Shirika la umeme Tanzania (TANESCO) limendelea na jitihada zake za uwajibikaji kwa jamii kwa kusadia uchimbaji wa Kisima Shule ya Msingi Nyani iliyoko Wilayani Kisarawe Mkoani Pwani.
Akizungumza Mkurungezi wa Fedha TANESCO Renata Ndege kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Maharage Chande amesema licha ya shughuli ya TANESCO kuwa ni huduma ya umeme, lakini wajibu wa kuisaidia jamii inayoihudumia limekuwa jambo la muhimu kwa Shirika.
“Tumekuja kukabidhi kisima cha maji chenye thamani ya shilingi milioni 14, ambacho kitawasadia wanafunzi na wanakijiji wa Nyani kuondokana na changamoto ya upatikanaji maji safi waliyokuwa wanakumbana nayo awali” amesema Ndege.
Ameongeza kuwa sambamba na kukabidhi kisima hicho wametekeleza zoezi la upandaji wa miti 100 katika eneo la Shule ya Msingi Nyani, ikiwa ni muendelezo wa mikakati ya Shirika katika kutunza mazingira.
“Sote tunafahamu umuhimu wa miti katika kuleta mvua ambazo kwa kiwango kikubwa huchangia uwepo wa maji katika mabwawa ya kuzalisha umeme, hivyo zoezi la leo lina uhusiano wa moja kwa moja na uwepo wa umeme wa uhakika nchini,” amefafanua Ndege.
Aidha, alisema kuwa matukio yote yanayofanyika ni muendelezo katika kuelekea maadhimisho ya siku ya wanawake duniani tarehe 8 Machi 2023.
“Ndio sababu leo tumekuja wanawake wa TANESCO, hususan wa Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani kutekeleza shughuli hizi,” ameongezea Ndege.
Akitoa shukrani, Diwani wa kata Mfizi Yadhamicas Nghondo ameishukuru TANESCO kwa ufadhili wa huduma hizo muhimu kwa jamii kwani changamoto ya maji katika Kijiji cha nyani imekuwa ya muda mrefu, hali iliyokuwa inawalazimu wanafunzi na wanakijiji kufuata maji mto Ruvu umbali wa zaidi ya kilomita 5.
“Ni kweli kwamba shughuli za TANESCO ni kusambaza umeme na kuangazia maisha ya watanzania, lakini wamekuja kutuangazia maisha yetu kwa kutulekea hizi huduma tunawashukuru sana,” alisema Diwani Nghondo.
Mwaka 2019 na wwaka 2020 TANESCO kupitia wafanyakazi wake wa Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani walijenga vyumba viwili vya madarasa, ofisi ya walimu na choo cha matundu 6. Jitihada hizo limesadia kuongeza ufaulu kwa wanafunzi wa shule hiyo hadi kufikia zaidi ya asilimia 80 mwaka 2022.
TANESCO imeahidi kuendelea kuboresha mazingira ya shule hiyo kwa kupaka rangi madarasa yaliyopo na kuboresha sakafu kwa madarasa yaliyochakaa.