Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa Tanzania (Takukuru) imepanga kuzikomalia timu za Yanga, Azam na Simba zenye nafasi ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) hili kudhibiti upangaji matokeo katika mechi za mwisho wa msimu huu.
Timu hizo ambazo zinashika nafasi za juu katika msimamo wa ligi hiyo zimekuwa walengwa wakubwa katika kudhibiti kupanga matokeo kutokana na kuwa ndiyo timu zinazotanzamiwa zaidi kutwaa ubingwa.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Ligi, Fatuma Abdallah, anasema wamegundua kuwa Ligi inapofikia mwishoni kuna kuwa na matukio ya utata hasa yanayohusishwa zaidi na upangaji wa matokeo, kutokana na hilo tumeamua kulikazia kamba zaidi msimu huu ili kudhibiti tatizo hilo ili kupata matokeo ya halali bila utatanishi.
Anaendelea, “Tumekuwa tukifanya kazi na Takukuru tangu mwanzo mwa msimu na Takukuru walikuwa wakiifanya kazi hiyo, lakini katika kipindi hiki wameamua kuongeza nguvu zaidi kwa kuwa ndicho cha hatari zaidi kufanyika matukio hayo.”
Anasema uchunguzi wao unaegemea timu ambazo zinafanya hujuma katika Ligi ikiwa ni pamoja na kutoa rushwa, madai ambayo yamekuwa yakijadiliwa zaidi na wadau wa soka.
“Sasa tumeongeza nguvu, hasa katika zile timu tatu za juu kwani hizo zinaweza kufanya vitendo vibaya ili waweze kutwaa ubingwa,” anasema Fatuma.
Pia alitoa wito kwa timu zote zinazoshiriki Ligi hiyo kufuata kanuni na sheria bila kufanya kitendo chochote kitakachowaingiza matatani kutokana.
Ikiwa ligi imebakisha angalau mizunguko mitano kumalizika msimu huu wa 2014/2015 hadi sasa Yanga ndiyo kinara kwa kufikisha pointi 40 ikifuatiwa na Azam yenye pointi 36 huku Simba ikishika tatu kwa ponti 32.