▪️Balozi wa Belarus aeleza utayari wao kubadilishana utaalam kwenye teknolojia*
▪️Waziri Mavunde anadi uwepo wa madini mbalimbali kuvutia wawekezaji zaidi.*
▪️Apigia debe mitambo na teknolojia kwa wachimbaji wadogo
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde leo tarehe 24 Oktoba, 2024 amekutaja na kufanya mazungumzo na Balozi wa Belarus nchini Tanzania, Pavel Vziatkin.
Katika mazungumzo hayo, Balozi Pavel amebainisha kuwa lengo la ziara yake ni kuendelea kuimarisha diplomasia ya uchumi baina ya Belarus na Tanzania, kuzifahamu zaidi fursa zinazopatikana katika sekta ya madini nchini Tanzania na kuonesha namna Belarus ilivyopiga hatua katika teknolojia na utengenezaji wa mitambo imara inayoweza kutumika katika sekta ya madini.
Akimkaribisha Balozi Pavel, Waziri Mavunde alieleza kwamba Nchi ya Tanzania imebarikiwa uwepo wa madini ya aina mbalimbali yakiwemo ya metali, Vito na madini mkakati na kusisitiza kuwa zipo fursa lukuki ambazo wawezekaji kutoka Belarus wanakaribishwa kuja kuwekeza katika sekta ya madini nchini.
Alimweleza kuwa, kupitia falsafa ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 4R iliyoweka msingi wa mazingira mazuri ya uwezekezaji, tumeendelea kupata wawekezaji wengi nchini na kuwakaribisha wawekezaji kutoka Belarus kuchangamkia fursa hiyo.
Aidha, Mheshimiwa Mavunde alimweleza Balozi Pavel kwamba Tanzania imepiga marufuku ya kusafirisha madini ghafi nje ya nchi, hivyo ni fursa kwa wawekezaji kuanzishwa viwanda vya kuongeza thamani ya madini hapa nchini.
Vilevile, Waziri Mavunde alibainisha kuwa Tanzania ina wachimbaji wakubwa wanaotumia teknolojia za kisasa na wadogo ambao bado wanatumia zana duni, na hivyo kumwomba Balozi Pavel kuangalia uwezekano wa kuzalisha mashine za bei nafuu ambazo zitarahisha shughuli za wachimbaji wadogo ambao wameendelea kuwa na mchango mkubwa kwa uchumi wa Taifa letu.
Kwa upande wa madini mkakati na muhimu, Waziri Mavunde alionesha kuwa ipo miradi zaidi ya 12 katika hatua za mwisho ili ianze uzalishaji na kusisitiza itakapoanza itakwenda kuiweka Tanzania katika ramani ya nchi zenye uzalishaji mkubwa wa madini mkakati na muhimu Barani Afrika.
Mwisho, Waziri Mavunde alitumia fursa ya mazungumzo hayo kukaribisha wawekezaji na makampuni mbalimbali kutoka Nchini Belarus kuja kushiriki Mkutano wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini (TMIC) unaotaraji kufanyika tarehe 19 hadi 21 Novemba, 2024 Jijini Dar es Salaam na kusisitiza kuwa itakuwa ni nafasi ya makampuni ya Belarus kufahamu zaidi fursa zilizopo nchini kwenye sekta ya madini.