru kufanya biashara bila kulipa kodi, lakini baada ya uchunguzi amebaini kuwa hawa wanafanya biashara kubwa kuliko hoteli kubwa hivyo nao wanastahili kulipa kodi.
“Nilianzisha restorant na baa pale Mtoni Mtongani (Dar es Salaam) nikawekeza gharama kubwa kwa kujenga jengo zuri nikachukua vibali vyote na kulipa kila kodi. Nilianza kuchoma mshikaki standard, lakini ghafla kina mama wakavamia pale nje wakawa wanachoma mishikaki ya Sh 50, wateja wote wakawakimbilia. Ikawa sina tena wateja na wala hawa kina mama hawalipi kodi. Kuna mama Ntilie anapata fedha nyingi kuliko wenye hoteli. Dawa hapa ni kila anayeingiza kipato kulipa kodi kwa mujibu wa sheria bila kujali ukubwa wa biashara,” anasema Nyambele.
Zitto alia na idadi ya walipakodi
Mbunge wa Kigoma (Ujiji – ACT), Zitto Zumberi Kabwe ameliambia JAMHURI Julai, mwaka huu kuwa idadi ya walipakodi hapa nchini ni ndogo na Serikali inabadi kuwabana wafanyakazi huku wafanyabiashara wakubwa wakitamba.
Anasema kwa miaka mingi, walipakodi wakubwa wamebaki 15 tu, huku kampuni nyingine zenye uwezo mkubwa kifedha zikiwa hazilipi kodi. Anasema tatizo jingine ni TRA kutokuwa na utaratibu wa kutangaza walipakodi ni akina nani na wanalipa kiasi gani.
Anasema kwa mfano Waziri Mkuu aliyepita, Mizengo Pinda ndiye aliyetoa orodha ya walipakodi wakubwa 15 kwa kuwataja na kiasi wanacholipa kwenye mabano kuwa ni:- Tanzania Breweries Ltd. (Shilingi Bilioni 165.4); National Microfinance Bank (Shilingi Bilioni 108.6); Tanzania Cigarette Company (Shilingi Bilioni 92.1) na National Bank of Commerce (Shilingi Bilioni 89.9).
Wengine ni CRDB Bank Ltd. (Shilingi Bilioni 79.2); Tanzania Ports Authority (Shilingi Bilioni 76.8); Tanzania Portland Cement (Shilingi Bilioni 73.4); Airtel (T) Ltd. (Shilingi Bilioni 63.6); Tanga Cement Company Ltd. (Shilingi Bilioni 43.6); Standard Chartered Bank Ltd. (Shilingi Bilioni 40.0); Citibank (T) Ltd. (Shilingi Bilioni 35.7); Resolute (T) Ltd. (Shilingi Bilioni 32.1); Tanzania International Container Terminal Services (Shilingi Bilioni 25.9); Tanzania Distillers Ltd. (Shilingi Bilioni 13.4); na Group Five International (PTY) Ltd. (Shilingi Bilioni 9.5).
Anahoji ziko wapi kampuni kama Vodacom, Tigo, migodi kama Geita Gold Mine, Buzwagi na mingine anayoamini inatengeneza faida kubwa. Hata hivyo, Mkurugenzi wa Huduma kwa Walipakodi, Richard Kayombo, hivi karibuni amekaririwa akisema kampuni ya Vodacom nayo inaangukia kwenye kundi la walipakodi wakubwa.
Kwa mwaka 2014, anasema katika kipindi cha miezi sita hadi Septemba Vodacom ilikwishalipa Sh bilioni 27.6 na kukusanya VAT zaidi ya Sh bilioni 141.5, huku mwaka 2013 kampuni hiyo ikiwa imelipa kodi Sh bilioni 47.1 na kukusanya VAT Sh 262.8.
Kabla ya kuondolewa madarakani na Rais John Pombe Magufuli kutokana na sakata la makontena 349 yaliyotoroshwa bandarini na kuchangia Serikali kupoteza kodi ipatayo Sh bilioni 80, baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuanzisha moto Novemba, aliyekuwa Kamishna Mkuu wa TRA, Rished Bade, alikuwa ameliambia JAMHURI kuwa tayari mianya karibu yote inayotumiwa kuvujisha mapato ya serikali zikiwamo bidhaa zinazoshushwa kwenye majahazi na Bagamoyo wanaifahamu na wanaendelea kuiziba.
“TRA inafanya kazi usiku na mchana, na ndiyo maana tumebadili utaratibu wa kulipa kodi kwa sasa mtu analipa kodi akiwa na simu yake ya mkononi, tumeongeza usalama na tuaendelea kuboresha mifumo itakayotusaidia kutambua kila kinachoingia nchini, kila biashara inayofanywa na kiwango cha kodi kinacholipwa. Tupe muda, hatujalala,” anasema Bade.
Wakati juhudi hizo zikiendelea, baadhi ya maafisa wa TRA wameliambia JAMHURI kuwa suala la anwani za makazi linaweza kuwa msaada mkubwa katika kufuatilia nani anapaswa kulipa kodi kwani kwa hali ilivyo sasa ambapo biashara zinaendeshwa katika viwanja ambavyo havijapimwa, inakuwa vigumu kujua una walipakodi wangapi na uwafuatilie kivipi. “Mtu anasajili biashara anasema ipo Temeke, kumbe anaishi Ilala. Hii shida tukiiondoa kwa kusajili viwanja na kutoa anwani za makazi (postal codes) ukwepaji kodi utapungua au kuisha kabisa,” anasema Afisa wa TRA.
Wakati Serikali ya Awamu ya Nne imekusanya kiasi cha Sh bilioni 900 kwa mwezi na kutamba kila mahala, Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Magufuli katika mwezi wa Novemba, imekusanya kiasi cha Sh trilioni 1.3, hasa baada ya kuwabana wafanyabiashara wakubwa waliokuwa hawaguswi kama akina Said Salim Bakharesa, ambaye amelipa zaidi ya Sh bilioni 4 ndani ya wiki moja. Rais Magufuli aliyeapa kutumbua majipu, akimaanisha kuwa angewagusa waliokuwa hawakusigi miaka yote, amewapa faraja Watanzania kwa hatua ya kuwabana wafanyabiashara wakubwa.
Kwa ujumla, ikiwa Serikali inapaswa kutanua wigo wa kodi, kilichoelezwa kupita uchunguzi huu kuwa kila Mtanzania anayeingiza kipato asajiliwe kama mlipa kodi na ziwepo fomu maalum la kupeleka marejesho ya kodi kila mwaka kama zinavyofanya nchi zilizoendelea, kikitekelezwa kinaweza kuwa mwanzo wa Tanzania kukusanya mapato ya kutosha. Unahitajika udhibiti wa kina juu ya mizigo ya transit na kuondoa kodi za kero hali itakayowavuta wengi kulipa kodi kwa hiyari.
Uchunguzi huu umefanywa na gazeti la JAMHURI kwa ufadhili wa Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF). Mwandishi wa habari hii anapatikana kwa simu Na 0784 404 827.