Wakati dunia ikiingia kwenye teknolojia mpya ya 5G katika intaneti ambayo tayari imeshafanyiwa majaribio kwenye baadhi ya nchi, Tanzania bado inasusua kwenye matumizi ya teknolojia ya nyuma yake ya 4G na kusambaza mitandao inayowezeshwa na masafa hayo yaliyoanza kutumika mwaka 2006.
5G na 4G ni mwendelezo wa vizazi vya teknolojia za 3G na 2G ambazo zilileta mapinduzi makubwa kwenye matumizi ya simu za mkononi na kuwezesha upatikanaji wa intaneti bila kutumia nyaya.
Tofauti ya vizazi hivi vya teknolojia ya mawasiliano ni kasi yake kubwa na wingi wa huduma za kimtandao ambao kila moja wapo inaweza kutoa.
Yenye uwezo wa chini kabisa ni 2G, ambayo ilianza kutumika duniani mwaka 1991 ikiwa ni teknolojia ya kwanza kuwezesha intaneti kupatikana bila kuunganishwa na nyaya, na ambayo kwa hivi sasa ndiyo iliyosambaa sana kwenye nchi zinazoendelea kama Tanzania.
Ripoti ya mwaka jana ya Umoja wa Makampuni ya Simu Duniani (GSMA) inaonyesha kuwa mitandao inayowezeshwa na 2G ilikuwa imesambaa kwa asilimia 90 humu nchini mwaka 2018, ikiwa ni nchi ya tatu kwenye nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Kinara wa 2G kwenye ukanda huu wakati huo ilikuwa Rwanda ambako upatikanaji wa teknolojia hiyo ulikuwa umefikia asilimia 100. Ya pili ilikuwa Kenya iliyokuwa na kiwango cha asilimia 95 huku Uganda ikiwa ya nne na asilimia 86.
Kwa upande wa 3G na 4G, matumizi yake Tanzania mwaka 2018 yalikuwa ni asilimia 61 na 28 mtawalia. GSMA inasema katika ripoti yake ya mwaka 2019 iitwayo ‘Uchumi wa Kimtandao wa Afrika’ kuwa kiwango cha kuenea kwa 4G nchini ni miongoni mwa viwango vidogo sana duniani.
Miongoni mwa wanachama wa EAC, Tanzania bado inashika nafasi ya tatu katika kusambaza na kutumia teknolojia ya 4G nyuma ya Rwanda yenye asilimia 99 na Kenya ambayo imefikia asilimia 61, huku Uganda ikiwa ya mwisho ikiwa na asilimia 23. Watu wanaofikiwa na teknolojia ya 3G kwenye nchi hizi tatu ni asilimia 95 kwa Rwanda, Kenya asilimia 88 na Uganda asilimia 78.
Kwa mujibu wa wadau wa sekta ya mawasiliano, kuwapo kwa teknolojia hizi kumesaidia sana kusambaza huduma za intaneti na kurahisisha matumizi ya data ambayo ni muhimu sana kwa biashara ya pesa mtandaoni na vitu kama mitandao ya kijamii.
Takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zinaonyesha kuwa hadi kufikia Disemba mwaka jana watumiaji wa intaneti nchini walikuwa takriban milioni 25.8 ukilinganisha na milioni 14.2 mwaka 2014.
Kati ya hawa, wengi ni wale wanaopata mtandao huu maarufu kwa kutumia vifaa visivyounganishwa na nyaya kama vile simu mtelezo, maarufu ‘simu janja’, vinavyowezeshwa na teknolojia za kizazi cha 3G na 4G.
“Unapozungumzia matumizi ya data, lazima ugusie upatikanaji wa huduma za intaneti na teknolojia za 3G na 4G lakini pia ili mtu kufurahia data za 3G na 4G lazima uwe na kifaa kinachokubaliana na data,” Mkuu wa Idara ya Mauzo na Usambazaji wa Kampuni ya Vodacom Tanzania, George Lugata, ameliambia JAMHURI hivi karibuni.
“Vodacom iko mstari wa mbele katika kuongeza idadi ya matumizi ya teknolojia hizi nchini. Kwanza mtandao wetu wa Vodacom umewafikia asilimia 92 ya Watanzania kwa masafa ya 3G, kupitia minara yetu zaidi ya 2,500 na 4G yenye minara zaidi ya 100 na 4G+ yenye minara zaidi ya 62,” anaongeza.
Takwimu za TCRA pia zinaonyesha kuwa kabla ya kuzimwa simu ambazo hazikusajiliwa kwa alama za vidole mwezi uliopita, huduma ya pesa mtandaoni ilikuwa na wateja karibu milioni 25.9 huku miamala ya biashara hiyo ikifikia Sh trilioni 9.5 mwezi Disemba mwaka 2019.
Hadi mwishoni mwa mwaka jana, laini za simu zilizokuwa sokoni zilikuwa milioni 48. Hii ni zaidi ya mara mbili ya laini zilizokuwepo mwaka 2010, wadau wakihusisha ongezeko hili kubwa na ujio wa teknolojia bora na za kisasa zaidi kama 4G.
Taarifa zilizopo zinaonyesha kuwa TCRA inazitaka kampuni za simu kuakikisha kuwa teknolojia za aina hii ambazo zinawezesha intaneti kupatikana bila nyaya zinasambazwa kwa kasi ili kufikia asilimia 90 mwaka 2024.
Ili kufikia lengo hilo, kampuni za simu za mikononi nchini zinaendelea kuwekeza kwenye masafa hayo huku kampuni nyingine kama Halotel Tanzania zikiweka malengo hata ya 5G, teknolojia itakayozidisha kasi ya kutuma data kupitia intaneti hadi mara mia zaidi ya 4G.
Masafa ya 5G ambayo kasi ya mawimbi yake ni kubwa sana itawezesha kuunganisha mabilioni ya vifaa kupitia intaneti huku huduma za kiroboti na kiautomatiki zikisaidia kupunguzia watu gharama na muda.
Wataalamu wanasema teknolojia hii mpya itamuwezesha mtu kufuatilia na kusimamia mali yake yote kama simu, kompyuta, kamera, televisheni, benki, elimu, uwekezaji na biashara nyinginezo kupitia intaneti ya moja kwa moja.
Katika mahojiano maalumu na JAMHURI mwishoni mwa mwaka jana, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Halotel Tanzania, Nguyen Anh Son, alisema kampuni yao mama ya Viettel tayari imeanza kufanya majaribio ya 5G kwenye baadhi ya masoko yake. Pamoja na Tanzania, kampuni hiyo inayomilikiwa na Jeshi la Vietnam pia inafanya biashara nchini Myanmar, Burundi, Peru, Msumbiji, Cameroon, Timor ya Mashariki, Haiti, Cambodia na Laos.
Nguyen alisema kwa Tanzania wana mpango wa kuomba leseni ya majaribio ya 5G, hii ikiwa ni miongoni mwa mipango ya Halotel ya mwaka 2020.
“3G na 4G na sasa 5G, ni teknolojia ambazo zina kasi nzuri ya intaneti,” anasema Jackson Mbando, Meneja Uhusiano wa Airtel Tanzania, ambayo mwanzoni mwa mwezi huu ilitangaza kuanza kupanua mtandao wake wa 4G baada ya kupata rasmi leseni ya kutumia teknolojia hiyo.
Uwekezaji huo wa kiasi cha dola milioni 12 za Marekani unategemewa kuisaidia kampuni hiyo kuongeza masafa yake ya 4G maradufu na idadi ya wateja wanaotumia mtandao wake.