*Makusanyo yagonga Sh bilioni 411 kwa miezi 7
*Wizara yaipa mwelekeo ikusanye Sh trilioni 1
*Sinema ya The Royal Tour yatajwa kuwa chachu
Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) limeendelea kuvunja rekodi ya wageni na mapato, na tayari hadi Machi ya mwaka huu wa fedha limeingiza Sh bilioni 411.3.
Kiasi hiki cha mapato ni kikubwa kuliko kile kilichokusanywa na shirika hili kwa mwaka mzima wa fedha wa 2023/2024 ambacho kilikuwa Sh bilioni 410.9.
Hii ina maana kwamba miezi iliyosalia katika mwaka huu wa fedha wa 2024/2025 ya Machi, Aprili, Mei hadi Juni 30, huenda zikakusanywa fedha nyingine nyingi na hivyo kuvunja rekodi ya shirika ya miaka 61 ya kuanzishwa kwake.
Ingawa TANAPA hawataki kuweka bayana kuhusu mafanikio haya, taarifa za siri kutoka ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii zinaonyesha kuwa viongozi wakuu wa wizara wameipongeza TANAPA kwa uvunjaji huo wa rekodi, na kutaka waendelee kuhakikisha mapato yanaongezeka.
“Tunajua TANAPA wanafanya vizuri sana kwenye mapato, hili linatusaidia kwenye utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020-2025 iliyotutaka kama wizara tuhakikishe watalii na mapato vinaongezeka.
“TANAPA kwa miezi hii pekee wamevunja rekodi ya mwaka mzima. Bado wana miezi minne. Tumewapa lengo wafikie mapato ya trilioni moja…huo ndiyo mwelekeo wetu kuanzia mwaka 2026,” kimesema chanzo chetu ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii.
Kamishna wa Uhifadhi (CC) wa TANAPA, Juma Kuji, ameulizwa kuhusu mafanikio hayo, lakini amekataa kuyaeleza kwa undani.
“Sisi kazi yetu ni kutekeleza malengo tuliyopewa na serikali, kama unataka kujua mafanikio ya sekta yote ya maliasili na utalii uliza wakubwa wetu wizarani, jambo moja tu nikueleze- maelezo ya serikali kwa mujibu wa ilani ya uchaguzi tunayatekeleza kadri ya uwezo wetu,” anasema CC Kuji.

Habari kutoka wizarani zinaonyesha kuwa kuanzia Julai 1, 2024 hadi Aprili 28, mwaka huu idadi ya wageni wa nje ilikuwa 864,000 na mapato yalikuwa Sh bilioni 405.4 Idadi ya wageni wa ndani hadi Machi 6, mwaka huu iliingiza mapato ya Sh bilioni 5.6.
Kwa kipindi kama hiki mwaka 2023/2024 idadi ya wageni wa nje ilikuwa 773,389 waliokaa hifadhini, pia wageni wa ndani ilikuwa 231,026. Mapato yalikuwa Sh bilioni 332.857
“Utalii unazidi kuimarika kwani idadi ya wageni wa nje imeongezeka kwa idadi ya wageni 104,273 (13.5%), aidha idadi ya wageni wa ndani imeongezeka kwa idadi ya wageni 79,859 (34.6%) na mapato yameongezeka kwa Sh bilioni 78.416 sawa na asilimia 23.55,” inasema taarifa ya Wizara ya Maliasili na Utalii.
Hifadhi ya Serengeti inaendelea kuongoza kwa idadi ya wageni na mapato, ikiwa imetembelewa na wageni 387,000 na kuingiza mapato ya Sh bilioni 216. 7. Kiasi hiki ni asilimia 32.52 kwa upande wa wageni na asilimia 52.6 kwa upande wa mapato yote ya Shirika kwa kipindi cha Julai 2024 hadi Machi, mwaka huu.
Hifadhi zinazofuata kwa mapato ni Kilimanjaro (Sh bilioni 90.3), Tarangire (Sh bilioni 48.37), Manyara (Sh bilioni 17.23), Nyerere (11.6), Arusha (Sh bilioni 8.7), MIkumi (Sh bilioni 7.5), Ruaha (Sh bilioni 4.2), Saadani (Sh bilioni 2), Mkomazi (Sh bilioni 1.079), Gombe (Sh milioni 773), na Mahale (Sh milioni 700)
Katika mwaka wa fedha wa 2023/2024 TANAPA pia ilifanya vizuri katika ukusanyaji mapato. Kwa kipindi cha kuanzia Julai 1, 2023 hadi Juni 30, 2024 ilikusanya Sh 410,902,998,132.31, ikiwa ni zaidi ya Sh 28,595,020,635.24 kuliko lengo la awali la Sh 382,307,977,497.07.
