Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma
Wizara ya Afya imeitaka Bohari ya Dawa (MSD) kutambua nafasi yake katika matumizi ya bima ya afya kwa wote na kuzingatia upatikanaji wa bidhaa za afya, ubora na bei zilizo katika muongozo wa matibabu wa Serikali.
Pia , amezitaka taasisi za afya kuangalia upya mifumo ya utoaji huduma lengo ni kuona namna gani inavyoweza kubadilika ili kukidhi mahitaji ya bima ya afya kwa wote.
Maagizo hayo yalitolewa jana jijini Dodoma na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dk.Grace Magembe wakati akifungua kikao cha MSD na wateja wake wakubwa.
Katika kikao kazi hicho Dk.Grace amesisitiza MSD kuhudumia wananchi kutokana na mahitaji na taasisi zote za afya kuangalia mifumo ya utoaji huduma inavyoweza kubadilika kukidhi mahitaji ya bima ya afya kwa wote.
“Tuangalie upya mifumo yetu ya utoaji huduma namna inavyoweza kubadilika ili kukidhi mahitaji ya bima ya afya kwa wote.Tusisumbue wananchi muwasiliane wenyewe wao wanataka huduma,”amesema
Kwa mujibu wa Dk.Grace amefafanua kuwa muswada wa bima ya afya umepitishwa kinachoendelea sasa ni kufanyia kazi kanuni kwa kushirikiana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Fedha, Ikulu na wadau wengine.
Kwa upande wake Mfamasia Mkuu wa Serikali Daud Msasi amesema, kikao hicho kitajadili changamoto na kutafuta suluhuhisho ili MSD aweze kuwahudumia wateja wakubwa kwa bidhaa wanazozihitaji.
“Tumeshiriki kikao cha MSD ambacho kinaunganisha wateja wake wakubwa kutoka katika hospitali kubwa lengo ni kuboresha huduma za kuwahudumia na kupata bidhaa wanazohitaji kwa ajili ya kutoa huduma.
Aliongeza kuwa :”Changamoto ambayo ipo inatokana na utendaji ni kwamba wateja hawa wanapokosa bidhaa MSD huagiza bidhaa zao nje ya nchi ambapo ni kinyume na sheria .
Naye Mkurugenzi Mkuu wa MSD Mavere Tukai amesema, lengo la kuwakutanisha wateja wakubwa ni kwa sababu mahitaji yao ya dawa ni makubwa tofauti na hospitali nyingine.
Ametaja wateja ambao wamekutana nao kuwa ni Hospitali ya Kibong’oto, Muhimbili, Ocean road, Benjamini Mkapa na Hospitali ya Mirembe.
“MSD tuna mkakati wa kuwa na wateja wakubwa ambao sio mpya lakini tumeamua kuweka katika uhusiano wa kibiashara.Tunachokifanya hapa leo kuangalia wapi tulipo sasa kuja na malengo ya pamoja ili kutengeneza mpango mkakati namna tunavyoweza kuyafikia malengo hayo.
Ameongeza kuwa “Tunakaa leo na kutengeneza mkakati wa pamoja na kuanza utekelezaji wake.Lengo tutembee pamoja katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF), Benard Konga , amesema, Rais Dk.Samia Suluhu Hassan amesaini Sheria ya Bima ya Afya kwa wote na utekelezaji wake unaanza hivi karibuni.
“Leo tumeshiriki katika kikao kilichoandaliwa na MSD ambapo unalengo la kutafuta suruhu ya pamoja kuhusu suala zima la upatikanaji wa dawa nchini.
Ameongeza kuwa :“Ili kutimiza adhma ya Serikali ya Awamu ya Sita ya bima ya afya kwa wote lazima tukae pamoja kuwa na mikakati ambayo itafanya adhma hiyo itimie pasipo vikwazo vyovyote,”amesema.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Temeke Dk. Joseph Kimaro amesema kumekuwa na maendeleo makubwa kwa MSD hasa katika kipindi hiki cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita.
“Lengo la kikao hiki ni kuimarisha ushirikiano katika utoaji huduma za afya ambapo inaenda sambamba na uwepo wa dawa na vifaa tiba ambapo kazi hiyo imepewa MSD ,”amesema