Na Cresensia Kapinga, JamhuriMedia, Mbinga
AFISA uhusiano wa huduma kwa wateja TANESCO Ruvuma, Allan Njiro, amewatahadharisha wananchi wa vitongoji vya Matemanga na Mkurusi vilivyopo katika kata ya Kigonsera Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga vijijini mkoani Ruvuma kuwa makini na watu ambao ni matapeli wanaopita kwenye nyumba zao kwa lengo la kuwaingizia umeme na kuwachaji hela nyingi kinyume na taratibu za shirika hilo.
Hayo ameyasema leo kwenye ziara yake ya kutoa Elimu, kusikiliza kero na kutatua changamoto mbalimbali zinazohusu umeme ambapo amewataka wananchi hao kuchukuwa tahadhari ya watu matapeli ambao wanapita kwenye nyumba zao na kuwatajia gharama za kuwaingizia umeme wakati serikali inagharamia na wao wanatakiwa kulipia kiasi cha sh. 27,000 tu na si vinginevyo.
“Niwaombe wananchi kuwa makini na mtu atakaye kuja akitaka pesa kiasi cha sh. 100,000 au 50,000 ili akuingizie umeme huyo ni mwizi hivyo unatakiwa kutoa taarifa kwa Mtendaji wa Serikali ya Kijiji ili aweze kuchukuliwa hatua za kisheria haraka iwezekanavyo” alisema Njiro.
Hata hivyo amewaeleza wananchi kuwa serikali iimeleta mradi wa Ujazilizi mradi ambao baadhi ya vijiji vinakuwa na umeme lakini kuna maeneo hayaafikiwa na huduma hiyo hivyo wanahakikisha wanapatiwa umeme.
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Kigonsera Simon Komba amewataka wananchi wa vitongoji hivyo kutoa ushirikiano kwa shirika la umeme Tanzania (Tanesco) kipindi mradi huo wa umeme utakapoanza ili waweze kumaliza kwa wakati.