Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Bi. Eda Sanga na mgeni rasmi katika sherehe za Mahafali ya nane ya Darasa la Saba ya Shule ya Msingi St. Aloysius ya Mbezi Beach jijini Dar es Salaam akihutubia wanamahafali na wageni waalikwa.

Mwenyekiti wa Kamati ya Shule ya Msingi St. Aloysius, Kenneth Sinare (katikati) akimpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Bi. Eda Sanga (kulia) mara baada ya hotuba yake.

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Bi. Eda Sanga (kulia) akimkabidhi cheti na zawadi mmoja wa wahitimu wa darasa la saba katika shule ya Msingi St. Aloysius  iliyopo Mbezi Beach Dar es Salaam katika sherehe za Mahafali ya nane.

Wanafunzi wa darasa la awali wa Shule ya Msingi St. Aloysius wakitoa burudani kwenye sherehe za Mahafali ya nane ya Darasa la Saba ya shule hiyo iliyopo Mbezi Beach Dar es Salaam.

VIONGOZI wa shule mbalimbali nchini Tanzania wameshauriwa kuhakikisha wanazifanya shule zao kuwa na mazingira salama, yenye utangamano, ushirikiano, upendo pamoja na furaha kwa wanafunzi ili yaweze kumjenga mtoto vyema kielimu na maadili katika jamii.

Ushauri huo umetolewa jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Bi. Eda Sanga alipokuwa mgeni rasmi katika sherehe za Mahafali ya nane ya Darasa la Saba ya Shule ya Msingi St. Aloysius ya Mbezi Beach jijini Dar es Salaam.

Alisema shuleni, watoto wanapaswa kupewe ushauri  na nasaha kadri inavyohitajika, huku wakiwa huru kutoa dukuduku zao na matatizo yao kwa walimu na kuyatatua kadri ya uwezo wao.

“Kuna kila sababu watoto kupewa ujuzi wa kutumia uwezo na mikono yao kufanya kazi na ujuzi wa kutumia akili zao za sasa kutatua migogoro yao kwa ngazi yao,” alisema Bi. Sanga katika hotuba yake.

Aliwataka walimu mbali na kumjenga mwanafunzi kielimu kuna haja ya kuwaandaa pia kuwa wazalendo wa taifa lao na kikazi kinachojali wasionacho kama tunavyowajali watu walionacho.

“Shule inatazamwa kama familia nje ya familia maana watoto wanatumia muda mwingi kuwa shuleni zaidi ya ule wawapo na familia zao nyumbani. Hofu ya Mungu ndiyo msingi wa mafanikio katika jambo lolote kwani inamjengea mtoto ujasiri, nidhamu na uthubutu, naomba haya tuyazingatie pia.

Aidha aliongeza kuwa kwa kutambua umuhimu wa elimu, TAMWA katika mpango mkakati wake wa miaka mitano 2016 hadi 202,  lengo namba tatu limehimiza kushughulikia masuala ya elimu kwa watoto wa kike, unyanyasaji wa kijinsia, ukatili kwa watoto na ndoa za utotoni.

Pamoja na hayo, aliwataka wazazi na walezi kutambua kuwa; mtoto umleavyo ndivyo akuavyo, hivyo kumjengea malezi mema mtoto ni kumjengea mazingira bora yenye maadili na usikivu katika jamii.

“Wazazi na walezi ambao mmeichagua shule hii kwa vyovyote mlitamani watoto wenu wawe wazalendo, wapenda nchi, na wapate elimu bora ujuzi na maarifa yanayofaa katika kuelekea kutimiza malengo ya mtoto aliyojiwekea (ndoto zake).”

Aliwataka wazazi kuwasaidia watoto wao kujitathmini na malengo yao hapo baadaye ili waweze kuyatimiza katika maisha yao. Ufuatiliaji wa mwenendo na masomo ya mtoto, kuwapa ushauri, upendo usaidizi pamoja na kuwa karibu zaidi na mtoto ili akiwa na tatizo lolote aweze kuwa huru kujieleza.

Alisema TAMWA imekuwa ikishauri siku zote kwamba ni vyema mzazi au mlezi akawa rafiki wa mwanaye ili kujenga ukaribu na upendo wa dhati kwao.

Kwa upande mwingine aliwataka wahitimu hao kuanza kuwa wazalendo na kujitolea kwa jamii ili kuwa mfano kwa wengine na pia kujenga upendo, huku wakitafsiri elimu waliyoipata katika hali halisi ndani ya jamii.