Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Shirikisho la Ethiopia zimesisitiza juu ya umuhimu wa kutumia fursa za ushirikiano zilizokubaliwa kati ya nchi hizo kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kwa maendeleo endelevu ya watu wake na nchi hizo mbili.
Msisitizo huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa na Mkurugenzi Mkuu wa Idara inayoshughulikia masuala ya Afrika wa Ethiopia, Balozi Jemaludin Mustafa wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Kwanza wa Tume ya Pamoja ya Mawaziri kati ya Tanzania na Ethiopia, ngazi ya Maafisa Waandamizi uliofanyika jijini Addis Ababa, Ethiopia leo tarehe 16 Desemba, 2024.
Akitoa salamu za ufunguzi, Balozi Mussa ameishukuru Serikali ya Ethiopia kwa mapokezi na maandalizi mazuri ya mkutano huo. Pia ameeleza kuwa mkutano huo ni utaratibu rasmi wa kufanya ufuatiliaji wa maeneo mbalimbali ya ushirikiano ambayo nchi hizo mbili zilikubaliana kushirikiana tangu kusainiwa kwa makubaliano ya kuanzisha Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Ethiopia mwaka 2017.
‘’Tanzania na Ethiopia zina fursa nyingi za kiuchumi ambazo bado hazijatumika kikamilifu hivyo, ni matumaini yangu kuwa kupitia majadiliano ya mkutano huu nchi zetu zitapata fursa kufahamishana hali halisi ya utekelezaji wa masuala mbalimbali ya ushirikiano na kufungua maeneo mapya ya ushirikiano kwa maslahi ya pande zote,” alisisitiza Balozi Mussa.
Vilevile, akaainisha kuwa takwimu zilizopo zinaonesha kuwa ushirikiano wa kibiashara upo chini ya dola za kimarekani milioni tano kwa mwaka 2023 na tangu mwaka 1997 Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimesajili miradi ipatayo kumi na tano (15) kutoka Ethiopia yenye thamani ya dola za kimarekani million 17.28. Kadhalika, kwa upande wa Tanzania ni Watanzania wachache wamefanikiwa kuwekeza nchini Ethiopia.
Naye Mwenyekiti Mwenza, Balozi Mustafa alieleza kuwa ushirikiano kati ya Tanzania na Ethiopia ni wa kihistoria tangu enzi za harakati za nchi zisizofungamana na upande wowote (NAM) na hadi sasa kupitia ushirikiano wake wa kikanda katika Umoja wa Afrika (AU).
Aidha, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano huo utaziwezesha Tanzania na Ethiopia kuimarisha ushirikiano katika masuala ya amani na usalama wa kikanda na kimataifa, biashara na uwekezaji, kilimo na utalii.
Mkutano huu wa Maafisa Waandamizi ni mkutano wa awali wa maandalizi ya agenda na nyaraka kwa ajili ya Mkutano wa Tume ya Pamoja ya Mawaziri utakaofanyika tarehe 17 Desemba, 2024 Addis Ababa, Ethiopia. Tanzania na Ethiopia zinashirikiana katika mashauriano ya siasa na diplomasia, ulinzi na usalama, masuala ya kisheria, fedha, biashara, uwekezaji utalii, kilimo, ujenzi wa miundombinu, teknolojia ya Habari na mawasiliano (ICT), afya, elimu pamoja na michezo na utamaduni.
Viongozi wengine walioshiriki mkutano huo ni pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar, Dkt. Aboud Suleiman Jumbe, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Bw. Abdul Mhinte na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Bw. Hussein Mohamed Omar.