Nimewahi kujenga hoja kuwa Mtanzania anaposhiriki kwenye uchaguzi haongozwi na msimamo wa kiitikadi wa chama chake cha siasa, bali na masuala mengine ambayo hayapewi uzito na wachambuzi.

Si vigumu kuamini kama nilivyoamini unaposhuhudia mara kwa mara wanachama kuhama chama kimoja cha siasa na kujiunga na kingine, hasa pale wanapofanya hivyo kwa kumfuata kiongozi wanayemuunga mkono na ambaye yeye pia kahamia chama wanachohamia. Hawa ni wapiga kura wanaofuata mtu, hawafuati chama wala itikadi yake.

Pamoja na kwamba tumeshuhudia hii hamahama, kwa kawaida kundi hili huwa ni dogo sana likilinganishwa na sehemu kubwa ya wanachama inayowakilishwa na yule mwanachama kindakindaki ambaye hubaki mwanachama katika mazingira yoyote yatakayomkabili. Huyu ni sawa na abiria atakayebaki ndani ya jahazi linalokabiliwa na dhoruba hata kama nahodha kamkimbia.

Ukweli huu unajitokeza kwenye utafiti wa wanachama wa vyama vya siasa nchini Marekani kwa mujibu wa matokeo ya utafiti wa Donald R. Kinder na Nathan P. Kalmoe yaliyochapishwa kwenye kitabu: Ideological Innocence in the American Public. Siasa ni Sayansi, kwa hiyo upo uhakika mkubwa kuwa pamoja na kuwepo mazingira tofauti kati ya siasa za Marekani na za Tanzania, matokeo ya utafiti huu yanaweza kutumika kutathmini siasa za Tanzania.

Itikadi ni muhimu kwenye siasa kwa sababu ni jambo la kwanza kabisa linalotofautisha chama kimoja cha siasa na kingine. Na ndiyo maana kuna umuhimu wa kuwepo uhakika kuwa wanachama pia wanafuata na wanaunga mkono itikadi ya chama chao. Itikadi ni mkusanyiko wa masuala mengi. Kwa ngazi ya awali kabisa ni mkusanyiko wa maadili, nguzo, misingi, imani na taratibu zinazounganisha kundi moja na kulitofautisha na jingine.

Iwapo tunaunga mkono itikadi moja ya siasa, baadhi ya masuala ambayo hatuna budi kukubaliana nayo ni jinsi gani tunataka jamii isimamie masuala yake, aina ipi ya taasisi zifanye usimamizi huo, nani na kwa njia ipi tutapata viongozi miongoni mwetu, malengo gani yapewe kipaumbele na mfumo upi wa uchumi utafaa kufikia malengo tunayojiwekea.

Pamoja na umuhimu mkubwa wa itikadi katika kuongoza maisha ya mpiga kura, jambo la msingi linalobainishwa na watafiti ni kuwa suala la itikadi linapewa uzito na wasomi tu, lakini halina umuhimu mkubwa kwa wapiga kura. Aidha, utafiti unabaini, hata baadhi ya viongozi wanaosema itikadi ni suala la msingi hawana uwezo mkubwa na kuelezea kwa umahiri na ufasaha ni itikadi ipi ambayo inafuatwa na chama chao.

Katika muktadha wa siasa, simulizi ya kwamba nahodha anaweza kuchupa baharini na kuachana na jahazi aliloongoza na kuwaacha abiria ndani ya chombo, ni kusema pia kuwa chama kinaweza kikabadilisha itikadi lakini wanachama wengi wakabaki na wakaendelea kujitambulisha na chama ambacho kimeachana na itikadi yake ya awali.

Inalazimu kuuliza kuwa kama itikadi si muhimu kwa mpiga kura, nini hasa suala la msingi? Utafiti unabaini kuwa wengi wetu tunafuata chama cha siasa ambacho ndugu, jamaa na marafiki zetu wamekwisha kujiunga nacho na tunatafuta zaidi mazingira ambayo hayatutofautishi sana na wale wanaotuzunguka.

Kama huu ndiyo ukweli, hii hali si salama hata kidogo kwa mpiga kura. Lakini si lazima kukubali hali halisi. Ni jambo moja kukubali kuwa mpiga kura hajali sana itikadi inayomuongoza, iwe kwa ngazi ya chama chake au kwa ngazi ya serikali iliyopo madarakani. Na ni suala moja pia kusema kuwa inawezekana kuwa kuna baadhi ya viongozi hawana hata chembe ya fununu juu ya itikadi wanayoisimamia. Lakini ukweli huu haufuti uwezekano kuwa wapo viongozi, ingawa ni wachache, ambao wamejitokeza na watajitokeza kutafuta nafasi za uongozi wakiwa na nia ya kutekeleza itikadi ambayo haikuwa dhahiri kwa sababu tu ya kwamba mpiga kura hakuona umuhimu wa kutafuta ufafanuzi wa kutosha kutoka kwa wagombea.

Mpiga kura alichungulia ndani ya basi la chama kimoja cha siasa akakuta limejaa jamaa, marafiki, majirani zake na watu wengine anaowafahamu na akaingia kwenye safari ambayo hakufahamu hata inampeleka wapi. Ni kwa kudra za Mwenyezi Mungu tu kuwa atafika mwisho wa safari na ataridhika kuwa ni sehemu aliyotaka kwenda.

Hali ambayo italeta uhakika wa matokeo ambayo yana manufaa kwa wengi ni kuwepo kwa mpiga kura ambaye anafahamu vya kutosha umuhimu wa itikadi inayosimamia maisha yake na jinsi gani hiyo itikadi itatimiza malengo yake na ya jamii.

Hata kama anaongozwa na viongozi ambao hawana mwelekeo wowote wa itikadi, hao watalazimika tu kunoa mwelekeo huo kwa msukumo wa wapiga kura wao.

Siamini kama watafiti waliobaini kuwa uelewa wa itikadi si muhimu kwa wapiga kura wanasema pia kuwa uelewa wa itikadi si muhimu kwa jamii. Uelewa wa itikadi ni muhimu sana kwa mpiga kura anayetaka kufahamu anapelekwa wapi, na uelewa huo unampa silaha ya kuwahoji viongozi wamhakikishie wanafahamu wanapoelekea ili kuwa na uhakika kuwa wote wanakubaliana na malengo ya safari hiyo.

Kwa chama cha siasa chenye wanachama wenye kufahamu vema itikadi inayowaongoza, ni kinga dhidi ya chama kupokonywa uongozi na mtu ambaye anaongozwa na itikadi isiyokubalika.