Vyama vya upinzani vilivyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) katika Bunge Maalum la Katiba vimesusia vikao vya bunge hilo tangu Aprili 16, mwaka huu.

Wapinzani wametoa sababu zao za kuchukua hatua hiyo. Kwa mfano, wamesema Rais Jakaya Kikwete na Waziri wa Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi, wametoa vitisho kwamba kukiwapo Serikali tatu Jeshi litachukua nchi.

Lakini kama sababu ni hiyo basi wapinzani wangesusia vikao vya Bunge Maalum la Katiba tangu siku Rais Kikwete alipozindua bunge hilo.

Vile vile wapinzani wamedai kuwa wamesusia vikao vya Bunge Maalum la Katiba kwa sababu kumekuwa na matusi na lugha chafu ndani ya bunge hilo. Lakini wapinzani wasituaminishe kwamba hawakushiriki katika kutoa matusi na lugha chafu.

Basi kuna sababu ambayo wapinzani hawakuiweka wazi ya uamuzi wao wa kususia vikao vya Bunge Maalum la Katiba.

Kama tunavyokumbuka wapinzani waliunda umoja wao [UKAWA] kwa lengo la kupigania mfumo wa Serikali tatu ambao inadaiwa ni wananchi waliopendekeza kwenye Tume ya Warioba.

Wapinzani walitaka kutuaminisha kwamba wanawapenda sana wananchi. Lakini tangu lini wapinzani wanawapenda wananchi?

Kwa jumla Bunge Maalum la Katiba lililoanza kukutana Dodoma Februari 18, mwaka huu, limetusaidia kujua mambo ambayo hatukubahatika kuyajua huko nyuma. Binafsi hilo limenisaidia kujua mambo mawili.

La kwanza, kwamba wapinzani wana uelewa mdogo wa mambo. Na hii inatofautiana na kauli zao za siku nyingi kwamba wao ndiyo wajuaji peke yao na tunaobaki hatujui chochote.

La pili, kwamba wapinzani wanawapenda sana wananchi.

Nianze na kutaja sababu ya kutamka kwamba wana uelewa mdogo wa mambo. Tazama! Wanaunda UKAWA kwa lengo eti la kupigania maoni waliyotoa wananchi mbele ya Tume ya Warioba.

Kwa sababu mbili wapinzani hawana haki ya kutetea maoni ya wananchi.

Kwanza, hili ni Bunge Maalum la Katiba si bunge la kawaida wanavyoliona. Pale wapinzani hawawakilishi wananchi. Hawapo pale kupigania maoni ya wananchi bali kuyafanyia kazi maoni ya wananchi waonavyo wao.

Pili, wapinzani hawana haki yoyote ya kupigania maoni ya wananchi wa kawaida kwa sababu tayari katika Bunge Maalum la Katiba kuna wajumbe wanaowawakilisha wananchi wenzao.

Pale kuna wajumbe 20 wanaowawakilisha wenye ulemavu, wajumbe 19 wanaowawakilisha wafanyakazi, wajumbe 20 wanaowawakilisha wakulima, wajumbe 10 wanaowakilisha wafugaji, wajumbe 10 wanaowawakilisha wavuvi, na wajumbe 20 wa makundi yenye malengo yanayofanana.

Hawa ndiyo wananchi tuliowatazamia kuunda Umoja wa Katiba ya Wananchi. Kwa hivyo, Umoja wa Katiba ya Wananchi ulioundwa na wapinzani ni feki. Tukubaliane kwamba si Umoja wa Katiba ya Wananchi, ni Umoja wa Katiba ya Wapinzani.

Kwa hiyo, ingekuwa ni hawa wananchi walioko bungeni ndiyo waliopendekeza kwenye Tume kuwe na Serikali tatu hawa ndiyo wangechachamaa kupigania maoni yao. Lakini wamekuwa watazamaji!

Wanaochachamaa ni wapinzani! Basi ni hawa wanaochachamaa waliopendekeza kuwe na Serikali tatu.

