Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Morogoro
Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) umeanza kutekeleza maagizo ya Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa aliyoyatoa Februari 22, 2024 wakati wa ziara yake ya siku Nne mkoani Morogoro ya kukagua miundombinu ya barabara ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kumtaka waziri huyo kufika kusiko fikika ili kutatua kero za wananchi hususani miundombinu ya Barabara.
Akizungumza mara baada ya kukagua barabara ya kutoka Gairo kwenda Kilindi mkoani Tanga Bw Adam Msovela ambaye ni Mhandisi Mwandamizi TANROADS Mkoa wa Morogoro amesema kuwa (TANROAD) imefanya usanifu wa kina wa madaraja hayo ili yawe ya viwango na yaweze kutumika pia wakati watakapoamua kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami.
Mhandisi Msovela amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika hatua za mwisho kuanza kujenga madaraja mawili ya Chakwale na Nguyami Wilayani Gairo ili kuwaondolea kero ya muda mrefu wananchi wa maeneo hayo.
“Ujenzi wa madaraja haya mawili ya Chakwale na Nguyami utaanza hivi karibuni mara baada ya mkandarasi kupatikana kwani Serikali ya Awamu ya Sita na uthamini wake kwa wananchi tayari imetenga fedha kwa ajili ya kazi hii” amekaririwa Mhandisi Msovela na kuongeza kuwa.
Daraja la Chakwale lina urefu wa mita 80 na lile la Nguyami likiwa na urefu wa mita 100 na ujenzi wake utafanyika kwa lengo la kuwaondolea wananchi kero ya kupoteza Maisha wakati wa kuvuka pamoja na kupoteza mali zao.
Kwa upande wa baadhi ya wananchi ambao ni watumiaji wa barabara hizo wameipongeza Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali katika kuwaletea maendeleo yao kwenye sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya Miundombinu.
Kwa nyakati tofauti wananchi hao Maneno Kashinde na Mussa Mtwale wakazi wa kata na kijji cha Chakwale, Magreth Thomas mkazi wa kijiji cha Nguyami-Ilala, Bw Hussein Salum ambaye ni dereva, Ismail Mussa Mtwale ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Tawi la Nguyami wameishukuru serikali kwa kuamua kuanza ujenzi wa madaraja hayo kwa kuwa yamepoteza Maisha ya watu wengi kwa kuchukuliwa na maji Pamoja na mali zao na kwamba Barabara hiyo ndiyo Barabara inayotumika Kwenda Makao makuu ya Wilaya ya Gairo.