Serikali za Tanzania na Finland zimeahidi kuendelea kuimarisha ushirikiano katika sekta zenye maslahi mapana ya kiuchumi kwa wananchi wa nchi hizi mbili ikiwemo biashara, utalii na uwekezaji.
Ahadi hiyo ilitolewa katika mazungumzo baina ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,Dkt. Stergomena Tax na Waziri wa Uchumi wa Finland, Mhe. Mika Lintilä walipokutana katika ofisi za Wizara jijini Dodoma tarehe 31 Januari 2023.
Katika mazungumzo hayo viongozi hao wamejadili juu ya kuimarisha ushirikiano katika sekta za biashara,uwekezaji, utalii, teknolojia ya habari na mawasiliano, usafirishaji, afya,kilimo, madini, nishati, elimu, mazingira na tafiti ili kupitia sekta hizo wananchi hususan wa Tanzania wanufaike kiuchumi na kijamii.
Dkt. Tax ameeleza kuwa amefurahishwa na ziara ya Mika Lintilä na ujumbe wake nchini ikiwemo ujumbe wa wafanyabiashara alioambatana nao kutoka katika sekta za msingi kwa maendeleo ya pande zote mbili.
“Tanzania na Finland zina ushirikiano wa kihistoria ulioasisiwa kati ya nchi hizo mara baada ya uhuru wa
Tanganyika mwaka 1962. Tupo tayari kuendelea kushirikiana na Finland katika kujenga uchumi wa kidigitali ili kuyafikia mapinduzi ya viwanda” alisema Dkt.Tax.
Vilevile, ametumia nafasi hiyo kuishukuru Serikali ya Finland kwa kuwa mwenyeji wa Mkutano wa 19 wa Nchi za Nordic na Afrika uliofanyika mwezi Juni 2022. Pia ameeleza kuwa Tanzania
itaendelea kushiriki kwenye majukwaa mbalimbali ili kuwasilisha mchango wake katika masuala ya kikanda na kimataifa.
Kwa upande wake, Mika Lintilä ameeleza kuwa Umoja wa Ulaya umetenga fedha kiasi cha Euro Billioni 300 kwa ajili ya kushirikiana na nchi zinazoendelea na zile za Kusini mwa Jangwa la Sahara katika sekta za maendeleo.
Vilevile, ameongeza kuwa tarehe 23 na 24 Februari 2023 kampuni za biashara zipatazo 40 kutoka Finland zitashiriki katika Jukwaa la Wafanyabiashara wa Tanzania na Umoja wa Ulaya litakalofanyika jijini Dar es Salaam.
Wakati huo huo,Waziri Lintilä amekutana na Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara,Dkt. Ashatu Kijaji ambapo viongozi hao wamekubaliana kuimarisha ushirikiano katika masuala ya biashara na uwekezaji ili kukuza uwiano wa
biashara kati ya nchi hizi mbili ambao bado ni mdogo.
Pia Dkt. Kijaji ameongeza kuwa,Tanzania itaendelea kuongeza samani ya bidhaa zake kama mbao,chakula na madini ili kuziwezesha kuingia katika soko la kimataifa ikiwemo Finland.
Waziri Lintilä yupo nchini kwa ziara ya siku nne (4) ambapo ameambatana na kundi la wafanyabiashara wapatao 18 kutoka katika sekta mbalimbali za kiuchumi ili kujionea maeneo mbalimbali ya uwekezaji na biashara.