Kwamba wapinzani wanapigania Serikali tatu kwa niaba ya wananchi ni uongo na unafiki wa kutupwa! Ni katika mazingira hayo najiuliza; tangu lini wapinzani wanawapenda wananchi kiasi hicho?

Wanatumia akili yao yote, nguvu zao zote, na ujuzi wao wote kupigania Serikali tatu eti kwa niaba ya wananchi! Tangu lini wananchi wamependwa na wapinzani kiasi hicho?

Wakulima na wafugaji wameendelea kuuana. Lakini wapinzani hawajaunda umoja wa amani ya wakulima na wafugaji. Upendo uko wapi?

Wakulima wameendelea kukopwa mazao yao na wanapewa malipo ya chini sana kwa mazao yao. Wapinzani hawajaunda umoja wa uchumi wa wakulima. Na wanawapenda sana!

Watoto wa maskini wanapewa elimu ya ovyo ovyo shuleni. Wanapelekewa vitabu vibovu shuleni. Fedha ya rada imetumika vibaya kununua vitabu vibovu. Na fedha ya rada iliyotengwa kwa ajili ya madawati inaonekana imeliwa.

Hatusikii madawati yanasambazwa upande gani. Na wapinzani hawajaunda umoja wa elimu ya watoto wa maskini!

Hospitalini hakuna dawa. Wagonjwa wengine wanalala hospitali sakafuni. Wapinzani hawajaunda umoja wa afya ya wananchi!

Katika hali hiyo yote, upendo wa wapinzani kwa wananchi uko wapi? Uko kwenye madai ya Serikali tatu tu? Kwani Serikali tatu zina manufaa gani kwa mwananchi wa kawaida?

Wananchi wa kawaida ni watu wa kutawaliwa tu. Hawana maslahi yoyote ama na Serikali tatu au Serikali 100.

Kwa hivyo, nadhani kuna umuhimu wa kuthibitisha kwa njia mbalimbali kwamba waliopendekeza kuwe na Serikali tatu ni wapinzani na mashabiki wao, si wananchi wa kawaida.

Kwanza, wananchi wa kawaida hawajaona faida au hasara ya kuwa na Serikali mbili. Kwa hiyo, hawawezi kupendekeza Serikali tatu.

Pili, Umoja wa Katiba ya Wananchi ungeundwa na wawakilishi wa wananchi walioko kwenye Bunge Maalum la Katiba. Lakini umeundwa na wapinzani!

Tatu, idadi ya wananchi waliotoa pendekezo la kuwa na Serikali tatu ni ndogo sana. Kwa hiyo, pendekezo hilo limetolewa na wapinzani.

Nne, UKAWA umepanga kuzunguka nchi nzima kupigania Serikali tatu. Ya nini kuwaendea wananchi ambao tunaaminishwa kwamba ndiyo waliopendekeza kuwe na Serikali tatu?

Maana yake ni kwamba lengo la wapinzani kwenda mikoani ni kutafuta kuungwa mkono na wananchi.

Tano, wananchi walioko mikoani wanajua kinachoendelea kwenye Bunge Maalum la Katiba. Hivyo, kama wangeona kwamba maoni yao kuhusu Serikali tatu hayazingatiwi basi ni wao ambao wangewafuata wapinzani Dodoma. Kinyume chake ni wapinzani wanawafuata wananchi mikoani!

Inavutia kuona kwamba watu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) hawakuficha kitu. Wao wameeleza waziwazi kuwa sera yao ni ya Serikali mbili. Kwa upande wao wapinzani wanadai wao hawana sera. Eti sera ya Serikali tatu ni ya wananchi! Hapana.

Pengine siyo vibaya kuwatahadharisha wawakilishi wa wananchi wa kawaida walioko kwenye Bunge Maalum la Katiba na wananchi walioko mikoni.

Hoja ya Serikali tatu imetekwa na inapigiwa kelele na wapinzani kwa sababu wana maslahi nayo. Wanaamini kabisa kwamba kukiwapo Serikali tatu moja itakuwa yao. Hawapiganii maslahi ya Taifa wala ya wananchi wa kawaida. Wanapigania madaraka!

