Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
MKURUGENZI wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade ), Latifa Khamis ameongoza zoezi la upokeaji na majadiliano ya matokeo utafiti wa awali wa hali ya biashara nchini.
Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam leo Machi 11, 2024 Latifa amesema kuwa utafiti huo wa hali ya biashara nchini ulifanyika mwaka 2023 katika mikoa saba ya bara na visiwani.
Akiiitaja hiyo ni pamoja na Dar es Salaam, Mwanza, Dodoma, Mbeya, Arusha na Unguja .
Amesema mbali na mikoa hiyo pia jumla ya makampuni 334 yaliyosajiliwa na Wakala wa Usajili Biashara na Leseni (BRELA ), pamoja na Wakala wa Usajili wa Biashara na Mali (BPRA) kwa upande wa Zanzibar yalifanyiwa utafiti huo.
“Katika utafiti huu sekta 10 zilihusika katika ukusanywaji wa takwimu hizo ambazo ni sekta ya kilimo, uvuvi, madini, utalii, viwanda, Ujenzi, Huduma ya fedha na bima pamoja na biashara za jumla reja reja”amesema Latifa
Aidha amesema kuwa utafiti huu utaleta matokeo ambayo yatatumika kama fursa katika kuishauri serikali na wadau mbalimbali wa biashara.
Pia amewapongeza wadau walioshiriki katika zoezi la ukasanyaji takwimu za utafiti huo wa awali.
Wadau hao ni pamoja na Ofisi ya Takwimu (NBS), Wakala wa Usajili na Leseni (BRELA), Ofisi ya mtakwimu mkuu seikali Zanzibar (OCGS), Wakala wa Usajili Mtandao (Ega), Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti (ipsos Tanzania), pamoja na wakuu wa mikoa utafiti ulipofanyikia, huku pongezi za dhati zikienda Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na Taasisi ya TanTrade.