Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia,Kibaha

Mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali mkoani Pwani zimesababisha kumomonyoka kwa kingo za kalavati na barabara ya Kimange-Chalinze upande wa kutokea Dar es Salaam.

Kutokana na athari hiyo kumesababisha miundombinu hiyo ya barabara kutokuwa salama kwa matumizi , msongamano wa magari kupita upande mmoja pekee .

Mkuu wa Mkoa Pwani Abubakar Kunenge amefika Kimange -Chalinze-Segera kukagua na kujionea ujenzi wa kalavati hilo ambalo liliharibiwa na mvua kubwa zilizonyesha April 15.

Kunenge ameeleza Serikali inaendelea kerejesha barabara hiyo katika hali yake ya kawaida na kazi ya Ujenzi wa eneo kwa kutumia zege .

Amewataka watumiaji wa Barabara kutii maelekezo ya Jeshi la polisi la kutumia upande mmoja wakati wakisubiri zege kukauka.

Nae Meneja wa TANROADS Pwani Mhandisi Baraka Mwambage ameeleza, wanaendelea kufanya kazi usiku na mchana kunusuru uharibifu wa miundombinu hiyo usiongezeke na tayari wapo kazini kuendelea na ujenzi wa eneo hilo kwa kutumia zege .