Ukitaka kusema kweli, wapinzani walifanya makosa kuunda Umoja wa Katiba ya Wananchi. Kwanza, kitendo hicho kilikuwa cha ubaguzi ndani ya Bunge Maalum la Katiba.

Wapinzani waliwabagua wajumbe wengine wa Bunge Maalum la Katiba kwa kuleta picha kwamba ni wao tu waliokwenda Dodoma kutafuta Katiba ya wananchi.

Ajabu ni kwamba wapinzani wametaja sababu nyingine ya wao kususia vikao vya bunge hilo kwamba wamekuwa wakibaguliwa wakati ni wao walioanzisha ubaguzi ndani ya bunge hilo.

Pili, kitendo cha wapinzani kuunda umoja wao katikati ya wajumbe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilichochea wajumbe wa chama hicho tawala kuungana katika mapambano ya kisiasa yaliyoanzishwa na UKAWA.

Tatu, wapinzani wanajiaminisha kwamba wao wako sahihi wakati wote na wanajua kila kitu. Kumbe ni Mungu tu aliye sahihi wakati wote na anayejua kila kitu.

Nne, wapinzani wanajiaminisha kwamba kila mtu anayetoa maoni tofauti na yao anatumiwa na CCM. Kwa mfano, wakati wasomi au maprofesa walipotoa kitabu chao kinachopendekeza muundo wa Serikali mbili kuendelea kutumika Tanzania wapinzani wamedai ni CCM iliyowatumia vibaya.

Tano, ni bahati mbaya kwamba baadhi ya wapinzani wanakubali kuburuzwa na msimamo wa watu wawili au watatu wanaojidai kuwa wanajua kila kitu. Hawa wanavuruga sana kambi ya upinzani. Hawatengenezi chochote.

Lakini wakati huo huo, hatuwezi kuficha ukweli kwamba Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji mstaafu Joseph Warioba, amechangia kwa kiasi kikubwa kuvurugika kwa Bunge Maalum la Katiba.

Kwa kuwa alikwishamaliza kazi ya kukusanya maoni ya wananchi hakuwa na sababu ya kwenda kulihutubia Bunge Maalum la Katiba. Hata kama alikuwa ametakiwa kufanya hivyo angekataa. Lakini akaenda bungeni kupigania Serikali tatu.

Hotuba ya mwenyekiti huyo ambayo ilishangiliwa sana na wapinzani iliwachochea kwa kiasi kikubwa kudai Serikali tatu.

Akaja Rais Kikwete ambaye pamoja na mambo mengine, alizungumzia athari za Serikali tatu. Wapinzani wakaona moja kwa moja kwamba Rais alikuwa kikwazo cha kupatikana kwa Serikali tatu. Ndipo katika kupigania maslahi yao wakaunda UKAWA.

Sasa wapinzani wamesusia Bunge Maalum la Katiba. Wametaja sababu mbalimbali za wao kususia bunge hilo. Lakini sababu ya kweli ni kwamba matumaini yao ya kupata Serikali tatu yamepotea kabisa. Kwa kuwa walikwenda bungeni kwa lengo moja tu la kupigania Serikali tatu.

Kuna habari kwamba wapinzani wanataka kuzunguka nchi nzima kuzungumzia Katiba. Kwa mambo mawaili, wasiruhusiwe kwenda kuwavuruga wananchi.

Kwanza, mazungumzo kuhusu Katiba yako kwenye Bunge Maalum la Katiba na wamesusia kwa hiari yao.

Pili, UKAWA ni chombo ambacho hakijasajiliwa. Itakuwa vibaya sana wapinzani wakienda kuwadanganya wananchi kwamba ni CCM iliyovuruga Bunge Maalum la Katiba wakati ni UKAWA iliyolivuruga.

Na kwa kweli hatua waliyochukua ya kususia vikao vya Bunge Maalum la Katiba vitasaidia sana kuleta umoja na utulivu ndani ya bunge hilo.

