Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Geita
Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imetekeleza maelekezo ya Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa kwa kukamilisha Upembuzi Yakinifu na Usanifu wa Kina wa Barabara ya Ushirombo – Nyikonga – Katoro (58km). Kipande cha Nikonga – Kashelo (10.48km) pamoja na Daraja la Nyikonga, kipande cha Kashelo – Ilolangulu (15.0km) na kipande cha Ushirombo (Kilimahewa) – Nanda (15.57km) vyenye jumla ya km 41.05 vipo kwenye hatua ya kumtafuta Mkandarasi wa kuanza Ujenzi kwa kiwango cha Lami.
Vilevile Serikali ipo katika maadalizi ya kutangaza kipande cha barabara ya Ushirombo – Kashelo (22.5km) ili kumpata Mkandarasi wa kuanza Ujenzi kwa kiwango cha Lami Waziri Bashungwa alitoa maelekezo hayo kwa TANROADS tarehe 08 Juni, 2024 katika mkutano wa hadhara wa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati ambaye pia ni Mbunge wa Bukombe, Dkt. Dotto Biteko katika Kata ya Katome Mkoani Geita.
Akizungumza mara baada ya kutembelea na kukagua miradi mbalimbali, Kaimu Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Geita Mhandisi Fredrick Mande amesema kuwa Katika kipindi cha miaka mitatu ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan miradi mbalimbali ya maendeleo imetekelezwa ikiwa ni Pamoja na miradi ya matengenezo.
Mhandisi Mande amesema kuwa barabara ya Ushirombo – Nyikonga – Katoro ni muhimu kwa ajili ya kuimarisha uchumi katika wilaya za Bukombe (Ushirombo), Mbogwe na Geita DC na ni Barabara unganishi ya Mkoa wa Geita na Shinyanga (Kahama).
Ameeleza kuwa TANROADS mkoa wa Geita inahudumia jumla ya Km 1,019.13 za Barabara Kuu na Barabara za Mkoa. Kati ya hizo, Km 401.98 ni barabara za lami sawa na asilimia 39.4 na sehemu iliyobaki yenye urefu wa Km 617.15 ni barabara za changarawe sawa na asilimia 60.6.
Hata hivyo ameitaja miradi inayotekelezwa na TANROADS Mkoa wa Geita kuwa ni Pamoja na Uwekaji wa taa 147 za barabarani katika Mji wa Geita na Katoro katika barabara kuu ya Nyamhama (Kagera/Geita BDR) – Ibanda (Geita/Mwanza BDR) kwa gharama ya Shilingi Milioni 658.980
Mhandisi Mande amesema kuwa kwa kutumia fedha zilizotengwa kutoka Mfuko wa Barabara, Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Geita ilitekeleza matengenezo ya aina mbalimbali katika barabara na madaraja. Jumla ya mikataba 51 ya miradi ya matengenezo ya barabara na madaraja yenye thamani ya Shilingi bilioni 10.309 inatekelezwa katika Mwaka wa Fedha 2023/24. Hadi sasa kwa mwaka wa fedha 2023/24, jumla ya fedha ambazo zimepokelewa ni Shilingi bilioni 4.069.36 (sawa na 39.5% ya bajeti, Shilingi bilioni 10.309).
Mhandisi Mande amesema kwa kutumia fedha zilizotengwa kutoka Mfuko wa Maendeleo, Wakala ya Barabara (TANROADS) Mkoa wa Geita inatekeleza matengenezo ya aina mbalimbali katika barabara na Kiwanja cha ndege cha Geita – Chato.
Hali kadhalika Mhandisi Mande amesema kuwa Serikali kupitia Wakala ya Barabara (TANROADS) imesaini Mkataba wa Ujenzi wa Barabara kwa kiwango cha Lami wa Barabara ya Sungusila – Nzera – Nkome Port (20km) na Mkandalasi China Communications Construction Company Ltd (CCCC) ya China kwa gharama ya fedha za Kitanzania Bilion 42.14 ambao wapo katika muda wa maandalizi ya kuanza Ujenzi.
Ameitaja miradi ambayo ipo katika upembuzi yakinifu na Usanifu wa kina kuwa ni Pamoja na barabara ya Geita – Nzera – Nyamadoke yenye urefu wa Kilomita 58.3 ambao umefikia asilimia 30 kwa gharama ya shilingi milioni 606.85 pamoja na Upembuzi Yakinifu na Usanifu wa kina wa barabara ya Mtakuja – Buhalahala (Geita Mjini) kilomita 24 ambao umefikia asilimia 57 kwa gharama 287.57