Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema Wizara kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) inatarajia kuanza kutekeleza mradi wa kimkakati wa Ujenzi wa Daraja la Jangwani.
Bashungwa ameyasema hayo Bungeni jijini Dodoma wakati wa kuwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara na Taasisi zake kwa mwaka wa Fedha 2024/25.
Amesema mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa maendelezo ya Bonde la Mto Msimbazi.
Bashungwa amesema daraja hilo litakalojengwa lina urefu wa mita 390 pamoja na Barabara unganishi zenye urefu wa mita 710 na kina cha mita 15.5 kutoka usawa wa bahari.
“Daraja hili litakapokamilika litatatua changamoto ya kujaa kwa maji katika barabara ya Dar es Salaam-Morogoro eneo la Jangwani wakati wa mvua na kusababisha kufungwa kwa barabara hiyo mara kwa mara.”, ameongeza Bashungwa.
Bashungwa amesema tathmini ya zabuni ili kumpata Mkandarasi na Mhandisi Mshauri zinaendelea.