Kwa hivyo, kuna haja ya Watanzania kuelimishana na kuhamasishana kuchagua muundo wa Serikali mbili siyo kwa sababu ya kuiunga mkono CCM bali kwa sababu za kulinda maslahi ya Taifa.

Tazameni! Viongozi wa dini wanataka mfumo wa Serikali mbili uendelee. Hawa hawana maslahi yoyote ya kisiasa. Maslahi yao yako kwenye Taifa.

Tazameni! Wasomi wameandika kitabu kinachosisitiza mfumo wa Serikali mbili uendelee. Hawa hawana maslahi yoyote ya kisiasa. Maslahi yao yako kwenye Taifa.

Tazameni! Mwalimu Julius Nyerere aliona umuhimu wa kuwa na Serikali mbili. Ni kweli leo kuna watu katikati yetu na akili zao timamu wanaotaka tusimwendekeze Nyerere. Lakini matatizo mengi yanayoendelea kuikumba nchi yetu yanatokana na kumpuuza Nyerere.

Tazameni! Rais Kikwete hakuficha kitu alipolihutubia Bunge Maalum la Katiba. Alieleza waziwazi matatizo yanayoweza kutokea katikati ya Serikali tatu. Pale hakuzungumzia maslahi ya CCM. Alizungumzia maslahi ya Taifa.

Kwa mfano, kukiwa na Serikali ya Tanganyika wananchi wa Zanzibar wanaoishi na kufanya biashara zao Tanganyika watakuwa wageni. Ni wazi yatawapata matatizo.

Kwa bahati mbaya Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Seif Shariff Hamad, amewambia wananchi wa Pemba kwamba hata ukivunjika Muungano hawatapata matatizo kwa sababu walikuja Tanganyika kuwekeza kama walivyowekeza Wachina na Makaburu.

Kitu ambacho hajui ni kwamba wananchi wa Pemba hawakuja Tanganyika kuwekeza, bali walihamia baada ya Tanganyika na Zanzibar kuwa nchi moja.

Kwa hivyo, majina ya wananchi wa Pemba hayako kwenye Kituo cha Uwekezaji Tanzania

Lakini kuna jambo jingine. Tuone mbali. Tanganyika kukiwa na Serikali Kuu mbili, ya Tanganyika na ya Muungano, zinazoongozwa na vyama viwili tofauti amani itatoweka.

Hatuwezi kuwa na vyama viwili tawala katika nchi moja. Kutakuwa na migongano ya kutisha na nchi inaweza kutawaliwa na Jeshi.

Na hili si jambo la kujaribu. Ni ujinga kujaribu maafa. Tanganyika haitakalika kama, kwa mfano, Serikali moja itaongozwa na CCM na nyingine na Chadema. Tutapata shida!

Katika mazingira hayo basi, Serikali ya Muungano ambayo imelala iamke. Ianze kushughulikia mara moja kero za Muungano zinazochangia madai ya Serikali tatu.

Mwisho, kuna jambo kubwa ambalo wapinzani hawalijui, nalo ni hili: Walichofanya mbele ya Tume ya Warioba ni kutoa maoni tu ya Serikali tatu. Hayo yalikuwa maoni tu. Hawakutoa Katiba. Katiba ya wananchi itapatikana baada ya kura ya maoni.

Kwa hiyo, inashangaza kuona kwamba wamegeuza maoni yao kuwa shehemu ya Katiba! Hawataki yabadilishwe kwa madai kuwa ni maoni ya wananchi! Na wameunda umoja wa kupigania maoni yao yasibadilishwe!

Huo ni udikteta ambao umeendelea kuvuruga umoja ndani ya vyama vya upinzani. Na sasa unavuruga umoja wa Bunge Maalum la Katiba!

Katika hali hiyo hapana shaka kuna wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba wanajiuliza wamefuata nini Dodoma!

Watanzania wanahitaji muundo wa Serikali utakaoendeleza umoja wao, amani yao, na usalama wao. Na muundo huo si mwingine ila ni wa Serikali mbili.