*Yafikishia umeme Watanzania asilimia 18.4, mita 65,000 za Luku zaingia
SHIRIKA la Umeme nchini (TANESCO) limeanza kupiga hatua kutokana na juhudi linazofanya za kuwafikishia umeme Watanzania walio wengi.

Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Injinia William Mhando, aliliambia Jamhuri mwishoni mwa wiki kuwa idadi hiyo imetokana na kazi kubwa iliyofanywa na Watendaji wa TANESCO kwa kutumia fedha kidogo zilizopo.

Naibu Mkurugenzi Mtendaji (Usambazaji), Felchesmi Mramba, aliliambia Jamhuri kuwa kwa sasa shirika hilo litafanya kazi ambayo watu hawataamini.

“Lengo ni kuunganisha watanzania asilimia 30 ifikapo 2015, na sasa tumefikia asilimia 18.4. Haya mambo yanawezekana. Ukiangalia milioni 42 ya Watanzania tumefikia asilimia 18.4, si jambo dogo,” alisema Mramba.

Kati ya Watanzania milioni 42, Mramba alisema Watanzania wanaotumia umeme kwa sasa ni 7,728,000.

Mramba aliliambia Jamhuri kuwa kuanzia jana mita 65,000 za Luku zilikuwa zimeingia nchini na hivyo wateja ndani ya wiki hii wataunganishwa kwa kasi kubwa.

Awali, Injinia Mhando aliliambia Jamhuri kuwa mahitaji halisi ya TANESCO kutenda shughuli zake inavyostahili ni Sh trilioni 1.3, lakini kwa sasa wanapata kiasi kidogo.