Hakika kuamini ni kuona. Sikupata kuamini uwepo wa tandala wakubwa hapa Tanzania hadi siku nilipozuru Hifadhi ya Taifa ya Ruaha (RUNAPA) na kujionea aina hiyo ya wanyamapori.
RUNAPA ndiyo mahali pekee katika Tanzania yanapopatikana makundi ya tandala wakubwa, ambao ni kivutio cha aina yake. Watu wengi kutoka ndani na nje ya Tanzania huzuru hifadhi hii kila siku kwa nia ya kujionea wanyamapori hawa wenye historia ya kipekee.
Juni 13, mwaka huu, itabaki kuwa siku ya kipekee katika historia ya maisha yangu, na pengine kwa wengine wengi tuliofuatana nao katika safari yetu ya RUNAPA. Ilikuwa ni ziara maalum kwa wahariri wa habari kutoka vyombo mbalimbali hapa nchini.
Ni saa tatu asubuhi tunawasili lango kuu la RUNAPA. Tunapokewa na watumishi kadhaa (wahifadhi). Baadhi yetu tunasogea hapa na pale kuangalia mandhari nzuri ya eneo hili. Wengi tunavutiwa zaidi na sampuli ya mafuvu ya vichwa na pembe za tandala wakubwa, yanayohifadhiwa mbele ya lango hili.
Mara tunaombwa kukusanyika pamoja kusikiliza maelekezo kutoka kwa mmoja wa wenyeji wetu. Huyu anajitambulisha kuwa ni Mhifadhi Ikolojia wa RUNAPA, Paul Ranga.
“Ndugu wageni wetu, wahariri na waandishi wa habari, karibuni sana katika Hifadhi hii ya Ruaha,” anasema Ranga na kuendelea:
“Tuna utaratibu wa kuwaelekeza wageni wetu mambo ya kuzingatia wawapo ndani ya hifadhi kwa lengo la kulinda uhifadhi.
“Mnapokuwa ndani ya hifadhi, mtu yeyote haruhusiwi kuvuta sigara na kutupa mabaki yake chini. Tunazuia hilo kuepusha hatari ya kuanzisha moto hifadhini.”
Anatutahadharisha kuzingatia pia masharti ya kutoingia na silaha yoyote, kutotupa takataka na kutopiga kelele tuwaonapo wanyama hifadhini.
“Tunazuia kelele ili kudumisha mazingira tulivu kwa wanyama na kuepusha bughudha kwa watalii wengine hifadhini,” anafafanua.
Mhifadhi Ikolojia huyu pia anawaelekeza madereva wa magari tunayotumia kuzingatia sharti la kuendesha kwa mwendo usiozidi kilomita 50 kwa saa hifadhini.
Wakati huo huo, wenyeji wetu wanatupatia ukarimu wa kutugawia vijitabu vyenye wasifu wa RUNAPA. Mara safari ya kuelekea katikati ya hifadhi inaanza. Yapata saa 3:37 hivi asubuhi.
Kuanzia hapa wengi tunaonekana kutabasamu na kuchangamka zaidi, huku tukiangalia huku na kule kwa shauku ya kuona wanyamapori ‘wanaoibeba’ RUNAPA, yaani tandala wakubwa.
Kwa bahati nzuri, mnyama wa kwanza tuliyeanzia kumwona ni tandala mkubwa, kwa mujibu wa mmoja wa wenyeji wetu. Tunamshuhudia mnyama huyu dume akiwa amesimama kwa mshangao kidogo kandokando ya barabara akitazama magari tunayosafiria.
Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa wengi wetu kumwona ‘live’ tandala mkubwa. Tunamchunguza na kubaini kuwa anakaribia kufanana na mbuzi. Ukubwa wa umbo, masikio na pembe zake ndefu zilizojisokota ndivyo vinavyomtofautisha na mbuzi. Lakini pia ni mzuri wa kuvutia macho ya kila mtu, hasa kutokana na muundo wa kipekee wa pembe zake.
