Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (TALGWU) Mkoa wa Dar es Salaam, Ibrahim Zambi, ameiomba Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuwabadilishia mishahara wanachama wake waliopandishwa madaraja katika mkoa huo.
Zambi amedai tangu mwezi Juni mwaka huu wanachama wake katika wilaya zote za Mkoa wa Dar es Salaam ambao wamepandishwa madaraja hawajabadilishiwa mishahara yao kama ambavyo sheria inataka.
Amesema kutokana na hali hiyo, wengi wao wamekuwa wakiishi kwa shida na sintofahamu kuhusu hatima ya mishahara yao.
Amesema kuwa kwa kawaida mtumishi wa serikali akipandishwa daraja anatakiwa kubadilishiwa mshahara wake kulingana na daraja jipya alilopo, lakini baadhi ya wafanyakazi mkoani humo wamekaa miezi miwili bila ya kubadilishiwa mishahara yao baada ya kupandishwa madaraja.
Amesema mbali na madai ya kupandishwa madaraja bado kuna baadhi ya wanachama katika mikoa yote kwa muda mrefu sasa wanadai malimbikizo ya malipo ya likizo, kufanya kazi muda wa ziada, nauli, masomo na usafiri.
Amesema ingawa hana takwimu sahihi kuhusiana na kiasi cha fedha ambacho watumishi hao wanastahili kulipwa, lakini madai hayo yanahusu watumishi 1,866 ambao wamepandishwa madaraja.
Zambi amesema malimbikizo mengi ya madai hayo yapo katika kada ya afya.
Ameongeza kuwa changamoto nyingine na kubwa kwa sasa miongoni mwa wanachama wake ni vitisho kutoka kwa viongozi, hasa wanasiasa.
Amesema watumishi wengi hawafanyi kazi kwa uhuru na ufasaha kwa kuwa wamezingirwa na woga unaotokana na kutishwa na kufokewa na viongozi ambao kimsingi si wasimamizi wao kazini.
Amesema kutokana na wimbi kubwa la wanasiasa wanaoingilia majukumu ya watendaji na wataalamu, watumishi wengi wamekuwa wakifanya uamuzi wa masuala muhimu kwa woga.
“Kitendo cha wataalamu hao kuingiliwa mara kwa mara na wanasiasa kimesababisha wafanye kazi kwa woga na shaka, wakihofia kuharibiwa kazi na wanasiasa hao,” amesema.
Katibu huyo pia alimwomba Rais John Magufuli kuona huruma na kuwarejesha kazini wanachama wake 80 ambao waliondolewa kazini kwa kigezo cha kutotimiza masharti ya kuwa na elimu ya kidato cha nne wakati walipoingia kwenye ajira mwaka 2004.
Zambi amesema kabla ya kuingia katika ajira ya serikali wanachama hao kwa pamoja walipewa barua kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii wakati huo, ikiwataka kuendelea na kazi kama kawaida bila kuwa na pingamizi la ulazima wa kumaliza kidato cha nne.
“Barua ninayo kabisa hapa ofisini iliyowataka watumishi hao kuingia katika ajira bila vigezo vya kufika sekondari,” amesema Zambi.