Katika toleo lililopita la gazeti hili, nilizungumzia hali halisi ya ujirani wa Tanzania na nchi nne nyingine zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki Tanzania.
Nilisisitiza kwamba katika Jumuiya ya Afrika Mashariki Tanzania haina majirani wazuri. Nilitoa mfano wa Kenya ambayo imekuwa ikihujumu Tanzania na kuifanyia mambo ya uhasama yanayodhoofisha umoja na ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Nilitoa mfano wa karibuni zaidi ambao ni kauli ya Kenya kwamba ikinyang’anywa eneo lake la pwani na Somalia, itaipokonya Tanzania Kisiwa cha Pemba. Nilizungumzia pia sababu moja kubwa ya Tanzania kuharakishwa kwenye uanzishaji wa Shirikisho la Afrika Mashariki. Ni kunyemelewa ardhi ya Tanzania.
Kama tujuavyo, Kenya ina tatizo kubwa la ardhi tangu enzi za ukoloni wa Kiingereza, kwa kuanzia Wanandi waliopambana na Waingereza wakipigania ardhi yao wakati wa ujenzi wa reli kutoka Mombasa kwenda Uganda. Baadaye katika miaka ya mwisho ya 1940 Wakikuyu, Waembu na Wameru walipambana na Waingereza katika vita vya Maumau.
Japokuwa vita ya Maumau ilihusisha madai mbalimbali, sababu moja kubwa ya vita hiyo ilikuwa kudai ardhi ambayo walikuwa wamenyang’anywa na Wazungu. Watu wamesema kwamba ardhi ni ufunguo wa maisha. Lakini ardhi ni zaidi ya hapo. Ardhi ni msingi wa uhuru wa nchi yoyote.
Katika somo la Uraia, wananchi wanafundishwa kwamba demokrasia ina misingi mitatu. Misingi hiyo ni uhuru wa nchi, uhuru wa mtu binafsi, na usawa wa binadamu. Katika misingi yote hiyo mitatu hapana shaka msingi mkubwa zaidi ya demokrasia ni uhuru wa nchi. Na nchi ni ardhi. Bila kuwa na ardhi hakuna nchi, hakuna uhuru.
Ni katika mazingira hayo, wananchi wa Kenya walipambana na Waingereza wakipigania ardhi yao. Vile vile Washona na Wandebele wa Zimbabwe walipambana na Waingereza wakiongozwa na Mfalme Lobengula. Nao Wanama na Waherero wa Namibia walipambana na Wajerumani wakipigania ardhi yao. Wananchi wa Zimbabwe wanaendelea kumheshimu Rais wao, Robert Mugabe, kwa sababu ameendelea kuwa imara kulinda na kusimamia ardhi yao.
Kwa mda mrefu Tanzania haijawa na matatizo makubwa ya ardhi. Kwa Watanganyika, miaka ya 1920 Wamaasai walipambana na makabila mengine wakipigania ardhi ya malisho. Serikali ya Kiingereza Tanganyika ilimaliza tatizo hilo kwa kuwatengea Wamaasai ardhi iliyo kati ya Arusha, Singida na Handeni mwaka 1923. Eneo hilo likaitwa “Maasai Reserve” yaani Hifadhi ya Wamaasai.
Halafu katika nusu ya mwisho ya miaka ya 1940, Serikali ya Mwingereza Tanganyika iliwanyang’anya Wameru ardhi yao mwaka 1952. Wameru walimtuma Japhet Kirilo kwenda Umoja wa Mataifa, Marekani, kudai ardhi waliyokuwa wamenyang’anywa.
Japhet Kirilo akahutubia Umoja wa Mataifa Julai 21, 1952 akiwa Mtanganyika wa kwanza kuhutubia umoja huo. Lakini, hata hivyo, Wameru hawakurudishiwa ardhi yao.
Miaka hii Tanzania haipo makini na ardhi yake. Kuna ugomvi wa ardhi kati ya wakulima na wafugaji. Kisha Tanzania imenyang’anya ardhi watu wake wa maeneo mbalimbali na kuwapa wageni wanaoitwa “wawekezaji”.
Katikati ya shughuli hiyo ya uwekezaji wananchi wa Tanzania wamegeuzwa wageni katika nchi yao kwa kunyang’anywa ardhi yao.
Hili ni jambo la kukatisha tamaa wakati Zimbabwe inanyang’anya wageni na kuwapa watu wake, Tanzania inanyang’anya ardhi watu wake na kuwapa wageni! Hii ni kusema kwamba Tanzania inawaandalia watu wake vita na mapambano kati yao na wageni. Busara itumike kukomesha uuzaji na utoaji huu ovyo wa ardhi kwa wageni, ambao unawanyang’anya wazawa ardhi yao na uhuru wao.