Sote tunaendelea kujikita katika kuwaangalia tandala wakubwa wengine kwenye maeneo tofauti hifadhini. Tunagundua pia kwamba tandala jike hana pembe kama ilivyo kwa tandala dume.
Hatujali sana kuangalia makundi ya wanyamapori wengine kama vile tembo, kiboko, simba, twiga, swala, mbuzi na ndege wakiwamo kanga kwani hao tumekuwa tukiwaona katika hifadhi nyingine.
Ziara yetu inazidi kunoga baada ya kupata kifungua kinywa katika moja ya majengo ya RUNAPA. Kutoka hapo tunapokewa upya na waongoza wageni hifadhini.
Sekunde chache baada ya gari letu kuondoka ili kutupeleka maeneo zaidi ya utalii ndani ya RUNAPA, anasimama kijana tusiyemfahamu. Anajitambulisha kwetu kwa jina la Suwedy Halfan, na kwamba ni mwongoza wageni katika hifadhi hii.
Anatuongoza katika maeneo mbalimbali. Anatuonesha vivutio tofauti vya utalii ukiwamo Mto Ruaha ambao maji yake hutegemewa sana na wanyamapori hapa RUNAPA.
Mhariri wa Habari Msaidizi wa Gazeti la HABARILEO, Stella Nyemenohi, na Mhariri wa Gazeti la The African, Shermarx Ngahemera, wanaeleza kuvutiwa pia na mto huu.
“Pamoja na kivutio cha tandala wakubwa, na huu Mto Ruaha nauona ni unique (wa kipekee/usio na kifani), unaongeza mvuto katika hifadhi hii,” anasema Nyemenohi.
Baadaye ninapata nafasi ya kufanya mahojiano maalum na Halfan. Lengo ni kujua upekee wa tandala mkubwa, na kwanini anapatikana kwa wingi zaidi katika hifadhi hii, na si pengine popote hapa Tanzania.
“Hawa wanyama [tandala wakubwa] wanapatikana kwa wingi hapa RUNAPA kwa sababu ya mazingira yanayohimili maisha yao,” anasema Halfan na kuongeza:
“Kikubwa zaidi, hapa hifadhini kuna mti unaofahamika kwa Kihehe kama Mohadada, ambao majani yake ndiyo chakula kikuu cha tandala wakubwa.
“Mti huu ni sumu, mtu yeyote akila majani yake, au mizizi yake atawashwa na kuharisha sana. Lakini sumu hiyo inawatibu tandala wakubwa na kuwakinga dhidi ya magonjwa mbalimbali.”
Kihistoria, inasadikika kuwa babu zetu walitumia mti huo kuchanganya na maji kwa ajili ya kudhuru maadui zao wakati wa ukoloni.
Kwa mujibu wa Halfan, tandala wakubwa wanapendelea kuishi na kutafuta chakula katika maeneo ya misitu na ya wazi. Wana kawaida ya kulala usiku.
“Umri wa mimba kwa tandala mkubwa ni miezi tisa, na kwa kawaida huzaa ndama mmoja. Ni mara chache sana kukuta amezaa pacha,” anasema Halfan.
Adui mkubwa wa tandala wakubwa, kwa mujibu wa mwongoza wageni huyu, ni simba. “Simba wanawawinda sana wanyama hawa,” anasisitiza.
Sifa nyingine ya pekee ni kwamba eneo hili la hifadhi lilikuwa mapito muhimu ya Chifu Mkwawa wa Wahehe – Iringa, na Chifu Mapesa wa Wagogo – Dodoma.
“Chifu Mkwawa na Chifu Mapesa walipendelea kupita hapa kwenda majumbani kwao,” anaongeza.
RUNAPA inaundwa na eneo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 20,300. Ndiyo hifadhi yenye eneo kubwa zaidi Tanzania. Eneo lake linahusisha mikoa ya Iringa, Dodoma na Mbeya.
Watu wengi wanahamasika kuzuru hifadhi hii kwa nia kuu ya kujionea tandala wakubwa. Kuamini ni kuona.