▪️Balozi wa Canada apongeza mageuzi makubwa ya sekta ya madini

▪️Wachimbaji wadogo kujengewa uwezo wa uchimbaji madini kwa teknolojia ya kisasa

▪️Mafunzo maalum ya uongezaji thamani kuendeshwa kupitia VETA

▪️Waziri Mavunde asisitiza ushirikiano katika utafiti wa kina wa Madini

Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

Waziri wa Madini Mh. Anthony Mavunde na Balozi wa Canada nchini Tanzania Mh. Emily Burns leo wamekutana Jijini Dodoma na kufanya kikao juu ya maendeleo ya sekta ya madini nchini.

Balozi Emily Burns ambaye pia ametumia kikao hicho kwa ajili ya kujitambulisha,amesema nchi ya Canada ipo tayari kushirikiana na Tanzania katika kuwaendeleza wachimbaji wadogo nchini kwa kuwajengeza uwezo katika uchimbaji wa matumizi sahihi ya Teknolojia utakaozingatia utunzaji wa mazingira na kuwajengea ujuzi ili kuongeza tija kwenye uzalishaji madini.

Aidha Balozi Burns ameonesha utayari wa serikali ya Canada kutoa mafunzo maalum(Tailor-made training) kwa wakinamama na Vijana kupitia vyuo vya Ufundi-VETA katika maeneo ambapo uzalishaji madini unafanyika kwa wingi.

Balozi Burns ametumia pia fursa hiyo kuupongeza uongozi wa Mh. Rais Dkt. Samia S. Hassan kwa mageuzi makubwa yanayofanyika kwenye sekta ya madini hadi kupelekea kuongezeka kwa mchango wa sekta ya madini kwenye pato la Taifa kufikia asilimia 10.1 kwa mwaka 2024.

Waziri Anthony Mavunde ameishukuru serikali ya Canada kwa dhamira yake ya kushirikiana na Tanzania katika kuendeleza sekta ya madini huku msisitizo mkubwa akiuweka katika ushirikiano wa Utafiti wa Kina wa upatikanaji wa madini nchini ili kusaidia upatikanaji wa taarifa sahihi za uwingi wa madini nchini.

Waziri Mavunde pia ameonesha umuhimu wa uwezeshaji wa Wakina mama na Vijana kupitia Programu ya Mining for a brighter Tomorrow(MBT) yenye lengo la kuyawezesha makundi hayo mawili katika ushiriki wake katika uchumi kupitia sekta ya madini.