Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Tabora

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilayani Sikonge Mkoani hapa imeagizwa kufanya uchunguzi wa kina kwenye mradi wa afya Tutuo unaotekelezwa kwa fedha za serikali kiasi cha sh mil 250.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Sahili Nyanzabara alitoa agizo hilo wakati mwenge huo ulipotembelea na kukagua utekelezaji mradi huo ili kuuwekea jiwe la msingi.

Alisema mradi huo ni mzuri lakini utekelezaji wake umegubikwa na kasoro nyingi za kiutendaji ambazo haziendani na uhalisia wake, pia mkandarasi ameshindwa kumaliza kazi kwa wakati licha ya kuomba kuongezewa muda.

Mkuu wa Wilaya ya Sikonge Mkoani Tabora John Ernest Pallingo akitoa taarifa ya mradi wa ujenzi Kituo cha afya Tutuo kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Sahili Nyanzabara hapo

Alibainisha kasoro nyingine kuwa ni uwepo wa nyufa katika baadhi ya kuta, kutoonekana kwa baadhi ya nyaraka zikiwemo za manunuzi ya vifaa jambo lilipelekea kutiliwa shaka na Kiongozi huyo.

‘Katika taarifa yenu mmeandika kwamba mradi umekamilika kwa asilimia 100, lakini baadhi ya vyumba havijakamilika hadi sasa ikiwemo kuwekwa marumaru sakafuni, mna mdanganya nani?’, alisema.

Alisema kuna baadhi ya halmashauri zilipewa kiasi kama hicho cha fedha na zimeweza kujenga majengo 3 ya maabara, OPD na kichomea taka, na yamekamilika kwa asilimia 100, lakini ninyi hata majengo 2 hayajakamilika.

Nyanzabara alibainisha kuwa serikali inadhamira njema kuwasaidia wananchi wake, lakini baadhi ya wataalamu hawapo makini kuisaidia ikiwemo kutekeleza wajibu wao ipasavyo.

Alisisitiza kuwa kuwa ni kosa kubwa kwa mtendaji yeyote wa serikali aliyepewa dhamana halafu asifanye kile serikali inachotaka, mtu kama huyo hafai hata kidogo na haitakii mema serikali iliyoko madarakani.

Aliagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kupitia nyaraka zote za mradi huo ili kujiridhisha nani kazembe wapi ili hatua zichukuliwe