Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inatarajia kutoa tuzo za wanahabari zinazofahamika kama ‘Samia Kalamu Award’ zinazolenga kuhamasisha uandishi wa habari za maendeleo unaojikita katika kufanya uchambuzi wa utafiti wa kina, kuongeza maudhui ya ndani, kuzingatia weledi, maadili, uwajibikaji wa kitaaluma pamoja na kukuza uzalendo na kujenga taswira chanya ya nchi.
Katika hafla hiyo ya utoaji tuzo inatarajia kufanyika jijini Dodoma Aprili 29, 2025 katika Ukumbi wa Mabele, Mabeyo Complex, huku mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 15, 2025 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Dkt. Rose Reuben, amesema kuwa Samia Kalamu Awards ni matokeo ya mafunzo yaliyotolewa kwa wanahabari mwaka 2024, kwa lengo la kukuza na kuendeleza uandishi wa habari za maendeleo nchini.

Dkt. Reuben amesema kuwa lengo la tuzo hizo ni kuhamasisha na kuthamini kazi za waandishi wa habari wanaojikita katika uandishi unaoleta uelewa, hamasa na mabadiliko chanya katika jamii.
“Tunataka kuona habari zinazoibua changamoto lakini pia zikitafuta suluhisho, hii ni njia mojawapo ya kuonyesha kuwa uandishi wa habari wana nafasi muhimu katika maendeleo ya Taifa letu,” amesema Dkt. Reuben.
Amesema kuwa tuzo hizo zimegawanywa katika makundi makuu matatu ikiwemo kundi la kwanza linahusisha tuzo za umahiri wa kitaifa pamoja na tuzo maalum kwa waandishi wanawake, maafisa habari wa serikali na wachapishaji wa mitandaoni.
Kundi lengine linajumuisha vyombo vya habari ikiwemo redio, televisheni, magazeti na mitandao ya kijamii, huku kundi la tatu ni tuzo za kisekta zinazohusu maeneo kama afya, maji, elimu, kilimo, mazingira, TEHAMA, uchumi wa buluu, vijana, sanaa, michezo, utalii pamoja na uwekezaji.

Katika hafla ya utoaji wa tuzo Mhe. Rais Dkt. Samia anatarajiwa kutoa zawadi kwa washindi kama ishara ya kutambua mchango mkubwa wa vyombo vya habari katika ustawi wa Taifa.
TAMWA na TCRA wamewataka waandishi wa habari nchini kushiriki kikamilifu katika tukio hilo, huku wakisisitiza kuwa tuzo hizo ni sehemu ya jukwaa muhimu la kutangaza mchango wao katika maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.
Tuzo hizo zinatolewa kwa mara ya kwanza na TAMWA kwa kushirikiana na TCRA ambapo katika hafla hiyo itarushwa mubashara kupitia vituo vya televisheni, redio pamoja na mitandao ya kijamii, ili kuwapa wananchi nafasi ya kushuhudia mchango wa wanahabari waliobobea katika kuelimisha na kuleta mabadiliko.