Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa amefafanua malalamiko yaliyotolewa kuhusu kuenguliwa kwa wagombea mbalimbali katika uchaguzi wa Serikali za Mtaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, mwaka huu.
Mchengerwa ameyasema hayo leo Novemba 16, 2024 jijini Dodoma wakati wa kuelezea mchakato wa uchukuaji, urejeshaji na uteuzi wa wagombea.
Alisema mwitikio wa vyama vya siasa katika shughuli ya kuchukua na kurejesha fomu za kugombea ulikuwa mzuri ambapo vyama vyote 19 vyenye usajili kamili vilijitokeza.
” Nafasi za mwenyekiti wa kijiji zinazogombewa ni 12,280 ambapo vyama 18 vya siasa viliweza kuweka wagombea katika nafasi 6,060 sawa na asilimia 49.35 ya nafasi hizo.
“Nafasi za mwenyekiti wa mtaa zinazogombewa ni 4,264 ambapo vyama 18 vya siasa viliweza kuweka wagombea katika nafasi 3,281 sawa na asilimia 76.94 ya nafasi hizo” amesema.
Ameongeza kuwa maeneo yatakayofanya uchaguzi tarehe 27 Novemba, 2024 kwa sasa ni vijiji 12,280 kutoka Vijiji 12,333 vilivyotangazwa hapo awali, mitaa 4,264 tofauti na mitaa 4,269 iliyotangazwa hapo awali.
Pia vitongoji 63,886 ukilinganisha na vitongiji 64,274 vilivyotangazwa kwenye gazeti la Serikali Tangazo Na.796 na 797 yote ya tarehe 06 Septemba, 2024.
Mabadiliko haya yemetokana na Halmashauri za Wilaya za Kaliua, Nsimbo na Tanganyika kuwa na makazi ya Wakimbizi ya Ulyankulu, Katumba na Mishamo, na wananchi kuhama kwenye baadhi ya vitongoji kutokana na sababu mbalimbali.
Amesema kuwa ameona ni muhimu kuweka idadi hii wazi ili kuupa umma taarifa ya hali halisi ya uchukuaji wa fomu za kugombea nafasi mbalimbali kwa vyama vyote vya siasa hata kabla ya malalamiko ya kuenguliwa kinyume na taratibu.
Akizungumzia rufaa, Mchengerwa Ofisi yake ilipokea malalamiko na kutoa muda kwa mgombea ambao hawakuridhika kukata rufaa.
Alisema taarifa kutoka katika halmashauri zote kati ya rufaa 16,309 zilipokelewa baada ya muda wa nyongeza wa siku mbili ni rufaa 5,589 zilizokubaliwa.
“Hii ilizingatia dosari ambazo zilisababisha kutoteuliwa kwao hazikuwa kubwa na ambazo haziathiri sheria na kanuni za uchaguzi.”
Hata hivyo, ametaja baadhi ya sababu zilizosababisha wengine kutoteuliwa ni kukosa sifa ya uraia Watanzania, kujidhamini wenyewe, kutojiandikisha kwenye Daftari la Wapigakura wa Serikali za Mitaa na wengine kuwa chini ya umri wa miaka 21.
Pamoja na hayo, amesema Ofisi ya Rais – TAMISEMI imefuatilia tuhuma zilizotolewa kwenye maeneo mbalimbali na kubaini hazikuwa na ukweli na zililenga kuleta taharuki na kuchafua mchakato wa uchaguzi unaoendelea vizuri.