Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limechachamaa na kuanzisha operesheni kabambe inayoambatana na kuwasweka lupango wateja wake wanaoiba umeme.

Operesheni kali iliyoanzia katika eneo la Kitunda Dar es Salaam, imefanikiwa kunasa wezi sugu wanne wa umeme ambao walikabidhiwa moja kwa moja Kituo Kikuu cha Polisi Jumamosi tayari kwa taratibu za kupelekwa mahakamani.

Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco (Usambazaji), Felchesmi Mramba, ameliambia Gazeti la JAMHURI mwishoni mwa wiki kuwa sasa wameamua kuwasha moto bila kusita.

“Leo (Jumamosi) tumekamata wateja wanne waliojiunganishia umeme huko Kitunda na tumewapeleka Central Police (makao makuu ya polisi Dar es Salaam). Tumeng’oa nguzo nne zilizounganishwa na vishoka, tumekata service line tano na kung’oa tatu zilizounganishwa kienyeji na tumeona ajabu kweli. Katika operesheni hii tumedisconnect (kata) AC (air conditioners) 20 waliojiunganishia umeme bila kupita kwenye mita,” Mramba aliiambia JAMHURI.

Alisema wateja hao (majina yanahifadhiwa) wengine ukionyeshwa kuwa wanaiba umeme, huwezi kuamini kwani ni watu wenye heshima kubwa katika jamii.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, aliiambia JAMHURI kuwa kilichofanywa na Tanesco huko Kitunda kitakuwa endelevu.

“Tunazo taarifa za siri zinazotufahamisha kila nyumba inayoiba umeme wetu. Sasa tumemaliza utafiti na tutakwenda nyumba hadi nyumba… tunamwambia mtu kiasi cha umeme alichoiba anatulipa na ikibidi tunampeleka polisi na hatimaye mahakamani.

“Wiki ijayo (kuanzia jana) tunakwenda Kariakoo. Huko tumepewa na michoro hadi ramani jinsi walivyojiunganishia nyaya, wanavyoiba umeme na hapa ndipo watakapotujua kuwa tuna akili kuliko wao,” aliseam Maswi.

Maswi alisema wateja wanapaswa kujua kuwa vya dezo vinaponza. “Walikuwa wanacheza na wengine, mimi nawahakikishia kuwa umeme wa wizi zamu hii utawatokea puani,” alisema Maswi.

Mpango huu ambao unatekelezwa nchi zima, unalenga kuzifikia hoteli kadhaa zinazoheshimika katika eneo la Kariakoo (majina yanahifadhiwa), zinazoiba umeme kwa ajili ya kupikia na matumizi mengine vyumbani mwa wateja.

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini wizi wa aina mbili. Wapo watu wanaoiba umeme kwa utaratibu wa kuunganisha nyaya nje ya mfumo halali wa Tanesco na wengine wanaotumia mbinu ya kuuziwa umeme wa bei chee kutoka kwa baadhi ya watumishi wasio waaminifu wa Tanesco.

“Ukienda kwenye mita ya mtu ndani ambaye si kiwanda ukakuta ana uniti hadi 900 kwenye mita wala usiulize. Hao wanauziwa na wafanyakazi wa Tanesco wanaotumia password kuupumbaza mfumo wa kompyuta kwa gharama ya Sh 15,000 au 20,000 na maisha yanakwenda. Matajiri wakubwa Mikocheni na Mbezi wanawasha AC nyumba nzima kwa Sh 5,000 kwa mwezi,” kilisema chanzo chetu.

Operesheni hii imeelezwa kuwa itakuwa ya kudumu na inaweza kuwaweka pabaya matajiri wengi wanaotanua kwa gharama ya kuibia wateja wanaolipa kihalali. Tanesco inasema baada ya majumbani watakwenda viwandani.