Tukirudi kwa majirani zetu Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi — zote zina matatizo ya ardhi. Sehemu kubwa ya matatizo hayo yamesababishwa na uongozi ambao baada ya kupatikana uhuru katika nchi zao, walichukua nafasi ya walowezi Wazungu, wakajichukulia maelfu na maelfu ya ekari za ardhi huku wakiwaacha watu wao hawana ardhi.
Sasa viongozi hao wameamua kuyahamishia matatizo ya ardhi Tanzania. Na wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kujipatia ardhi ya Tanzania kutokana na uzembe wetu wa kushindwa kusimamia masuala yetu muhimu. Wakati Serikali imesimama imara kutohusisha suala la ardhi katika Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Ardhi ya Tanzania inaendelea kuchukuliwa kila siku na majirani zetu kwa kutumia hila mbalimbali. Kuna nchi zinahimiza watu wake kuoa wanawake wa Tanzania na kwa njia hiyo watu wa nchi hizo. Wameendelea kujipatia ardhi ya Tanzania.
Kuna nchi zilizo jirani na Tanzania ambazo watu wake wanatumia viongozi wa Tanzania kujipatia ardhi Tanzania. Kwa mfano, mtu mmoja aliyewahi kuwa mkuu wa mkoa na waziri alifuatwa na mtu wa Kenya akatakiwa achukue ardhi ya ekari 10,000 ili mtu huyo wa Kenya atoe fedha za kuendeleza ardhi hiyo, kiongozi huyo mstaafu na mzalendo alimkatalia Mkenya huyo ushirikiano huo.
Halafu kuna mkuu mmoja wa wilaya ambaye aliombwa na mama mmoja Mtanzania aliyekuwa nchini Italia, atengeneze eneo kubwa la ardhi ambalo Mtanzania huyo alidai angeliendeleza kwa kushirikiana na Waitalia.
Kumbe mkuu huyo wa wilaya alipofuatilia suala hilo aligundua kuwa hakukuwa na Waitaliano waliotaka kuwekeza katika ardhi ya Tanzania bali ni Wakenya waliomtumia Mtanzania kupata ardhi nchini.
Hii ni mifano michache tu ya viongozi wachache wazalendo waliolinda ardhi ya Tanzania. Lakini kwa vyovyote, wapo viongozi waliokosa uzalendo ambao tayari wametoa ardhi kwa Wakenya na kwa watu wengine wa nchi jirani.
Kwa ajili hiyo, wakati umefika kwa Tanzania kuunda tume kwa kila wilaya kuchunguza maeneo ambayo wageni wamepewa ardhi ili wanyang’anywe sasa. Kwa kuwa Watanzania tunaendelea kukabiliwa kwa kupuuza ushauri kwa kuundwa tume za kufuatilia suala la ardhi kila wilaya hautafuatwa. Kwa hiyo, ardhi ya Tanzania itaendelea kuchukuliwa na wageni kwa uzembe wetu.
Mbali na hila hizo zinazotumiwa na majirani zetu kuchukua ardhi ya Tanzania, hila kubwa zaidi inayotumika ni kuiharakisha Tanzania ikubali kuanzishwa shirikisho sasa. Katika kuiaminisha Tanzania kuwa inabaki nyuma tumeshuhudia Kenya, Uganda na Rwanda zikikutana na kufanya mambo peke yao na kumweka kando Rais Kikwete. Hiyo ni hila ya nchi hizo zenye lengo la kuifanya Tanzania ijione kwamba inachelewa na inaachwa nyuma peke yake, kisha ikubali kuanzishwa kwa shirikisho mara moja ili ardhi ya Tanzania iwe ya watu wote wa Afrika Mashariki.
Imedaiwa kuwa kwa kuwa na Shirikisho la Afrika Mashariki lenye watu million 150 uchumi wa ukanda huu wa Afrika Mashariki utakua na utaimarika sana, jambo ambalo halina ukweli wowote.
Tazama! China na India zina uchumi imara lakini hazina shirikisho kadhalika na Mauritias na Singapore. Nigeria yenye watu milioni 170 na mafuta, uchumi wake si imara ingawa ni shirikisho. Leo Afrika ina watu kama bilion moja. Kiuchumi kwa miaka ishirini sasa uchumi wa nchi za kusini ya Jangwa la Sahara (nchi 49) pamoja na Afrika Kusini ambayo ni tajiri zaidi nchi zote kwa pamoja, ni kama asilimia 2 tu ya uchumi wa dunia.
Uchumi wa Afrika Kusini ni kama asilimia 0.5 ya asilimia 2 ambao ni uchumi wa nchi hizo zote 49. Hii ni kusema kwamba ukitoa Afrika Kusini uchumi wa nchi 48 zinazobaki ni kama asilimia 1.5 ya uchumi wa dunia.
