KABUL, AFGHANISTAN
Kitendo cha Marekani kuondoa majeshi yake nchini Afghanistan kumewaachia uhuru wanamgambo wa kundi la kigaidi la Taliban ambao wameanza kuiteka miji muhimu nchini humo.
Taarifa kutoka Afghanistan zinaeleza kuwa katika kipindi cha mwezi mmoja tu wanamgambo hao tayari watakuwa wameshaiteka nchi hiyo.
Wiki iliyopita walikuwa wanapambana kuukamata mji wa Kandahar ambao unatajwa kuwa ndio makao makuu ya kundi hilo. Walifukuzwa katika mji huo baada ya askari wa Marekani kuweka kambi nchini humo katika mpango wake wa kuhakikisha amani inatamalaki.
Hadi wiki iliyopita miji mikubwa katika majimbo 12 ilikuwa imeshaanguka mikononi mwa Taliban na kuufanya mji mkuu wa nchi hiyo, Kabul kuwa hatarini kuanguka kwa wanamgambo hao.
Jiji la Herat, la tatu kwa ukubwa nchini humo na mji mwingine mkubwa magharibi mwa Afghanistan, ilitekwa wiki iliyopita.
Wanamgambo hao walikamata maeneo muhimu katika miji hiyo zikiwamo ofisi za serikali na vituo vya polisi.
Mji mkuu wa Jimbo la Badghi lililopo kaskazini magharibi, Qala-I-Naw, nao ulitekwa Alhamisi iliyopita. Wanajeshi wa serikali katika mji huo walilazimika kukimbia baada ya kuzidiwa nguvu.
Mapema, mji wa Ghazni, ambao ni mji muhimu katika jimbo ukiunganisha na Jiji la Kabul, nao ulitekwa baada ya mapigano makali.
Msemaji wa Taliban alituma ujumbe wa tweeter Alhamisi jioni akisema kuwa mji huo ulikuwa umetekwa ikiwamo ofisi za gavana, makao makuu ya polisi na gereza.
Viongozi wengi wa serikali katika miji inayotekwa wanalazimika kujisalimisha kwa wanamgambo hao ambao wanaonekana kupata nguvu baada ya Marekani kuanza kuondoa majeshi yake nchini humo.
Kwa wiki kadhaa sasa Taliban wanaushambulia mji wa
Kandahar, kusini mwa nchi hiyo, kwa lengo ya kujitwalia makao makuu yao. Inaelezwa kuwa tayari wanamgambo hao wanashikilia robo tatu ya jiji hilo.
Baada ya luliteka gereza katika mji huo wanamgambo hao waliwaachia wafungwa 1,000, wengi wao wakiaminika kuwa askari wa kundi hilo waliokuwa wamekamatwa na kufungwa na serikali.
Baada ya kuuteka mji wa Ghazni, hivi sasa Taliban wanayadhibiti maeneo muhimu kaskazini na kusini mwa Kabul.