Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Serikali kupitia Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa) limesema kwa mwaka huu wa fedha 2023/2024 katika kipindi cha Julai 2023 hadi Machi 19, 2024 idadi ya watalii imeongezeka na kufikia 1,514,726.
Aidha limesema katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wake Dk. Samia Suluhu Hassan, kumekuwepo na ongezeko la mapato kutoka shilingi 174,715,158,494 (2021/2022) hadi kufikia shilingi 337,424,076,896 (2022/2023) sawa na ongezeko la shilingi 162,708,918,402 ambayo ni asilimia 94.
Hayo yamebainishwa na leo Machi 21, 2024 jijini Dar es Salaam na Kamishna wa Uhifadhi Tanapa (CC), Juma Kuji kwenye kikao kazi baina ya Tanapa na Wahariri wa vyombo vya habari chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina ili kueleza mafanikio ya utekelezaji wa shughuli za Shirika hilo katika kipindi cha miaka mitatu ya serikali ya awamu ya sita.
Amesema watalii katika kipindi hicho cha Julai 2023 hadi Machi 2024 watalii wa ndani walikuwa 721,543 na wa nje wakiwa 793,183 wametembelea Hifadhi za Taifa sawa na ongezeko la asilimia 5 ikiwa ni zaidi ya lengo la kupokea watalii 1,387,987 katika kipindi husika.
“Idadi ya watalii wanaotarajiwa kutembelea Hifadhi za Taifa kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ni 1,830,081 (watalii wa nje 963,413 na watalii wa ndani 866,667). Vilevile, katika kipindi cha miaka mitatu kumekuwepo na ongezeko la siku za kukaa wageni kutoka wastani wa siku 1,749,194 katika mwaka wa fedha 2021/2022 hadi kufikia wastani wa siku 2,669,586 kufikia Februari 2024.
“Ongezeko hili limechangia ongezeko la mapato ambapo katika kipindi cha miaka mitatu, kumekuwepo na ongezeko la mapato kutoka shilingi 174,715,158,494 (2021/2022) hadi kufikia shilingi 337,424,076,896 (2022/2023) sawa na ongezeko la shilingi 162,708,918,402 ambayo ni asilimia 94,” amesema.
Aidha, amesema kwa mwaka wa fedha 2023/2024 (Julai 2023 hadi Machi 19, 2024) Shirika limekusanya shilingi 340,101,108,465 ukilinganisha na matarajio ya kukusanya shilingi 295,466,811,506 mpaka Machi 2024. Kiasi hiki (Bilioni 340) ni ongezeko la shilingi 44,634,296,959 ambayo ni sawa na asilimia 15.
“Shirika lina matarajio ya kukusanya kiasi cha shilingi 382,307,977,497 hadi Juni 2024. Mapato haya ya sasa yanazidi mapato ya shilingi 282,450,446,103 yaliyokusanywa mwaka 2018/2019 kabla ya janga la UVIKO – 19 ambayo yalikuwa ndio kiwango cha juu cha mapato katika Shirika.
“Ongezeko hili la watalii na mapato linaenda sambamba na malengo ya Ilani ya Chama Chama cha Mapinduzi 2020 – 2025 inayoelekeza idadi ya watalii nchini,” amesema.
Vilevile amesema jumla ya vikundi 138 vimewezeshwa miradi mbalimbali ya uzalishaji mali ikiwemo ufugaji wa nyuki, uchakataji wa viungo vya chakula na ufugaji. Jumla ya shilingi billion 2.4 zilitumika kuwezesha miradi ya uzalishaji mali.
“Pia, Benki za Kijamii za Uhifadhi “Community Conservation Bank” (COCOBA) 159 zilianzishwa kupitia mradi wa REGROW na kupewa fedha mbegu kiasi cha shilingi 1,453,272,934. Miradi hii imesaidia kuongeza wastani wa pato la wananchi katika maeneo husika na kupunguza utegemezi wa Maliasili,” amesema na kuongeza:
“Jumla ya wanafunzi 1,051 kutoka vijiji 60 vinavyotekeleza mradi wa REGROW wamepatiwa ufadhili wa masomo wenye thamani ya shilingi 4,273,315,700 katika vyuo mbalimbali vya kitaaluma hapa nchini. Ufadhili huu utasaidia kuongeza kiwango cha uelewa kwenye jamii na kuongeza uwezo wa uzalishaji mali kwenye jamii husika,”.