*Awataka wananchi kutumia fursa za kiuchumi zinazotokana na Utalii katika hifadhi hiyo.

*Aiagiza Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kuimarisha Mawasiliano.

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ameiagiza Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) kuanzisha programu za kutangaza vivutio vilivyopo katika Tifadhi ya Taifa ya Mkomazi ili kuongeza idadi ya watalii wanaoingia katika hifadhi hiyo.

Amesema Serikali imefanya uwekezaji mkubwa ikiwemo ujenzi wa barabara, lango la watalii na huduma nyingine za kijamii ndani ya hifadhi hiyo hivyo ni lazima sasa Mamlaka hiyo itumie fursa hiyo kuongeza idadi ya watalii.

Ametoa maagizo hayo leo (Jumanne Machi 25, 2025) alipokuwa akizungumza na wahifadhi na wananchi baada ya kuzindua lango la kuingia na kutoka watalii la Ndea kwenye Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi lililoko Wilaya ya Mwanga Mkoani Kilimanjaro.

“Tutangaze mbuga yetu ya Mkomazi na vivutio vyake, wanyama ambao hawapatikani maeneo mengine watamkwe sana kwamba wanapatikana hapa, elezeeni umbali wa kutoka Moshi na Tanga mjini hadi hapa hifadhini.”

Amesema ujenzi wa lango hilo ni sehemu ya maboresho makubwa yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita katika kuchochea na kuongeza vivutio vya utalii nchini.

Aidha, ameiagiza TANAPA kutoa elimu kwa wananchi kuhusu fursa zinazopatikana kutokana na uwepo wa watalii ikiwemo vitu vinavyopendwa na watalii ili waweze kunufaika huku akiwataka wanananchi kuchangamkia fursa hizo.

Katika hatua nyingine Mheshimiwa Majaliwa amemuagiza Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Jerry Silaa kuweka mkakati wa kuimarisha mawasiliano katika njia na maeneo yaliyoko ndani ya hifadhi hiyo.

“Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari nayo ihakikishe kunakuwa na mawasiliano ya uhakika katika maeneo ya mbuga hiyo.”

Akitoa taarifa juu ya manufaa ya lango hilo Mhifadhi Mkuu Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi Emmanuel Mwailama amesema ujenzi wa lango hilo utaongeza idadi ya watalii katika mbuga hiyo ambao wengi wanakwenda kuona maisha ya jamii ya ziwa jipe, Faru weusi pamoja na Tembo.

Amesema pia lango hilo litachochoe fursa za kiuchumi kwa wananchi wanaozunguka eneo hilo la hifadhi kutokana ongezeko la watalii watakaopita njia hiyo ikiwa ni pamoja na kutengeneza ajira kwa wakazi wa vijiji vya eneo hilo.

Ujenzi wa lango hilo limegharimu Shilingi Milioni 350 na lina ofisi za idara nyingine za serikali kama Uhamiaji, Mamlaka ya mapato na benki.