SERIKALI ya Tanzania imeendelea kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia na Serikali ya Hispania katika sekta za utalii, afya, maji, miundombinu, usafi wa mazingira, kilimo na nishati ambazo zinachangia katika kuboresha maisha ya Watanzania.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi, Dk Pindi Chana usiku wa Oktoba 11, 2024 wakati wa hafla fupi ya Maadhimisho ya Siku ya Kitaifa ya Hispania ambayo pia inajulikana kama Dia De la Hispanidad yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.
“Tanzania na Hispania zimekuwa na uhusiano mzuri wa kidiplomasia tangu mwaka 1967 Hispania ilipofungua ubalozi wake nchini Tanzania na baadaye kufungua Ubalozi mdogo wa Heshima Zanzibar. Tanzania inathamini uungaji mkono wa Serikali ya Hispania katika ajenda ya maendeleo ya Tanzania,” amesema Dk Chana.
Dk Chana amesema kuwa Tanzania inatambua maendeleo na mafanikio ya Hispania kwenye utalii kutokana na utaalamu wake pamoja na kuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa kutembelewa na watalii duniani, hivyo ushirikiano baina ya Tanzania na Hispania ni muhimu katika kuhakikisha maendeleo ya sekta hiyo nchini.
Waziri Chana ametumia fursa hiyo kuzikaribisha kampuni za Hispania nchini kuangalia fursa za uwekezaji katika sekta hizo na usafirishaji huku akisisitiza kuwa Serikali ya Tanzania ina dhamira ya dhati kufanya kazi kwa karibu na Hispania katika kuimarisha zaidi uhusiano baina ya nchi hizo mbili.
Naye, Balozi wa Hispania nchini Tanzania, Jorge Moragas Sánchez amesema kuwa Tanzania na Hispania zina mahusiano ya takribani miaka 16 katika Sekta za utalii, utamaduni, biashara, miundombinu ya maendeleo, maji, usafi wa mazingira, kilimo na kwamba Hispania inafurahia ushirikiano huo.
“Eneo jingine ambalo ushirikiano wetu unang’ara ni Utalii. Uhispania na Tanzania ni nchi zinazojulikana sana kwa uzuri wa maliasili na urithi wake. Kuongezeka kwa idadi ya watalii wanaotembelea Tanzania ni jambo la dhahiri na kuzidi kwa wawekezaji binafsi nchini” amesema Sánchez.
Amefafanua kuwa mahusiano baina ya nchi hizo mbili hayanufaishi tu uchumi lakini pia kukuza kiwango cha uelewano na ushirikiano kati ya watu wa nchi hizo na kusaidia kujengadaraja kati ya mataifa hayo. Hafla hiyo imehudhuriwa na mabalozi mbalimbali, wakuu wa mashirika ya kimataifa na maafisa wa Serikali.