Ongezeko hilo lilitokana na juhudi mbalimbali za kuboresha miundombinu ya utalii, kuimarisha huduma kwa watalii, na shughuli za utangazaji zilizofanywa na TANAPA.

Katika kipindi cha Julai 2023 hadi Machi 19, 2024, watalii 1,514,726 walitembelea Hifadhi za Taifa, ambako watalii wa ndani walikuwa 721,543 na wa nje 793,183. Hilo lilikuwa ni ongezeko la asilimia 5 ikilinganishwa na lengo la awali la kupokea watalii 1,387,987 katika kipindi hicho.
Mafanikio ya utalii nchini Tanzania, hasa kwa TANAPA na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa jumla, hayawezi kutenganishwa na sinema ya The Royal Tour ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Sinema hii imekuwa na umuhimu mkubwa katika kukuza na kuhamasisha sekta ya utalii, na imechochea mafanikio makubwa kwa TANAPA na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa jumla.
Sinema ya The Royal Tour imeleta umaarufu mkubwa kwa Tanzania duniani. Rais Samia ameonyesha vivutio vya kipekee vya utalii nchini kupitia maeneo maarufu kama Serengeti, Ngorongoro, na Mlima Kilimanjaro. Hii imeendelea kuvutia watalii kutoka sehemu mbalimbali duniani, na kuchangia ongezeko la idadi ya watalii wanaotembelea Hifadhi za Taifa. Matokeo yake, TANAPA imeona ongezeko la mapato kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watalii wa kigeni.
Kwa Rais Samia kuwa mtangazaji mkuu wa vivutio vya utalii vya Tanzania, The Royal Tour imechochea hamasa kubwa kwa Watanzania wenyewe kuzuru vivutio vyao vya utalii. Vilevile, sinema hii imesaidia kuvutia watalii kutoka nchi mbalimbali, hasa kutoka kwa wale ambao walikuwa hawajui vivutio vya Tanzania. Ongezeko la watalii, hasa katika hifadhi za TANAPA, ni moja ya mafanikio yaliyotokana moja kwa moja na The Royal Tour.
Kwa kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea hifadhi za taifa, The Royal Tour imechangia moja kwa moja katika ongezeko la mapato kwa TANAPA. Hii ni kutokana na ongezeko la kiingilio cha watalii na shughuli za ziada zinazohusiana na utalii, kama vile malazi, usafiri, na huduma.
Sinema ya The Royal Tour imefungua milango ya uwekezaji na ushirikiano katika sekta ya utalii, kwani imevutia wawekezaji kutoka sehemu mbalimbali duniani. Kwa kuwa Tanzania imeonekana kama sehemu salama na yenye vivutio vya kipekee, wawekezaji wameonyesha nia ya kuwekeza katika hoteli, miundombinu, na huduma za ziada; jambo ambalo limeimarisha sekta ya utalii na kuzalisha ajira kwa Watanzania.
Kwa kuwa TANAPA inasimamia hifadhi za taifa, ongezeko la utalii lililochochewa na The Royal Tour limesaidia kuhifadhi na kutunza maeneo haya kwa njia endelevu. Watalii wengi wamevutiwa na mazingira ya asili ya Tanzania, na hivyo kuweka mkazo zaidi kwenye juhudi za kulinda rasilimali hizi za asili ili ziendelee kuwa na manufaa kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Sinema ya The Royal Tour imesaidia kuendeleza kampeni za kimataifa za utalii zinazoratibiwa na Wizara ya Maliasili na Utalii. Kwa kuwa imeonyesha Tanzania kwa jicho la kipekee na la kuvutia, imehamasisha mashirika ya utalii na waandishi wa habari kuandika na kutangaza zaidi kuhusu vivutio vya utalii vya Tanzania. Hii imeongeza idadi ya watalii wanaotembelea Tanzania, huku pia ikitangaza Tanzania kama moja ya maeneo bora ya utalii duniani.
Mafanikio ya utalii nchini Tanzania, kama vile ongezeko la mapato kwa TANAPA, ongezeko la watalii, na ukuaji wa uchumi, yamejengwa kwa nguvu na mafanikio ya The Royal Tour ya Rais Samia. Sinema hii ilileta mabadiliko makubwa katika mtazamo wa dunia kuhusu vivutio vya Tanzania na imechangia kwa kiasi kikubwa katika kukuza utalii wa ndani na nje, na pia kusaidia kukuza hifadhi za taifa na mazingira ya kibiashara kwa wafanyabiashara wa utalii.