Na Eleuteri Mangi,JamhuriMedia,Bunjumbura
Tanzania inashiriki Tamasha la Tano la Sanaa na Utamaduni la Jumuiya ya Afrika Mashariki (JAMAFEST) 2022 ambalo linafanyika nchini Bujumbura Burundi likiongozwa na Kaulimbiu “Kutumia Rasilimali za Kiutamaduni kukabiliana na Athari za UVIKO-19 kwa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki”.
Akifungua tamasha hilo Septemba 5, 2022 katika Uwanja wa Intwari Bujumbura nchini humo, Rais wa Jamhuri ya Burundi Evariste Ndayishimiye amewashukuru Wakuu wa nchi za jumuiya hiyo kufanikisha vikundi vya Utamaduni na Sanaa kushiriki Tamasha la JAMAFEST 2022 kwa mafanikio nchini Burundi.
“Tukio hili husaidia sio tu ubadilishanaji wa kisanii na kitamaduni, lakini pia hukuza ushirikiano wa kikanda. Kuweza kuandaa tamasha hili la Sanaa na Utamaduni nchini Burundi, ni dalili tosha kwamba UVIKO 19 ipo nyuma yetu ushahidi kwamba jumuiya yetu ni thabiti na kwa pamoja tunaweza kukabiliana na changamoto yoyote” amesema Rais Ndayishimiye.
Awali akiwakaribisha washiriki wa tamasha hilo Rais Mhe. Ndayishimiye, amesema kutoka nchi mbalimbali za Jumuiya ya Afrika Mashariki amesema wafurahie sio tu hewa ya Burundi, bali watafurahia madhari nzuri ya Ziwa Tanganyika, kula samaki aina ya mgebuka,dagaa na kuhe ambao wanapatikana katika ziwa Tanganyika.
Aidha, Rais Mhe. Ndayishimiye amesisitiza umuhimu wa Tamasha hilo na kusema kuwa linanaongeza kuimarisha umoja na muingiliano kati ya watu wa wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Tamasha la JAMAFEST linafanyika kwa mzunguko ambapo mwaka 2022 ni zamu ya nchini Burundi baada ya kufanyika tamasha la 4 kufanyika kwa mafaniko makubwa jijini Dar es Salaam 2019.