Kwa hivyo, tusidanganyane kwamba suluhisho la umaskini wetu ni kuunda shirikisho au soko la pamoja. Soko la pamoja halitaishia kwenye soko tu bali pia linaweza kutumiwa kuingiza watu Tanzania kuchukua ardhi yetu.
Wakati umefika kwa Tanzania kujiuliza siyo tu tutapata shida gani tukijiunga kwenye shirikisho bali pia tutapata hasara gani. Hasira moja kubwa itakuwa kuhalalisha ardhi yetu kuchukuliwa na wageni. Mpaka sasa unaweza ukasema kwamba ni Kenya inayonufaika zaidi na ushirikiano huu wa Afrika Mashariki.
Chukua, kwa mfano, upande wa vyombo vya habari, vyombo vya habari Tanzania vimekataa kuandika au kutangaza habari za Kenya huku vyombo vya Kenya vikiacha kabisa kuandika au kutangaza habari za Tanzania.
Na kwa upande wa uchumi, Tanzania imeendelea kuiuzia Kenya malighafi huku Kenya ikigeuza malighafi ya Tanzania kuwa bidhaa ambayo inaiuzia Tanzania kwa bei kubwa, katika mazingira hayo wakati umefika tena kwa Tanzania kufikiria upya dawa ya kumaliza matatizo yake ya kiuchumi kwa faida.
Kwanza, ni usimamizi mzuri wa rasilimali zake zikiwamo ardhi, madini na wanyamapori, Tanzania imeendelea kuwa maskini kwa sababu tumeshindwa kusimamia rasilimali zetu. Kwa mfano, ingawa ni Tanzania pekee inayotoa madini ya tanzanite duniani, nchi zilizoendelea kunufaika na madini hayo ni Kenya, Afrika Kusini na India.
Leo tunaaminishwa kuwa umaskini utatoweka eti Tanzania kwa sababu tumegundua gesi asilia ya kutosha, bila usimamizi nzuri unaoendana na uzalendo, Tanzania itaendelea kuwa maskini katikati ya gesi hiyo.
Halafu, ni vyema Tanzania ikafikiria kuanzisha viwanda vyake vya kutengeneza bidhaa mbalimbali badala ya kuendelea kuziuzia Kenya na nchi nyingine malighafi. Vile vile badala ya kuendelea kuaminishwa kwamba ushirikiano wa Afrika Mashariki wenye watu milioni 150 ndiyo mwarobaini wa uchumi wetu, tupanue soko letu pande zote za dunia hii yenye watu bilioni saba.
Na kama ni ushirikiano basi bora tuimarishe ushirikiano wetu na nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) ambazo zina watu milioni 280.
Na hapa si idadi kubwa zaidi tu ya watu. Nchi za SADC ni majirani zetu wazuri wasio na hila na wasio inyemelea ardhi yetu.
Tusiendelee na mradi mbovu na hatari wa Jumuiya ya Afrika Mashariki eti kwa sababu tumewekeza huko. Ni kweli kujitoa kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki kunaweza kutugharimu sana kwa kuwa tayari tumeweka lakini tutaacha salama zaidi. Ukitaka kusema kweli ni Kenya inayonufaika zaidi na Jumuiya ya Afrika Mashariki na imejiandaa kunufaika zaidi tukianzisha shirikisho kichwa kichwa.
Alikuwa Waziri wa Kenya wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kingi, aliyewaambia waandishi wa habari nchini Kenya Julai 1, 2010 kwamba Kenya ndiyo inayonufaika zaidi na Jumuiya ya Afrika Mashariki. Na akawataka Wakenya wawe watu wa mwisho kutoa malalamiko yao dhidi ya Soko la Pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashriki. Kwa jumla, Watanzania wanahitaji uvumilivu wa fikra kufikiria hali yao ya baadaye.
Si kweli kwamba bila Jumuiya au Shirikisho la Afrika Mashariki hawatapata maendeleo. Mbali na utulivu, Watanzania wanahitaji pia kujiamini. Tusifike mahali ambapo tunaiona Kenya kuwa mfano wa kuigwa katika kila kitu.
Hakuna asiyekubali kwamba Kenya iko mbele yetu katika maendeleo ya kielimu. Kurekebisha hali hiyo, wizara inayosimamia elimu Tanzania iboreshe elimu kwa kujali maslahi ya walimu na kuhakikisha kuwa shule zina vitabu bora. Na kwa upande wa ardhi inafurahisha kuona kwamba Katiba mpya itatamka kwamba ardhi ya Tanzania ni kwa ajili ya Watanzania.