PANJSHIR, AFGHANISTAN
Wanamgambo wa Taliban wametafuna ng’ombe mzima ila mkia unataka kuwashinda. Mkia unaotaka kuwashinda upo katika ngome ya waasi iliyopo katika Mkoa wa Kaskazini wa Panjshir unaozungukwa na milima na mabonde.
Waasi wa Panjshir wameamua kupigana kufa au kupona kwa ajili ya kuulinda mji huo usiangukie mikononi mwa wanamgambo wa Taliban waliofanikiwa kudhibiti karibu miji yote ya Afghanstan.
Kutokana na mapigano makali kati ya pande hizo mbili kuibuka na kuendelea tangu wiki iliyopita, mamia ya familia wamekimbia.
Baadhi ya wakazi wa maeneo jirani ya Mkoa wa Parwan wanasema kwa siku kadhaa sasa maisha yao yanapiga ‘makitaimu’ kutokana na mapigano yaliyopamba moto kati ya wanamgambo hao na vikosi vya waasi vinavyoongozwa na Ahmad Massoud, ambaye ni mtoto wa Kamanda alieuawa, Ahmad Shah Massoud.
Wanamgambo hao wanasema juhudi za kufikia mwafaka kwa njia ya majadiliano zimeshindwa huku wakijiandaa kutangaza kuundwa kwa serikali mpya, ikiwa ni wiki chache tangu kutwaa madaraka.
“Mapigano yamekuwa mabaya zaidi na zaidi kila usiku,” anasema mkazi wa Mji wa Jab, Al-Seraj Asadullah (52).
Pia anasema licha ya mapigano hayo kujikita milimani, lakini wakazi wengi wa eneo hilo bado wanaendelea kukimbia eneo la Panjshir.
Huku familia zisizopungua 400 zimelazimika kukimbia vijiji vilivyoko kwenye barabara inayoelekea katika mabonde ya Panjshir yaliyopo umbali wa kilomita 125 kaskazini mwa Kabul.
Pia moshi uliotokana na makombora umeonekana ukitanda angani, ukitokea milima ya mbali wakati wana mgambo huo wakipambana kudhibiti mkoa wa mwisho kati ya mikoa 34 ya nchi hiyo.
Katika hatua nyingine, baadhi ya wakazi wanasema katika siku za kuanguka Serikali ya Kabul Agosti 15, mwaka huu waliona wanajeshi wa zamani wa Jeshi la Afghanistan kutoka mikoa ya Kunduz, Kapisa, Parwan na Takhar wakielekea Panjshir baada ya mikoa hiyo kuangukia mikononi mwa Taliban.
Wanasema wanajeshi hao walikuwa wanasafirisha magari ya kijeshi na vifaa vingine na kukiwa na taarifa chache kwenda na kutoka Panjshir, huku ikiwa ni vigumu kuhakiki madai hayo au kujua ni kiasi gani cha zana hizo zimetumiwa katika siku za karibuni.
Kama ilivyo ada, mapigano ya makundi hayo hasimu pia yameibua zahama kubwa kwa wanawake na watoto na kuwasababisha kukimbilia katika miji ya Parwan Charikar na Kabul.
Mkazi wa Syed Khil, Shah Rahman, anasema mke wake na watoto walikimbilia Kabul siku chache zilizopita na yeye ameamua kurudi asubuhi ya mwishoni mwa wiki iliyopita ili kukusanya vitu vyao na njiani akasimamishwa na wanamgambo hao.
“Wanakagua kitambulisho chako na usajili wa gari kuhakikisha unatokea Parwana, kisha wanakuachia kuingia,” anasema Shah.
Pia mkazi mwingine wa Parwan, Rahman Asadullah, anasema amesikia vifo vimetokea Panjshir, hata hivyo madai hayo hayakuthibitishwa na vyanzo huru, kwa sababu barabara ya kwenda Panjshir inaendelea kuzuiwa na mawasiliano ya simu yamekatwa tangu wiki iliyopita.
Anasema Panjshir na Parwan ikiwa ndiyo mikoa iliyokuwa salama zaidi nchini Afghanistan kwa muda mrefu, wakazi wanatatizwa zaidi na mapigano kuliko maeneo mengine ya nchi.
“Watu hawa hawajapitia mapigano ya kweli kwa miaka 20 na hawawezi kumudu kuwaona watoto wao wakilia usiku wakati risasi na maroketi vikinguruma,” anasema Asadullah.
Pamoja na mambo mengine, si mapigano tu yanayotokea umbali mfupi kutoka makazi yao yanayowazuia kuondoka nyumbani kwao pia kuna madai kwamba wanamgambo hao wanawashurutisha raia kukusanya maiti za wenzao waliokufa kutoka maeneo ya milimani.
“Wanajua kuna mabomu ya ardhini, hivyo wanawafanya watu wasio na hatia kukusanya maiti,” anasema mkazi mmoja.
Hata hivyo, wanamgambo hao wanakanusha madai ya wapiganaji wao kuwadhuru kwa makusudi raia huku wakisisitiza kuwa hatari ya kudhuru maisha ya raia ndiyo imewafanya kujizuia kushiriki vita kamili ya Panjshir.
“Hatutaki kuwadhuru raia, vinginevyo tungeingia kikamilifu na vita hii ingekuwa imekwisha kwisha ndani ya siku mbili, lakini hatutaki watu maskini na wasio na hatia kuteseka tena. Licha ya ahadi hizo, raia bado hawajihisi salama, hata katika maeneo yanayoizunguka Panjshir,” anasema mmoja wa wanamgambo hao.
Ingawa Panjshir ni ngome ya muda mrefu ya Massoud mkubwa, wakati wa ukaliaji wa majeshi ya Sovieti na upinzani wake dhidi ya utawala wa Taliban katika miaka ya 1990, wakazi wa Parwan wanasema wanataka kukomesha mapigano.
“Pande zote zinazungumzia Quran na wanasema ni Waislamu, lakini wanafanya nini, kuua Waislamu wengine! Hii lazima ikome,” anasema Shir Agha (30).
Kwa wakazi wanaobakia Jab al-Seraj, wanasema maeneo yao yanayotegemea zaidi utalii wa ndani katika Bonde la Panjshir yanapambana kutokana na kufungwa kwa bonde hilo na ukosefu wa huduma za kibenki nchini kote.
Kwa upande wa Mji wa Charikar, nao unateseka kutokana na ukosefu wa fedha taslimu, wakati benki zikipambana kurudisha huduma zake tangu wanamgambo hao walipotwaa madaraka.
Naye Habib Golbahar anasema kuhamisha familia yake kutamgharimu fedha kidogo alizoweka akiba huku watu wa Parwan wanapambana kutafuta hata dola 1.13 za Marekani.
Pia anasema ofisi nyingi za serikali na binafsi zikiwa bado zimefungwa huku uchumi na utalii ukishuka, ni hatari sawa na kama si zaidi ya vita yenyewe.
“Wanaweza kupigana kwa miaka mingine 10 wakiuawana lakini sote tutakufa kwa njaa kabla ya hapo,” anasema Habib.