Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) umenunua mtambo wa kisasa wa kukagua madaraja marefu yenye maji na kurahisisha shughuli hiyo, tofauti na njia iliyokuwa ikitumika awali ya kutumia kamba iliyohatarisha maisha wataalamu.
Mtambo huo wa kisasa (Bridge Inspection Vehicle) ambao umeanza kutumika Tanzania, kwa Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, umegharimu Sh. bilioni 1.2 na utatumika kupima madaraja mbalimbali nchini.
Mhandisi wa Miradi wa Tanroads, Mkoa wa Pwani, Obed Panga, anasema mtambo huo wa kisasa utatumika kukagua madaraja yanapokuwa katika hali zote yale yaliyoharibika na yaliyoko katika hali nzuri ili kubaini kama yana tatizo lolote yafanyiwe marekebisho.
Mhandisi Panga anasema kazi ya upimaji wa madaraja hufanyika mara moja kwa mwaka, hivyo kupatikana kwa mtambo huo kumerahisisha kazi hiyo na kuwaepusha na hatari wataalamu waliotumia kamba ili kuingia chini ya madaraja hayo kufanya ukaguzi.
Anasema mwaka huu wamefanya ukaguzi katika madaraja ya Ruvu na Wami na kwamba wanatarajia kufanya ukaguzi kwenye madaraja mengine makubwa na yenye maji likiwamo Daraja la Mkapa.
Naye Meneje wa Tanroads Mkoa wa Pwani, Mhandisi Tumaini Sarakikya, amewataka madereva kuheshimu alama za barabarani na kutozidisha mizigo katika magari yao ili kuepuka uharibifu wa barabara.
Mhandisi Sarakikya akiwa katika mzani wa Vigwaza, amewaeleza waandishi wa habari waliotembelea mzani huo wa kisasa wenye urefu wa mita 22, kwamba umeondoa msongamano wa magari katika eneo hilo tofauti mzani uliokuwa ukitumika awali.
Anasema kwa sasa upimaji wa gari moja huchukua muda wa dakika moja tu, tofauti na mzani wa awali ambako upimaji wa gari moja ulichukua dakika tano au zaidi na kusababisha msongamano mkubwa wa magari.
Mhandisi huyo anasema kwa siku wanapima uzito magari 1,800 hadi 2,000 na kutoa elimu kwa madereva kuhusu namna bora ya kutumia mizani na kufuata maelekezo ya alama za barabarani.
“Gari lililozidisha uzito au linalokwenda kwa mwendo kasi wa zaidi ya 50 kama ulivyoelekezwa kwenye kibao hiki cha alama za barabara, yanaelekezwa na taa iliyopo mbele ukiingia ofisini ili kuhakiki upya uzito na iwapo itabainika umezidi kulingana na ule ulioruhusiwa, dereva hutozwa faini na wanaoendesha kwa mwendo kasi wanaelimishwa,” anasema.
Hata hivyo, anasema madereva wanaokwepa kupita kwenye mzani wanavunja sheria na wanapokamatwa hutozwa faini ya dola za Marekani 2,000 kwa kosa hilo. Pia kabla ya kutenda kosa hilo wanapaswa kuelewa kwamba kuna kamera zinazonasa kila tukio katika barabara hiyo.
Naye Mhandisi Japhet Kivuyo anasema uzito ulioruhusiwa katika barabara zetu mwisho ni tani 56 na wanaozidisha kiwango hicho wanalipa faini au kutakiwa kupunguza mzigo na kwamba kwa kuchukua mizigo mizito wanaharibu barabara ambazo hutengenezwa kwa gharama kubwa.
Anasema magari yenye uzito wa kuanzia tani 3.5 kama yamepakia mzigo ni lazima yapite kwenye mzani kwa ajili ya kuhakiki uzito uliopo na pia kupata maelekezo kutoka kwa wataalamu kuhusu matumizi bora ya barabara.
Kwa upande mwingine, Msimamizi Mkuu wa Kituo hicho, Godo Biwi, anasema mzani huo wa kisasa umerahisisha utendaji kazi na kupunguza msongamano wa magari eneo hilo tofauti na ule uliokuwa unatumika kabla ya huu.
Anasema matatizo yaliyokuwa yanalalamikiwa awali ikiwamo rushwa yamedhibitiwa kwa kiasi kikubwa, kwani si rahisi kwa mfanyakazi yeyote kupokea rushwa katika eneo hili licha ya kwamba vitendo vya rushwa mara nyingi ni tabia ya mtu binafsi.